Tuesday, July 17, 2018

Mjue mwanafunzi anayetengeneza mvinyo kwa kutumia karoti

PichaKIGALI, Rwanda
MWANAFUNZI wa taasisi iitwayo Independent Institute of Lay Adventist of Kigali (INILAK), Marc Niyigeza amepata umaarufu baada ya kufanikiwa kutengeneza kinywaji cha mvinyo kwa kutumia karoti.

Kijana huyo aliyetumia msimu wa karoti kubuni wazo la kutengeneza kinywaji hicho, anatengeneza lita 100 hadi 200 za mvinyo kwa mwezi, akitumia uwepo wa karoti nyingi kwa sababu ni kipindi cha mavuno. Niyigeza alisema katika msimu wa mavuno ya karoti hasa mwezi Mei, mazao mengi yanaharibika kutokana na mazao huwa mengi kuliko mahitaji.
Alisema kutokana na hali hiyo, aliamua kuongeza thamani ya karoti hizo kwa kutengeneza mvinyo, unaopendwa na wananchi wengi nchini Rwanda. “Wazo la kuongeza thamani ya karoti hizo lilinijia wakati wa mavuno baada ya kuona mazao mengi ya karoti yanatupwa baada ya kuharibika.
Nilianza na miradi miwili, wa kwanza ni kutengeneza mvinyo, lakini wa pili ni kukausha karoti na kutengeneza unga kama njia mojawapo ya utunzaji wa karoti,” alisema kijana huyo.
Kijana huyo mbunifu mwenye umri wa miaka 30 kutoka wilaya ya Kirehe, anasoma kozi ya Biashara na Masoko. Aliungana na mwanafunzi mwenzie wa chuo hicho anayesoma Sayansi ya Chakula ili kuimarisha mradi wake na kuanza kuzalisha Februari 2018. Baada ya wazo lake kukamilika, aliamua kuagiza mashine ya kumsaidia kusaga karoti ili kupata juisi inayotakiwa ili kutengeneza mvinyo.
“Niliagiza mashine kwa bei rahisi kutoka China iliyogharimu Faranga 200,000 na vifaa vingine vichache na kuanza kuzalisha mvinyo kwa faida kubwa,” alisema Niyigeza. Baada ya kufanikiwa kutengeneza mvinyo, kijana huyo aliamua kupanua biashara yake kwa kuimarisha kiwanda, ambapo alianza kufanya kazi na wakulima wengi wa karoti na kuwapa soko la mazao yao.
Alisema ingawa kiwanda chake kipo katika hatua za mwanzo, lakini uzalishaji wake unaridhisha kwani ameweza kuzalisha lita za mvinyo kuanzia 100 hadi 200 kwa mwezi kutegemea na mahitaji ya soko. Kila chupa ya ujazo wa lita 33, inauzwa kwa faranga za Rwanda 2,500 wakati chupa moja yenye ujazo wa lita 75 inauzwa kwa Faranga za Rwanda 5,000.
“Mvinyo tunaozalisha tumeanza kuuza katika maduka makubwa na katika baa. Nilipoanza kuzalisha mvinyo niliajiri wafanyakazi 10 waliolipwa kila mmoja Faranga za Rwanda 2,500 kila siku,” alisema.
Aliongeza kuwa aliwaajiri wataalamu wa mvinyo, waliokuwa na jukumu la kuhakikisha ubora wa bidhaa yake na alikuwa akiwalipa kila mmoja Faranga za Rwanda 5,000 kwa siku kila siku.
Ubunifu wa kijana huyo umekuwa neema kwa wakulima wengi nchini Rwanda wanaolima karoti, kwani wamekuwa wakimuuzia magunia kwa magunia kulingana na uzalishaji wao. Kwa mujibu wa kijana huyo, kilo moja ya karoti ananunua kwa faranga 500 wakati wa msimu wa mavuno na faranga 700 wakati wa shida ya karoti.

No comments :

Post a Comment