Sunday, March 18, 2018

TANROADS IMEJIPANGA KUWALIPA WAKANDARASI KWA WAKATI


1
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Aggrey Mwanry akisisitiza umuhimu wa wananchi kulinda miundombinu ya barabara katika kijiji cha Imalamakoye katika jimbo la Urambo wakati wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu walipokagua ujenzi wa barabara Tabora- Urambo-Kaliua inayojengwa kwa kiwango cha lami, kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi) Mhe. Elias John Kwandikwa.
2
Muonekano wa barabara ya kutua na kurukia ndege ambayo ujenzi wake umekamilika katika uwanja wa ndege wa Tabora.
3
Muonekano wa barabara ya Mwigumbi-Maswa KM 50.3 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Mwigumbi-Maswa-Bariadi-Lamadi KM 171.8
4
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Moshi Selemani Kakoso akifafanua jambo kwa  Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi) Mhe. Elias John Kwandikwa wakati Kamati hiyo ilipokagua ujenzi wa barabara ya Mwigumbi-Maswa-Bariadi-Lamadi KM 171.8 inayojengwa kwa kiwango cha lami, wengine ni wajumbe wa kamati hiyo wakifuatilia.
5
Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi) Mhe. Elias John Kwandikwa akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu walipokagua ujenzi wa barabara ya Mwigumbi-Maswa-Bariadi-Lamadi KM 171.8 inayojengwa kwa kiwango cha lami.
……………….
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anaeshughulikia (sekta ya ujenzi), Mhe. Elias John Kwandikwa amesema Serikali inaendelea kuwalipa wakandarasi wa barabara madeni yao ya zamani nay a sasa ili kuwawezesha kuongeza kasi katika miradi mipya ya ujenzi wanayopewa.
Mhe. Kwandikwa ameiambia Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuwa tayari kiasi cha shilingi bilioni 400 kimelipwa kwa wakandarasi katika muda mfupi ikiwa ni mkakati wakuwawezesha kuwa na kasi katika miradi mingine ya ujenzi inayoendelea.
“Tumejipanga kuhakikisha madeni ya ujenzi wa barabara yanalipwa kwa wakati ili tuwe na nguvu ya kuwabana wakandarasi kumaliza miradi kwa wakati”, amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.
Amesema nia ya Serikali ni kuziwezesha barabara kuu na za mikoa kufunguka kwa lami ili kupunguza mzunguko kwa njia nyingi na kuiunganisha mikoa na wilaya kiurahisi na hivyo
kuchochea shughuli za kilimo,mifugo,uvuvi na biashara nchini kote.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Moshi Sulemani Kakoso amesisitiza umuhimu wa barabara zinazojengwa kuwekewa maeneo maalum ya kuvusha mifugo ili zidumu kwa muda mrefu na kusisitiza umuhimu wa kuwawezesha wakandarasi wa ndani katika miradi midogo ili kuwajengea uwezo.
“Hakikisheni mnakuwa na programu endelevu za kuwawezesha wakandarasi wa ndani ili baadhi ya miradi waitekeleze wenyewe na hivyo kukuza uwezo wa kitaalamu na kiuchumi”, amesema Mhe. Kakoso.
Aidha Mwenyekiti huyo wa kamati ya miundombinu amesisitiza umuhimu wa kuwaelimisha wananchi umuhimu wa barabara za lami ili badala ya kuzihujumu kwa kuharibu miundombinu yake wazilinde na kuzitumia kuibua fursa za kiuchumi na kijamii katika maeneo yao.
Kamati ya Bunge ya Miundombinu iko katika ziara ya kutembelea miundombinu inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mwanza, na Mara.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano

No comments :

Post a Comment