Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Serikali imetenga jumla ya
shilingi Trilioni 1 mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kulipa madeni
mbalimbali ya watoa huduma, wazabuni na watumishi wa Umma.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari
(MAELEZO) Dkt. Hassan Abbasi ameeleza hayo leo Mjini Dodoma alipokuwa
akiongea na waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa miradi na ahadi
mbalimbali za Serikali.
“Kati ya shilingi Trilioni 1
zilizotengwa kulipia madeni kwa mwaka huu wa fedha, shilingi Bilioni
896.3 zimeshalipwa kwa watoa huduma, wazabuni na watumishi wa Serikali,”
alisema Dkt. Abbasi.
Amesema hesabu hiyo inajumuisha
shilingi Bilioni 43 ambazo zimelipwa Februari, 2018 ikiwa ni malimbikizo
ya wafanyakazi wa
sekta ya Umma.
“Madeni mengine uhakiki unaendelea na yataendelea kulipwa siku zijazo na tutawajulisha,” alifafanua Dkt. Abbasi.
Vile vile amesema, Serikali katika
kuwaondolea adha ya usafiri kwa wananchi wa maziwa makuu likiwemo Ziwa
Nyasa, Tanganyika na Victoria. Kwa upande wa Ziwa Victoria, mkandarasi
amepatikana na majadiliano ya mwisho na kusaini mkataba na kampuni ya
STX ya Jamhuri ya Korea vitafanyika mwezi huu kwa ajili utengenezaji wa
meli mpya itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo tani
400.
Kwa upande wa Ziwa Tanganyika
zabuni kwa ajili ya utengenezaji wa meli mpya ya abiria na mizigo
itatangazwa mwezi huu. Meli hiyo mpya itakuwa na uwezo wa kubeba abiria
600 na tani 400 za mizigo na italeta mapinduzi makubwa katika usafiri
ziwani hilo.
Aidha Dkt. Abbasi amesema Julai
mwaka huu nchi itapokea ndege kadhaa mpya ikiwemo Boeing Dreamliner na
ukarabati wa viwanja vya ndege vya Kitaifa, Kimataifa na Kimkoa
unaendelea kwa kasi kote nchini.
No comments :
Post a Comment