Wednesday, September 19, 2018

KAMPUNI YA MOHAMMED OMAR BIN HAIDER HOLDING GROUP –MOBH IMETIA SAINI MKATABA WA MAKUBALIANO YA KUUNGA MKONO JITIHADA ZA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR KATIKA MASUALA YA KUIMARISHA UWEKEZAJI.


452
Mkurugenzi wa Bodi akiwa pia Meneja Mkuu wa Kampuni ya Mohammed Omar Bin Haider Holding Group (MOBH) , Bwana Omar Mohammad Bin Haider Kulia akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kabla ya utiaji saini Mkataba wa Makubalizno ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala ya kuimarisha Uwekezaji.
470
Waziri wa Fedha wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohamed kulia na Mkurugenzi wa Bodi akiwa na Meneja Mkuu wa  Kampuni ya Mohammed Omar Bin Haider Holding Group -MOBH, Bwana Omar Mohammad Bin Haider, wakiwa katika Hoteli ya Kimataifa ya Grand Exelsior iliyopo katika mji wa Al – Brsha Dubai  wakitia saini mkataba wa makubaliano ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala ya kuimarisha uwekezaji.
Wa kwanza kutoka Kulia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akishuhudia tukio hilo la Kihistoria kwa Zanzibar katika harakati za kunyanyua uchumi wake.
478
Dr. Khalid Kulia na Bwana Omar Mohammad Bin Haider wakibadilishana hati ya Mkataba mara baada ya kuusaini  wa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala ya kuimarisha Uwekezaji.
482
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kulia akimpongeza Meneja Mkuu wa  Kampuni hiyo Bwana Omar Mohammad Bin Haider baada ya kukamilisha zoezi la kutia saini, Waziri wa Fedha wa Zanzibar Dr. Khalid kati kati akishuhudia.
491
Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dr., Khalid Salum Mohamed akitoa Hotuba katika chakula Maalum cha Mchana kilichoandaliwa na Kampuni Bwana Omar Mohammad Bin Haider mara baada ya kumalizika kwa hafla ya utiaji saini.
505
Kampuni ya MOBH Holding Group Bwana Omar Mohammad Bin Haider mwenye  Kilemba katikati kulia yake Balozi Seif na kushoto yake Dr. Khalid wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi na watendaji wa Kampuni hiyo na Wanabalozi wa Tanzania nchini Dubai  mara
baada ya kukamilika kwa zoezi la utiaji saini.
Safari ya Zanzibar kuelekea katika mtazamo wa matarajio ya kuwa Dubai ya Afrika Mashariki inaanza kuchipua  kufuatia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutiliana saini Mkataba na Kampuni ya Kimataifa ya Mohammed Omar Bin Haider Holding Group (MOBH ) ya Nchini Dubai.
Saini ya Mkataba huo ilitiwa baina ya Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohamed ambaye alitia saini hiyo kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati Bwana Omar Mohammad Bin Haider wa Kampuni ya Mohammed Omar Bin Haider Holding Group ilitiwa na Mkurugenzi wa Bodi akiwa pia Meneja Mkuu wa  Kampuni hiyo Bwana Omar Mohammad Bin Haide, hafla iliyofanyika katika Hoteli ya Kimataifa ya Grand Exelsior Mjini Al Barsha Nchini Dubai, imelenga kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala ya kuimarisha uwekezaji na maendeleo ya Zanzibar Kiuchumi.
Hafla hiyo ilishuhudiwa pia na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyetokea Nchini China kuhudhuria Maonyesho ya 15 ya Kimataifa ya China- Asean Expo 2018 yaliyofanyika katika Mji wa
Nanning katika Jimbo la Guangxi.
Akizungumza mara baada ya utiaji saini mkataba huo Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohamed alisema Zanzibar imeahidi na kuwa tayari kuiona Kampuni hiyo yenye Makao Makuu yake Nchini Dubai inazitumia furza za Uwekezaji zilizopo Visiwani Zanzibar ambapo  ndipo palipokuwa kitovu cha harakati za Kibiashara kilichokuwa kikiunganisha Bara la Asia na Ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Bara la Afrika lenye wakaazi zaidi ya Milioni 360,000,000, kwa  hivi sasa imepania kuirejeshea hadhi yake kwa kutanua maeneo mengine ya Uwekezaji.
Aisema Miundombinu iliyoimarishwa katika Sekta za Mawasiliano ya Anga, Uvuvi wa Bahari Kuu, Utalii na Biashara ikiambatana na Sera inayotekelezeka imezingatia kuwajengea mazingira bora awekezaji wa Ndani na Nje kuwekeza Miradi yao katika mfumo wa makubaliano ukiwemo ule wa Ubia.  “ Tunakaribisha wawekezaji wa kigeni zaidi katika kusaidia kuimarisha uchumi wa Zanzibar hasa katika sekta ya Utalii inayounganishwa hivi sasa na safari za moja kwa moja za anga kutoka maeneo mbalimbali ya Dunia”. Alisema  Dr. Khalid Salum.
Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar aliueleza uongozi huo wa Kampuni ya MOHB Holding Group kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika juhudi za kuimarisha Uchumi wake imeanzisha maeneo mengine ya uwekezaji ili kutanua wigo wa uchumi wake ambayo ni mradi mpya wa utafiti wa Mafuta na Gesi  Asilia unaoendelea pamoja na matayarisho ya ujenzi wa Bandari ya Mizigo ya Mpiga Duri maeneo ambayo Kampuni hiyo inaweza kufikiria namna ya kusaidia kwake.
Alisema Dira ya Maendeleo ya 2025 na Mpango wa Maendeleo 2020 imelenga kuinyanyua Zanzibar kiuchumi ili wananchi wake wafikie hatua ya ustawi uliotukuka, mipango ambayo inayohusishwa pia na Taasisi, Mataifa na Mashirika ya Maendeleo ya ndani na nje ya Nchi.
Dr. Khalid alifahamisha kwamba Kampuni ya Mohammed Omar Bin Haider Holding Group kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu uliyonayo na mtandao mzuri wa uwekezaji bado wana fursa ya kuangalia maeneo zaidi wanayoweza kufikiria kuwekeza Zanzibar.
Aidha Uongozi wa Kampuni hiyo umeridhika na ukarimu mkubwa walionao Watu wa Visiwa vya Zanzibar wakati wa ziara ya ujumbe huo uliyoifanya Zanzibar mwishoni mwa Mwezi Agosti 2018 ambao umeshawishika kutaka kuwekeza miradi yao ya kiuchumi Visiwani Zanzibar.
Katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye uimarishaji wa Uchumi wake Taasisi hiyo ya Uwekezaji imeonyesha nia ya kuwasilisha maombi yake ya kutaka kuwekeza miradi katika sekta mbalimbali zikiwemo za Mawasiliano, uvuvi wa Bahari Kuu, Kilimo pamoja na Viwanda.
Kampuni ya MOHB Holding Group yenye Makampuni  tofauti zaidi ya Sita katika Mataifa mbali mbali ya Mashariki ya Kati  inajishughulisha zaidi na Miradi  mbali mbali ya Ujenzi wa Miji ya Kisasa, Huduma za Afya, Elimu, Miundombinu, Biashara pamoja na Sekta ya Utalii.
Muungano wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE) imewekeza Nchini Tanzania Miradi mbali mbali ya Kiuchumi inayokadiriwa kuwa na gharama ya Dola za Kimarekani Milioni 991 kuanzia Mwaka 2003.
                              
            Habari na Picha kwa hisani ya:-
Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Ofisi ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki-Zanzibar.
19/09/2018.

No comments :

Post a Comment