WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemkabidhi Bibi Tecla Hamidu ambaye ni mlemavu wa miguu sh. milioni
tano ili aweze kuongezea katika mtaji wake.
Ametoa fedha hizo leo (Jumanne,
Machi 20, 2018) ikiwa ni katika kutimiza ahadi yake aliyoitoa Februari
22, 2018 kwenye Mkutano wa Sita wa Wamiliki wa Viwanda na Watumiaji wa
simbomilia (barcodes).
Waziri Mkuu alitoa ahadi hiyo
baada ya Bibi Tecla ambaye ni mjasiriamali anayejihusisha na ushonaji wa
bidhaa mbalimbali zikiwemo nguo kumuomba amchangie sh. 500,000 ili
aweze kuongezea mtaji wake.
Wakati akimkabidhi fedha hizo,
Waziri Mkuu amesema kwamba anatarajia zitamsaidia katika kuongeza mtaji
wake, hivyo atazalisha bidhaa nyingi zenye ubora unaohitajika katika
masoko ya ndani na nje.
Kwa upande wake, Bibi Tecla alimshukuru Waziri Mkuu kwa msaada huo na ameahidi kuzitumia fedha hizo kama ilivyo kusudiwa.
“Nashukuru kwa msaada huu kwani
kuna watu wanakopa sh. laki mbili ili waongeze mitaji, lakini mimi leo
nimepewa milioni tano bure na kiongozi wetu,”
Amesema licha ya kukabiliwa na
changamoto ya upatikanaji wa masoko anaamini tatizo hilo litakuwa
historia baada ya kuwa na mtaji wa kutosha kwani atakwenda kuzalisha
bidhaa zenye ubora zaidi.
No comments :
Post a Comment