Na Jonas Kamaleki
Matumaini ya wananachi wa wilaya
za Ulanga, Malinyi na Kilombero ya kijamii na kiuchumi yarejea baada ya
Daraja la Magufuli kujengwa na kuzinduliwa.
Kipindi cha zaidi ya miongo
mitano ya adha, bughudha, mateso na hata watu kupoteza maisha kimeisha
baada juhudi za makusudi za Serikali ya Awamu ya Tano kukamilisha ujenzi
wa
daraja lenye urefu wa mita 384 kwenye mto wa Kilombero.
Usafirishaji wa mazao kati ya
wilaya za Ulanga, Malinyi na Kilombero hadi Morogoro ilikuwa ni shida
kwani njia pekee ilikuwa ni ya kutumia kivuko ambacho hakikuwa na
uhakika. Suala hili liliathiri sana uchumi wa watu wa maeneo hayo na
kuwafanya waishi maisha ya kimaskini huku wakiwa na mchele na mazao
mengine ya kilimo yasiyo na soko.
Baada ya Rais Magufuli kuzindua
daraja la mto Kilombero ambalo limepewa jina la Magufuli, wananchi wa
wilaya ya Ulanga, Malinyi na Kilombero wameishukuru Serikali ya Awamu ya
Tano kwa kutimiza ahadi waliyoitoa kwa wananchi hao ya kuwajengea
daraja la mto Kilombero ambalo lilikuwa kilio chao cha muda mrefu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
katika kijiji cha Kivukoni, mkoani Morogoro, wakazi hao wamesema kuwa
hivi sasa changamoto zao zimetatuliwa baada ya kukamilika kwa daraja
hilo.“Tunaishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja hili kwani limekuwa
mkombozi kwetu wananchi wa wilaya za Ulanga na Kilombero kwani hapo
nyuma vifo vingi vimetokea pasipo kutegemewa wakati tukitumia kivuko
kufuata huduma za kijamii wilaya jirani ambapo ndio kuna huduma zote za
muhimu”, amesema Bi. Zainabu Mtalanga.
Kujenga daraja ni suala moja na
utunzaji wa daraja hilo ni suala jingine. Kwa mukhtadha huo, Waziri
mwenye dhamana ya Ujenzi, Prof. Mbarawa anatoa wito kwa wananchi hao
kulilinda daraja hilo kwa kutojihusisha na vitendo vya kuchimba kokoto
chini ya daraja, kuiba alama za barabarani na kuacha kupitisha mifugo
juu ya daraja kwani Serikali imetumia gharama kubwa kujenga daraja hilo
na barabara unganishi katika eneo hilo.
Daraja hilo ambalo limezinduliwa
na Rais Magufuli wiki iliyopita (tarehe 05 Mei, 2018) limejengwa pamoja
na barabara zake zenye urefu wa kilometa 9.142 kwa gharama ya Shilingi
Bilioni 61.133 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.
Kutokana na juhudi za Rais
Magufuli kuboresha miundombinu nchini, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa amemuomba Mhe. Rais Magufuli
daraja hilo liitwe “Daraja la Magufuli” (Magufuli Bridge). Rais naye
ameridhia daraja hilo liitwe kwa jina lake. Hii ni mara ya pili Mhe.
Rais kuombwa daraja liitwe kwa jina lake na ni mara ya kwanza kukubali
baada ya kukataa ombi la awali la daraja la Kigamboni ambalo Rais
Magufuli alisemwa liitwe daraja la Nyerere.
Prof. Mbarawa ameamua kutoa jina
hilo ikiwa ni kwa mujibu wa sheria, na amebainisha kuwa uamuzi wake huo
umezingatia juhudi kubwa zilizofanywa na Mhe. Rais Magufuli tangu akiwa
Waziri wa Ujenzi, ambapo baada ya kutokea ajali ya kuzama kivuko
iliyosababisha takribani watu 30 kupoteza maisha mwaka 2001 alifika
Ifakara, akatoa pole kwa wafiwa na akaagiza kuanza kwa mchakato wa
ujenzi na kisha kuufuatilia kwa ukaribu hadi daraja hilo limekamilika.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema daraja
hilo lenye njia mbili litadumu kwa miaka zaidi ya 120, lina uwezo wa
kubeba tani 180 kila upande, lina njia za watembea kwa miguu na
limefungwa taa zinazotumia nishati ya jua (Solar Power).
Akizungumza na wananchi wa
Ifakara katika uwanja wa michezo mjini hapo Mhe. Rais Magufuli
aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amewapongeza wananchi wa
Ifakara kwa kujengewa daraja hilo, na pia amewapongeza Watanzania wote
kwa kulipa kodi zilizowezesha kutekelezwa kwa mradi huo mkubwa kwa
kutumia fedha zao.
