Na Emmanuel J. Shilatu
Leo ni Julai 25 siku ya Maadhimisho ya Mashujaa waliopambana kwa hali
na mali kutetea nchi yetu ya Tanzania katika maeneo mbalimbali.
Hawa walimea uzalendo mkubwa, mwili na nafsi zao walikubali kuviweka
rehani kwa ajili ya Tanzania. Bado tunawakumbuka na kuwaombea kheri
kutokana na kujali na kudumisha misingi ya amani.
Misingi mizuri iliyojengwa na waasisi wa Taifa, Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume , imesababisha
Wananchi wa Tanzania kwa muda mrefu kuishi kwa amani na utulivu, huku
wakifanya mambo yao kwa uhuru bila ya kuingiliwa na mtu yeyote wa ndani
ama wa nje.
Tofauti na mataifa mengine, Watanzania wako huru zaidi kwenda kokote
wanakotaka na hata kuishi ama kufanya kazi au biashara bila ya bughudha
yeyote endapo kanuni, taratibu na sheria za nchi zitafuatwa ama
kuzingatiwa vyema. Hali hiyo ni tofauti kabisa na nchi nyingine zikiwamo
zile za jirani zetu kama Kenya, Rwanda, Burundi, Kongo na hata Uganda,
nchi ambazo kwa kiasi kikubwa ukabila na chokochoko za kisiasa
zimetamalaki kuanzia ngazi za kijiji hadi Taifa. Hapa kwetu tumeishi
kama Ndugu bila ya u-rangi, udini, ukabila wala harakati za kiitikadi na
kisiasa kutugawa.
Jambo la kushangaza ni kuwa misingi hiyo ya amani na utulivu
iliyogharamikiwa na Waasisi wetu, hivi sasa ipo shakani na hatarini
kutoweka kwani ilishaanza kuchezewa na chokochoko za aina mpya ya siasa
(kwa maana ya ukosefu wa uvumilivu na uchu wa madaraka) iliyoanza
kurindima katika siku za hivi karibuni.
Tukiwa tunawakumbuka Mashujaa hao inabidi nasi tujitathmini nafasi yetu
kwa Taifa letu endapo inaedana na hali ya uzalendo. Hali ilivyo sasa
kiwango cha uzalendo kimeshuka sana. Mtu yupo radhi kulalamika na kudai
haki pasipo kutimiza wajibu wake kwa Taifa. Wameshajiuliza, wamelifanyia
nini Taifa kabla ya kudai haki?
Vijana walio wengi wameweka pembeni uzalendo wa kulipenda Taifa lao
kiasi cha kufikia hatua ya kukufuru kwa maneno ya kashfa dhidi ya Taifa
lao. Hali hiyo ni tofauti kabisa na mataifa mengine ambayo hatuoni
wakiyakashifu mataifa yao hadharani. Hii tabia ya kujivua nguo hadharani
ni kwa faida ya nani?
Hapo hapo utakuta kuna baadhi ya Watanzania wanenda nchi za kimataifa
na kuanza kuikashfu nchi yao kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya
habari vya kimataifa. Laiti kama Wazee wetu waliotutangulia wangekuwa na
akili mbovu kama hizi, leo hii sidhani kama tungelikuta Taifa hili
likiwa salama kama lilivyo. Umejiuliza haya ya kulichafua Taifa letu
unataka uache urithi gani kwa vizazi vijavyo kwa Taifa letu?
Vijana wengi wa Leo, wananyooshewa vidole kwa kutothamini tunu ya kuwa
Mtanzania. Je, U-Miongoni mwao? Kwako uzalendo ni nini? Kwako amani
unailindaje?
Ndugu zangu, Wapo wanaosema kuwa amani ni sawa na yai mkononi,
ukilivunja hautaweza kuliunganisha kamwe; wengine wanasema kuwa amani
haina bei na ikipotea haina soko la kununua. Tuitunze amani yetu na
kamwe tusiizoee wala kuichoka, tuige uzalendo waliokuwa nao Mashujaa
wetu ambao walihakikisha amani ya nchi wanailinda vilivyo kwa machozi,
jasho na damu.
*Shilatu E.J*
0767488622

No comments :
Post a Comment