Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
JUMLA YA VIWANDA 1,596 VIMEJENGWA NCHINI-MAJALIWA
*Asema ni utekelezaji wa agizo la ujenzi wa viwanda 100 katika kila mkoa
WAZIRI MKUU,
Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia Juni, 2018 jumla ya viwanda 1,596
vimejengwa ambapo ni sawa na asilimia 61.4 ya lengo la kujenga viwanda
2,600 hadi Desemba 31, 2018 ikiwa ni utekelezaji wa agizo la ujenzi wa
viwanda 100 katika kila mkoa.
Ameyasema hayo
leo (Alhamisi, Septemba 27, 2018) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 34 wa
Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), kwa niaba ya Rais Dkt. John
Magufuli. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Jakaya Mrisho
Kikwete, jijini Dodoma.
Waziri Mkuu
amesema kuwa viwanda hivyo vimejengwa kupitia agizo la Waziri wa Nchi
OR- TAMISEMI kwamba kila Mkoa ujenge viwanda 100.
Amesema tathmini
ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali kuelekea uchumi wa viwanda,
inaonesha kwamba mpaka sasa jumla ya hekta 367,077 zimetengwa katika
Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya viwanda vikubwa, viwanda vya
kati na viwanda vidogo.
“Nitoe wito kwenu
kwamba mwendelee kupiga hatua nyingine mbele zaidi katika hili, tujue
katika hekta hizo zilizotajwa ni kiasi gani kimerasimishwa kwa viwanda
vipi, bidhaa zipi zinazalishwa, hali ya miundombinu ikoje na kuna
mikakati gani ya kuiendeleza. Pia tufahamu ni ajira ngapi zilizozalishwa
kutokana na uanzishwaji wa viwanda hivyo.”
Kadhalika, Waziri
Mkuu amewaagiza viongozi na wasimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa
kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili kuwawezesha wananchi kushiriki
katika kubuni na kusimamia miradi ya maendeleo na kuibua fursa za
uwekezaji.
Pia kuanzisha na
kuendeleza viwanda vidogo na vikubwa ili Tanzania iweze kufikia lengo la
kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. “Tumieni asilimia 10 ya
mapato ya ndani ya Halmashauri kuwawezesha wanawake, vijana na watu
wenye ulemavu kupitia vikundi vyao ili wawekeze katika viwanda vidogo
vidogo vyenye kuleta tija na kuongeza pato la kaya ili kuutokomeza
umaskini.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali katika Dira ya Maendeleo
ya 2025 ni kuhakikisha Halmashauri zinakuwa na uwezo wa kujitegemea
kimapato kwa zaidi ya asilimia 80 ifikapo 2025.
Amesema Serikali
ya Awamu ya Tano imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha
lengo hilo linatimia. Serikali imeanzisha utaratibu wa kugharamia miradi
ya kimkakati yenye lengo la kuziongezea halmashauri mapato ya uhakika
na kupunguza utegemezi wa ruzuku.
“Hadi sasa, sh.
bilioni 131.5 zimeidhinishwa kutekeleza miradi ipatayo 22 katika
halmashauri 17 zilizokidhi vigezo kwenye mikoa 10. Hivi ninavyozungumza,
tayari kiasi cha sh. bilioni 16.4 zimekwishapelekwa kwenye halmashauri
hizo kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi iliyokusudiwa.”
Waziri Mkuu
amesema kuwa uchambuzi wa miradi mingine zaidi unaendelea na halmashauri
zitakazokidhi vigezo zitapata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
hiyo.
Amesisitiza
kwamba fedha hizo zikatumike kwa ajili ya malengo yaliyokusudiwa na si
vinginevyo. Amesema kwa sasa, hatutakuwa na utaratibu wa kutoa fedha
bila kufahamu kwa kina fedha hizo zinakwenda kufanya nini na zitaleta
mabadiliko gani.
“Nimesikia kwamba
katika baadhi ya halmashauri fedha zilizokwishatolewa bado hazijaanza
kutumika kikamilifu watu wanaendelea kujadili namna ya kuzitumia,
niwakumbushe tu kwamba Mheshimiwa Rais hakutoa fedha hizo ili zikakae
benki. Wakurugenzi wa Halmashauri mlisaini makubaliano ya matumizi ya
fedha hizo, hivyo, zingatieni hilo.”
Waziri Mkuu
amewataka Madiwani wasimamie matumizi ya fedha hizo ili halmashauri
zipate miradi yenye ubora unaotakiwa, inayolingana na kiasi cha fedha
kilichotolewa pamoja na inayokamilika kwa wakati.
Kauli mbiu ya Mkutano huo wa 34 inasema “Umuhimu
wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Kutoa Huduma na Ushiriki wa
Wananchi Kupitia Fursa na Vikwazo Kuelekea Uchumi wa Viwanda”.
Amesema kauli
mbiu hiyo, inatilia mkazo maneno ya awali ya Rais Dkt. Magufuli, kwamba
Mamlaka za Serikali za Mitaa zipo karibu zaidi na wananchi na zinapaswa
kutoa huduma na kuwashirikisha wananchi katika kujiletea maendeleo ya
kiuchumi na kijamii.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 980,
41193 – Dodoma
ALHAMISI, SEPTEMBA 27, 2018.
No comments :
Post a Comment