SPIKA wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA),
Dkt. Martin Ngoga ameishukuru na kuipongeza Serikari ya Tanzania kwa
ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo wa reli kwa sababu
inaleta manufaa hata kwa nchi jirani.
“Miradi hiyo ambayo kwa sasa
inatekelezwa kwa kasi si kwamba inachochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania,
bali hata wa nchi nyingi za jirani kwa kuwa nazo zitanufaika na miradi
hiyo kwani si nchi zote zina bandari”.
Dkt. Ngoga ameyasema hayo leo
(Jumatatu, Aprili 23, 2018) alipokutana na kufanya mazungumzo
na Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, Bungeni mjini Dodoma.
Amesema tayari wamejadili ripoti
iliyotokana na ziara iliyofanywa na wabunge hao katika upande wa korido
ya kuishi na korido ya kaskazini ambapo wametoa mapendekezo
yatakayofanyiwa kazi na baraza la mawaziri.
“Tayari tumeshajadili miswada miwili
inayohusu Itifaki ya Sarafu Moja ambayo ni mswada wa taasisi ya Fedha na
mswada wa Takwimu yote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2017.”
Pia Spika huyo amesema wamefurahia uwepo
wao nchini, ambapo mbali na shughuli zao za kibunge pia kwa kushirikiana
na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wameshiriki kampeni ya kukijanisha
Dodoma kwa kupanda miti 1,000 kwenye eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM).
Kwa upande wake, Waziri Mkuu amesema
amefarijika na uamuzi wa Bunge la EALA kufanya vikao vyake katika nchi
wanachama kwa sababu unatoa fursa ya kujua mazingira ya nchi hizo pamoja
na maendeleo yake.
Amesema nchi wanachama wanamatumaini
makubwa na bunge hilo katika kuimarisha na kuboresha maendeleo ya
mataifa yao, hivyo amewatakia mjadala mwema.
Katika hata nyingine, Waziri Mkuu
amewakaribisha wabunge hao na marafiki zao kuja kuwekeza kwenye sekta
mbalimbali nchini ikiwemo ya viwanja, utalii, kilimo na madini.
Kwa mara ya kwanza vikao vya Bunge la
Afrika Mashariki, (EALA) vinafanyika Dodoma katika ukumbi wa Bunge wa
Msekwa ulipo ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vikao
hivyo vilianza Aprili 17, 2018 na vinatarajiwa kumalizika Aprili 29,
2018.
No comments :
Post a Comment