Mhe. Rais Magufuli amewataka
wananchi wa Ifakara, Malinyi, Kilombero, Kilosa na maeneo mengine
yatakayonufaika na kujengwa kwa Daraja la Magufuli na ujenzi wa barabara
ya Kidatu – Ifakara kutumia miundombinu hiyo kwa manufaa yaani kuongeza
uzalishaji wa mazao ya kilimo na kuyasafirisha kwenda kwenye masoko, na
amewahakikishia kuwa Serikali itaendeleza ujenzi wa barabara ya lami
kutoka Ifakara – Malinyi – Londo hadi Lumecha Wilayani Songea ambako
itaungana na barabara kuu ya Songea – Namtumbo – Tunduru – Mtambaswala.
Mhe. Rais Magufuli amebainisha
kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu
ya Tano kujenga uchumi na kwamba juhudi kama hizo pia zinafanyika
kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia miradi ya Kinyerezi 1,2-3 na mradi
wa umeme katika mto Rufiji (Stieglers Gorge) itakayoiwezesha Tanzania
kuwa na Megawati 5,000 za umeme ifikapo mwaka 2021, kujenga reli,
kuimarisha usafiri wa anga, kulinda rasilimali ikiwemo madini na
kuboresha huduma za jamii zikiwemo kutoa elimu bure kwa shule za msingi
hadi sekondari, kuongeza mikopo ya elimu ya juu, kuimarisha miradi ya
maji na kuboresha huduma za afya.
Mhe. Rais Magufuli ambaye akiwa
njiani kuelekea Ifakara alisimamishwa na wananchi wa vijiji vya Sande,
Misufini, Mkula, Mang’ula, Mang’ula Kona, Kisawasawa, Kiberege na Sululu
ambako alisikiliza kero zao na kuchangia fedha katika miradi ya
maendeleo, aliwataka wabunge kuwajibika ipasavyo kwa kusikiliza kero za
wapiga kura wao na kuzifanyia kazi badala ya kuacha kero hizo ziwasubiri
viongozi wa kitaifa.
“Wabunge mna fedha za mfuko wa
jimbo, wasaidieni wananchi wenu, haiwezekani wananchi wawe wanamuomba
Rais fedha za kujengea matundu ya vyoo vya shule wakati nyinyi mpo”
amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu kero ya wananchi kuendelea
kutozwa ushuru wa mazao yasiyozidi tani moja kwa mujibu wa sheria, Mhe.
Rais Magufuli aliwataka viongozi kote nchini kuwashughulikia wanaotoza
ushuru huo na kusisitiza kuwa “Najua viongozi wote Tanzania mnanisikia,
nataka mtu atoke na mchele hapa Ifakara apeleke Dar es Salaam, apeleke
Moshi, apeleke Tabora na ashuke nao mpaka Mpanda bila kubughudhiwa
ilimradi hauzidi tani moja”.
Akiwa katika vijiji vya Mang’ula
na Mang’ula Kona Mhe. Rais Magufuli alisema Serikali imeanza kuchukua
hatua za kukirejesha kiwanda kutengeneza vipuri cha Mang’ula ili
kuhakikisha kinaendeshwa kwa malengo yaliyokusudiwa na Baba wa Taifa
Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Barabara na madaraja yanayowekewa
mawe ya msingi na kuzinduliwa ni dalili kwamba uchumi wa Tanzania
utakua kwa kasi kwani mazao na malighafi ya viwanda yatafikishwa
viwandani kwa muda mwafaka na hatimaye bidha za viwanda
zitawezakulifikia soko kwa wakati kutokana na ubora wa mioundombinu.
Usafiri wa uhakika utapunguza
hata bei hivyo kuwawezesha wananchi hata wa kipato cha chini kuweza
kununua bidhaa hizo. Kwa kipindi cha nyuma ilikuwa inachukua takriban
siku tatu hadi nne kusafirisha mahindi toka Songea, mkoani Ruvuma na
kuyafikisha Dar es Salaam, lakini baada ya kujengwa barabara za lami
toka Dar es salaam hadi Songea, ni siku moja mazao hayo kusafirishwa kwa
umbali ulele.
Miundombinu bora ni muhimili wa
uchumi, hivyo wananchi hawanabudi kuunga mkono juhudi za Serikali ya
Awamu ya Tano katika kuboresha miundombinu. Ikumbukwe kuwa na ujenzi wa
reli ya kisasa ya viwango vya kimataifa (Standard Gauge Railway)
itasaidia zaidi kwenye kusafirisha tani nyingi za mazo kwa pamoja na kwa
wakati muda mfupi. Takriban nchi zote duniani hutumia usafiri wa treni
katika kusafirisha mizigo.
Upatikanaji wa uhakika wa nishati
ya umeme nalo ni suala muhimu sana katika ujenzi wa uchumi unaotegemea
viwanda. Sanjari na ujenzi wa madaraja na barabara, ujenzi wa
miundombinu ya umeme hasa mradi wa Stieglers Gorge ni ushahidi tosha
kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya kuwakomboa wananchi wake.
No comments :
Post a Comment