Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama
akizungumzia mikakati ya Serikali kupambana na janga la Ukimwi hapa
nchini wakati wa warsha kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Ukimwi na Madawa ya Kulevya mapema leo Bungeni mjini Dodoma. kushoto ni
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana na Ajira mhe. Antony
Mavunde.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Ukimwi na Madawa yakulevya Mhe. Osca Mukasa (Mb) akisisitiza
jambo wakati wa warsha kwa wabunge wa Kamati hiyo kuhusu hali ya Ukimwi
hapa nchini iliyofanyika mapema leo mjini Dodoma.kulia ni Katibu wa
Kamati hiyo Bi Happiness Ndalu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya
Taifa ya Kudhibi Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Leonard Maboko akiwasilisha mada
kuhusu hali ya Ukimwi hapa nchini wakati wa warsha kwa wajumbe wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya mapema leo Bungeni
mjini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya
Taifa ya Kudhibi Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Leonard Maboko (kulia) akiteta
jambo na mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ukimwi na
Madawa ya Kulevya Mhe. Edward Mwalongo (Mb) mara baada ya warsha kwa
wajumbe wa Kamati hiyo mapema leo mjini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya
Taifa ya Kudhibi Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Leonard Maboko (katikati)
akitoka nje ya Viwanja vya Bunge leo mjini Dodoma mara baada
yakuwasilisha mada kuhusu hali ya ukimwi hapa nchini wakati wa warsha
kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ukimwi na Madawa yakulevya
mapema leo Bungeni mjini Dodoma.
( Picha zote na Frank Mvungi, Maelezo Dodoma
……………..
Frank Mvungi- MAELEZO, Dodoma
Serikali imesema itaendeleza
mapambano ya Vita dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi kwa kuongeza kasi katika
kuzuia maambukizi mapya ikiwemo kutoa elimu kwa umma.
Akizungumza leo mjini Dodoma
wakati wa warsha kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge
inayoshugulikia Ukimwi na Madawa yakulevya Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu mhe. Jenista Mhagama
amesema kuwa dhamira ya Serikali baada ya kuanzisha mfuko wa Udhamini wa
Kudhibiti Ukimwi (ATF) ni kuhakikisha kuwa mfuko huo unajengewa uwezo
ili lengo la kuanzishwa kwake litimie.
“Tayari mfuko umeweza kukusanya
bilioni 279 katika kipindi kilichopita na mwaka huu bilioni 3 zimetengwa
katika Bajeti na zitaingizwa katika mfuko huu ili uweze kutimiza
majukumu yake kwa ufanishi na tumekuwa tukiwashirikisha wadau katika
kuchangia na wamekuwa wakituunga mkono na tunaendelea kuwaomba
wajitokeze zaidi kuchangia mfuko huu ” Alisisitiza Mhagama.
Akifafanua Mhe. Mhagama amesema
kuwa tayari mapendekezo kuhusu kuwepo kwa tozo maalum katika kodi
yameshawasilishwa katika kamati husika kwa hatua zaidi dhamira ikiwa ni
kuujengea mfuko huo uwezo wa kuwa na fedha za kutosha katika kufanikisha
vita dhidi ya Ukimwi hapa nchini.
Mkakati mwingine ni ujenzi wa
kituo maalum katika eneo la Mererani Mkoani Manyara kitakachosaidia
katika mapambano dhidi ya Ukimwi kwa kuwa eneo hilo ni moja ya maeneo
yenye mwingiliano mkubwa wa watu kutokana na shughuli za uchimbaji
madini.
Hatua nyingine ni kufanya kazi kwa
kushirikiana kati ya TACAIDS na Mamlaka ya Kupambana na Dawa za
Kulevya ili kuwafikia waathirika wa dawa za kulevya ambao ni moja ya
makundi yanayoathika na ugonjwa wa ukimwi kwa mujibu wa tafiti
mbalimbali.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa
Kamati hiyo Mhe. Osca Mukasa (Mb) amesema kuwa kutengwa kwa fedha
katika bajeti ya 2018/19 zitakazopelekwa katika mfuko wa kudhibi Ukimwi
ni ishara nzuri kuwa serikali imeweka mkazo katika mapambano dhidi ya
janga hilo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
TACAIDS Dkt. Leonard Maboko amesema Tume hiyo iko katika hatua za
mwisho za kukamilisha mkakati wa Nne unaolenga kuongeza nguvu ili
kufikiwa kwa malengo ya mkakati huo.
Akifafanua Dkt. Maboko amesema
kuwa Tume hiyo imeandaa kampeni maalum kuhamasisha wananchi kupima ili
kujijua kama wameambikizwa virusi vya ukimwi au laa hali itakayowasaidia
kuchukua hatua stahiki na kwa wakati hivyo kuzuia maambukizi mapya hasa
kwa vijana.
“Hapa nchini kwa mwaka kuna
maambukizi mapya elfu 81,000 hivyo ni vyema tukaungana katika mapambano
dhidi ya ugonjwa huu kwa kuwa uwezo wa kuzuia maambuki mapya tunao”.
Alisisitiza Dkt. Maboko.
Warsha kwa wajumbe wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya imefanyika mjini Dodoma
leo ikiwashirikisha wajumbe wote wa kamati hiyo, Aidha mfuko wa
Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) unalenga kuongeza rasilimali fedha
kutoka asilimia 7 (2015) hadi asilimia 30 (2018).
No comments :
Post a Comment