Kufuatia Ofisi ya Rais, TAMISEMI
kuwapangia jumla ya walimu 4,840 vituo vya kazi kwenye Shule za Msingi
na Sekondari nchini, Katibu Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Walimu,
Bibi Winifrida Rutaindurwa amewataka waajiriwa hao kuzingatia kanuni na
taratibu zinazosimamia utumishi wa walimu ili kujiepusha na makosa ya
kinidhamu.
Amesema kuwa, kumekuwa na mazoea
kwa walimu wengi kusaini nyaraka wanazopewa wakati wa kuanza ajira bila
kuzisoma kitu kinachosababisha kutoelewa kanuni na taratibu za
taaluma
ya ualimu katika utumishi wa Umma.
“Wapo walimu wengi ambao
wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu na wengine wamejikuta
wakipoteza ajira zao kwa sababu ya kwenda kinyume na Sheria, Kanuni na
Taratibu za Utumishi wa Walimu pamoja na zile zinazoongoza Utumishi wa
Umma” amesema Bibi Rutaindurwa.
Amefafanua kuwa,
Mwajiriwa atakaporipoti kwenye Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya yenye
Shule aliyopangiwa, atapewa mkataba wa ajira ulioandaliwa na Tume ya
Utumishi wa Walimu. Mwajiriwa anatakiwa kusoma mkataba huo pamoja na
viambatisho vyake ili aweze kujua haki na wajibu katika utumishi wake.
“Mara nyingi walimu
wanapoajiriwa, wengi wao wanasaini mikataba ya ajira bila kuisoma na
kuelewa. Sasa naelekeza kuwa, kila Mwalimu ahakikishe anasoma mkataba
wake na anauelewa vizuri kabla hajausaini ili kujua kwa undani kile
anachotakiwa kufanya katika utumishi wake” amesema Bibi Rutaindurwa.
Ameongeza kuwa, waajiriwa
wanapaswa kusoma Sheria ya Utumishi wa Walimu ya mwaka 2015, Kanuni
pamoja na Miongozo mingine ambayo inapatikana katika tovuti ya Tume ya
Utumishi wa Walimu kupitia www.tsc.go.tz.
Wakati huo huo, Bibi Rutaindurwa
amewataka Kaimu Katibu Wasaidizi Wilaya zote kuhakikisha wanatoa
ufafanuzi wa mikataba pamoja na kuwaelimisha walimu walioajiriwa masuala
mbalimbali yanayohusu ajira zao kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya
Utumishi wa Walimu na. 25 ya mwaka 2015.
Ameelekeza kuwa, baada ya mwalimu
kukamilisha taratibu zote za kiutumishi, Kaimu Katibu Wasaidizi watoe
barua za ajira kwa waajiriwa wapya kwa wakati bila kuweka urasimu
unaoleta usumbufu.
Ameongeza kuwa, hatamvumila
Mtendaji yeyote wa Tume ya Utumishi wa Walimu ambaye atafanya uzembe au
kuchelewesha barua za ajira kwa Walimu bila sababu za msingi.
“Mwalimu anapokamilisha
kujaza nyaraka za ajira yake apewe barua ya ajira, bila urasimu wowote
ili aanze kutekeleza majukumu yake kwa haraka. Sitaki kusikia mwalimu
amechelewa kupata barua ya ajira au kuna mtumishi wa Tume analeta
urasimu kinyume na taratibu, kwa kweli sitamvumilia” amesema Bibi Rutaindurwa.
Vilevile, amewakumbusha Walimu
Wakuu na Wakuu wa Shule kuwashauri na kuwaelimisha walimu juu ya kanuni
na taratibu za kiutumishi badala ya kukaa na kusubiri wafanye makosa ili
wawachukulie hatua za kinidhamu.
Kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya
Utumishi wa Walimu ya mwaka 2015, Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule ndio
mamlaka ya kwanza ya nidhamu kwa mwalimu. Hivyo, walimu wanapaswa
kuzingatia matakwa ya Sheria na Kanuni za Utumishi wa Walimu na zile za
Utumishi wa Umma.
Adili Mhina,
Afisa Mawasiliano,
Tume ya Utumishi wa Walimu.
22/07/2018.
No comments :
Post a Comment