Na Lilian Lundo – MAELEZO,Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Wanaafrika Mashariki
kujiamini kuwa wanaweza kutekeleza miradi ya maendeleo bila kutegemea
mataifa mengine.
Rais Dkt. Magufuli ameyasema hayo
leo Mjini Dodoma alipokuwa akihutubia Bunge la Nne la Jumuiya ya Afrika
Mashariki linalofanyika mkoani humo kwa mara kwanza tangu kuanza
kwa
Bunge hilo.
“Ninazungumza hili si kwamba
hatuhitaji msaada au hatuhitaji ushirikiano, lakini ni lazima tuliweke
hili wazi, kwamba tukiamua tunaweza na mifano ipo mingi ikiwemo
Tanzania”. Alisisitiza Mhe. Rais Dkt. Magufuli.
“Tanzania tunajenga reli ya kisasa
yenye urefu wa kilometa 700.26 kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa
thamani ya shilingi Trilioni 7.6, tumeweza kununua ndege sita na pia
tumejenga meli kubwa katika Ziwa Victoria bila kuomba mkopo popote,”
amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli ameongeza
kuwa wabunge wa Afrika Mashariki wanaowajibu wa kuhakikisha wanalinda na
kuendeleza mafanikio yaliyopatikana ndani ya Jumuiya hiyo.
Akitaja baadhi ya mafanikio
yaliyopatikana na Jumuiya hiyo Rais Magufuli amesema kuwa kabla ya
kuanza kwa umoja wa forodha mwaka 2005 biashara kati ya nchi wanachama
ilikuwa na thamani ya dola za kimarekani bilioni 1.8 lakini baada ya
kuanzishwa kwa umoja wa forodha imeongezeka hadi kufikia zaidi ya dola
za kimarekani bilioni 5.
Mbali na hayo Rais, Magufuli
ameshukuru uamuzi wa bunge hilo kufanyika mjini Dodoma ambapo kwa sasa
Serikali imehamishia shughuli zake zote katika mkoa huo, na tayari
watumishi wa serikali zaidi ya 3000 wameshahamia huku Rais Magufuli
akitarajiwa kuhamia muda wowote mwaka huu.
Kwa upande wake Spika wa Bunge
la Afrika Mashariki Dkt. Martin Ngoga amesema Bunge hilo linasubiri
marekebisho ya mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ili lugha ya
Kiswahili ianze kutumika kama lugha rasmi katika vikao vya bunge hilo na
katika jumuiya hiyo kwa kuzingatia azimio lililokwishapitishwa.
“Hatuoni sababu ya kutumia lugha za wageni wakati kuna lugha yetu ambayo tunazungumza ambayo ni kiswahili,” alisema Dkt. Ngoga.
Bunge la Afrika Mashariki
linaendelea na vikao vyake mkoani Dodoma katika ukumbi mdogo wa Bunge wa
Pius Msekwa. Bunge hilo limefanyika kwa mara ya kwanza mkoani humo.
No comments :
Post a Comment