Mwenyekiti wa Baraza la
Wafanyakazi la Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila akisoma hotuba
ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko kwenye mkutano wa
baraza la kwanza la wafanyakazi wa Wizara ya Madini mjini Morogoro
wenye lengo la kujadili utendaji kazi na namna ya kukabiliana na
changamoto katika sekta ya madini.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula akitoa ufafanuzi katika mkutano huo
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki
(katikati waliokaa mbele), Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ( wa nne
kutoka kulia waliokaa mbele), Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini ( wa nne
kutoka kushoto waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na
washiriki wote mara baada ya uzinduzi wa mkutano huo.
…………………
Greyson Mwase na Asteria Muhozya, Morogoro
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini,
Profesa Simon Msanjila amesema kuwa zoezi la utoaji wa leseni kwa ajili
ya utafiti, uchimbaji na biashara ya madini linatarajiwa kuanza muda
wowote kuanzia sasa mara baada ya uanzishwaji wa Tume ya Madini.
Profesa Msanjila ameyasema hayo
katika mahojiano maalum na waandishi wa habari kwenye
mkutano wa baraza
la kwanza la wafanyakazi wa Wizara ya Madini mjini Morogoro tarehe 07
Mei, 2018 wenye lengo la kujadili utendaji kazi na namna ya kukabiliana
na changamoto katika sekta ya madini.
Akielezea hatua iliyofikiwa ya
zoezi hilo, Profesa Msanjila amesema kinachofanyika kwa sasa ni
uchambuzi wa maombi ya leseni zote zilizokwishawasilishwa na kampuni
mbalimbali zenye lengo la kujihusisha na shughuli za madini nchini.
Katika hatua nyingine, akielezea
mkutano huo, Profesa Msanjila amesema mkutano huo wa kwanza unaambatana
na uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi ambalo lipo kisheria.
Ameendelea kueleza kuwa masuala
yatakayojadiliwa katika mkutano huo kuwa ni pamoja na umuhimu wa baraza
la wafanyakazi, muundo wa Wizara ya Madini na maadili katika utumishi wa
umma.
Ametaja masuala mengine kuwa ni
pamoja na mapitio na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018,
mpango wa bajeti wa mwaka 2018/2019 na marekebisho ya Sheria ya Madini
ya mwaka 2017.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume
ya Madini Profesa Idris Kikula amesema kuwa tayari tume imekaa na
kuweka mkakati kuhusu masuala ya leseni ili kuhakikisha kuwa leseni
zinatolewa kwa wakati baada ya zoezi la utoaji wa leseni kusitishwa
tangu Julai mwaka 2017.
Akielezea hatua iliyofikiwa ya
zoezi la uchambuzi wa leseni, Profesa Kikula amesema zaidi ya leseni
8,000 zimeshachambuliwa na kusisitiza kuwa zoezi litakapokamilika
waombaji waliokidhi vigezo watataarifiwa ili kuanza kufanya taratibu za
malipo.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha
Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Tawi la Wizara ya
Madini, Agathon William amesema kuwa baraza la wafanyakazi ni chombo
muhimu kinachowaunganisha wafanyakazi wa Wizara katika uongozi kwa
pamoja mahali pa kazi ili kuleta tija katika utekelezaji wa shughuli za
Wizara.
Amesema baraza huishauri Wizara
juu ya kuongeza ufanisi wa kazi na hatua zinazofaa kuchukuliwa
kuhakikisha kuwa huduma zitolewazo na Wizara ni za kuridhisha kulingana
na malengo ya Taifa ya kuleta maendeleo na kupunguza umaskini kwa
kuanzisha viwanda vingi vitakavyoongeza kasi ya ukuaji wa Uchumi wa
Taifa.
Ameendelea kusema kuwa baraza hilo
hujadili na kushauri mipango na bajeti ya wizara na kupima mafanikio na
kuridhia utekelezaji wake pamoja na upandishwaji wa vyeo wafanyakazi
kutokana na miundo ya utumishi.
No comments :
Post a Comment