Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini,
Profesa Simon Msanjila akifafanua jambo kwenye uzinduzi wa ripoti ya
Nane ya ulinganishi wa mapato ya Serikali na malipo ya kampuni za
madini, mafuta na gesi asilia kwa mwaka wa fedha 2015/16 uliofanyika
jijini Dar es Salaam na kukutanisha wawakilishi kutoka Kamati ya TEITI,
Wizara ya Madini, makampuni ya mafuta na gesi tarehe 30 Aprili, 2018.
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki
akisoma hotuba ya uzinduzi wa ripoti ya Nane ya ulinganishi wa mapato
ya Serikali na malipo ya kampuni za madini, mafuta na gesi asilia kwa
mwaka wa fedha 2015/16 uliofanyika jijini Dar es Salaam na kukutanisha
wawakilishi kutoka Kamati ya TEITI, Wizara ya Madini, makampuni ya
mafuta na gesi tarehe 30 Aprili, 2018.
Kutoka kulia mbele, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Waziri wa Madini, Angellah
Kairuki na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI, Augustina Rutaihwa
wakifuatilia ripoti ya Nane ya ulinganishi wa mapato ya Serikali na
malipo ya kampuni za madini, mafuta na gesi asilia kwa mwaka wa fedha
2015/16 iliyokuwa inawasilishwa na mtaalam mwelekezi kutoka kampuni ya
Boas & Associates na MM Attoneys, Symphorian Malingumu (hayupo
pichani)
Mtaalam mwelekezi kutoka kampuni
ya Boas & Associates na MM Attoneys, Symphorian Malingumu
akiwasilisha ripoti ya Nane ya ulinganishi wa mapato ya Serikali na
malipo ya kampuni za madini, mafuta na gesi asilia kwa mwaka wa fedha
2015/16 kwenye uzinduzi huo.
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki
( wa pili kulia) akizindua ripoti ya Nane ya ulinganishi wa mapato ya
Serikali na malipo ya kampuni za madini, mafuta na gesi asilia kwa mwaka
wa fedha 2015/16. Katikati ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa
Simon Msanjila.
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki
(wa pili kulia mbele) Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon
Msanjila (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi kutoka
Kamati na Sekretarieti ya TEITI mara baada ya kuzindua ripoti hiyo.
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki
(katikati, waliokaa mbele ) Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa
Simon Msanjila (wa tatu kutoka kulia waliokaa mbele) wakiwa katika picha
ya pamoja na wawakilishi kutoka Kamati na Sekretarieti ya TEITI mara
baada ya kuzindua ripoti hiyo.
………………….
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Aprili 30, 2018
Leo tarehe 30 Aprili, 2018 Waziri
wa Madini, Angellah Kairuki amezindua ripoti ya Nane ya ulinganishi wa
mapato ya Serikali na malipo ya kampuni za madini, mafuta na gesi asilia
kwa
mwaka wa fedha 2015/16 iliyoandaliwa chini ya Mpango
wa Uhamasishaji Uwazi katika Mapato ya Madini, Gesi Asilia na Mafuta
Tanzania (TEITI) kwa kushirikiana na Mtaalam Mwelekezi, Boas &
Associates na MM Attoneys.
Akizungumza katika uzinduzi wa
ripoti hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam na kukutanisha wawakilishi
kutoka Kamati ya TEITI, Wizara ya Madini, makampuni ya mafuta na gesi,
Waziri Kairuki amepongeza Kamati ya TEITI na Sekretarieti kwa mchango
wake katika uandaaji wa ripoti hiyo.
Mbali na Pongezi hizo, Kairuki
ameiagiza Kamati ya TEITI kuongeza nguvu katika kuhakikisha wananchi
wanakuwa na uelewa mpana wa umuhimu na wajibu wa TEITI kwa kutumia
mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na warsha mbalimbali pamoja na vipindi
vya redio na televisheni.
Amesisitiza kuwa, kipaumbele
kiwekwe kwenye maeneo yaliyozungukwa na shughuli za utafutaji na
uzalishaji wa madini, mafuta na gesi asilia na kupata taarifa ndani ya
kipindi cha miezi sita.
Awali akielezea ripoti hiyo,
Kairuki amesema kuwa ripoti hiyo inahusu tathmini ya mapato ya madini
katika kipindi cha kuanzia tarehe 1 Julai, 2015 hadi tarehe 30 Juni,
2016 na kufafanua kuwa jumla ya shilingi 434,627,874,380 zilipokelewa
serikalini kutoka kwenye kampuni 55 za madini, mafuta na gesi asilia
zilizoshiriki zoezi la ulinganishi.
Hata hiyo amesema taarifa
inaonesha kuwa kampuni zililipa kiasi cha shilingi 465,164,747,725 za
kitanzania serikalini na kusababisha tofauti kati ya malipo kuwa ni
pungufu ya shilingi 30,536,873,345 za kitanzania chini ya kiasi ambacho
Serikali imekiri kupokea.
“ Ni lazima tufahamu ni vipi
imejitokeza tofauti hii na ninachukua fursa hii kuelekeza taarifa hii
kupelekwa kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa ajiili ya
uchunguzi kama kifungu 18(1) cha Sheria ya TEITI ya mwaka 2015
kinavyotaka,” alisema Waziri Kairuki.
Katika hatua nyingine, Waziri
Kairuki amefafanua kuwa ripoti imeonesha kuwa sekta ya madini
imechangia zaidi kwa asilimia 85 na sekta ya mafuta na gesi ikionyesha
kuchangia asilimia 15 ya mapato ya Serikali chini ya Sekta ya Madini kwa
mwaka 2015/16
Akielezea mafanikio ya Serikali ya
Awamu ya Tano katika sekta ya madini, Kairuki amesema kuwa ili
kuhakikisha madini yanakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi,
Serikali imeanza kuchukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kufanya
mabadiliko ya Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake.
Ametaja hatua nyingine ambayo ni
endelevu kuwa ni kufanya tathmini ya jinsi gani nchi inapata mapato
yake kwenye sekta ya madini kutokana na hatua mbalimbali
zinazochukuliwa.
Ameendelea kusema kuwa jukumu
linafanywa na taasisi mbalimbali za Serikali lakini TEITI nayo
inatekeleza jukumu husika kwa kuhakikisha taarifa za mapato ya madini
zinatolewa kwa uwazi kwa wananchi na wadau mbalimbali katika Serikali,
Sekta Binafsi na Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Wakati huo huo akizungumza
na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon
Msanjila amesema kuwa mara baada ya ripoti kuzinduliwa na kukabidhiwa
kwa Kamati ya TEITI hatua inayofuatia ni kamati ya TEITI kuwasilisha
ripoti hiyo kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili achukue hatua
kwenye hoja zilizotokana na ripoti hiyo.
Profesa Msanjila amezitaka kampuni
nyingine ambazo hazikushiriki katika kipindi cha ukaguzi kujitokeza
katika ukaguzi unaofuata ili takwimu halisi za mapato zifahamike.
Aidha, ametumia fursa hiyo
kukaribisha kampuni nyingine zenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya
madini kujitokeza kwa wingi ili sekta ya madini iwe na mchango mkubwa
katika ukuaji wa uchumi.
No comments :
Post a Comment