Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akiongea na wajumbe wa
Menejimenti ya Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) (hawapo pichani)
wakati wa ziara yake kwenye taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.
Anayemsikiliza ni Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo Bwana Tito
Kasambala
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bwana Richard Mayongela (kushoto)
akimkaribisha Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta
Nditiye (kulia) kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam wakati wa ziara
yake ya kutembelea na kukagua Wakala wa Ndege za Serikali
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akipanda kukagua mojawapo ya
ndege za Wakala wa Ndege za Serikali inayosafirisha viongozi wa ngazi ya
juu wa Serikali wakati wa ziara yake kwa Wakala hiyo kwenye uwanja wa
ndege wa Dar es Salaam
Mkaguzi Mkuu wa Wakala wa Ndege za
Serikali Mhandisi Bernard Mayila akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye wakati akifanya
ukaguzi ndani ya ndege mojawapo inayosafirisha viongozi wa ngazi za juu
wa Serikali wakati wa ziara yake alipotembelea Wakala hiyo kwenye uwanja
wa ndege wa Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akiteremka baada ya kukagua
mojawapo ya ndege za Wakala wa Ndege za Serikali wakati wa ziara yake
kwenye Wakala hiyo kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam
……………….
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania imejipanga kuboresha Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) ambayo
inasimamia na kuendesha ndege ambazo zinasafirisha viongozi wa kitaifa
wa Serikali
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa ziara yake ya kikazi alipotembelea
na kukagua utekelezaji wa majukumu ya Wakala wa Ndege za Serikali ambayo
inasimamia na kuendesha ndege ambazo zinasafirisha viongozi wa kitaifa
wa Serikali ambapo alizungumza na Menejimenti na wafanyakazi na
kuwaeleza kuwa Serikali imejipanga kuboresha Wakala hiyo
Mhandisi Nditiye alisema kuwa azma
ya Serikali ya Awamo ya Tano inayosimamiwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ni kuhakikisha kuwa
Taasisi za Serikali zinafanya kazi zake kwa weledi na uadilifu ili
kufanikisha malengo ya Serikali ya kuwatumikia wananchi. “Serikali
inatambua umuhimu wa Wakala hii na ina imani kubwa nanyi katika
kuhakikisha kuwa mnafanya kazi zenu za kusafirisha viongozi kwa usalama
na kwa uhakika ili waweze kutimiza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi
na tayari ina nia ya kuboresha taasisi hii”, amesema Mhandisi Nditiye.
Naye Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa
TGFA Bwana Tito Kasambala amemueleza Mhandisi Nditiye kuwa taasisi yake
ina ndege nne ambazo zinatumika kusafirisha viongozi wa kitaifa wa
Serikali katika kutimiza majukumu yao ya kuwatumikia watanzania na
tayari Serikali imetenga shilingi bilioni 11.4 kwenye bajeti ya mwaka wa
fedha wa 2017/18 kwa ajili ya shughuli mbali mbali za Wakala ikiwemo
matengenezo ya ndege, mafunzo kwa wanahewa na ukarabati wa karakana.
Mhandisi Nditiye amewaeleza
wajumbe wa Menejimenti na wafanyakazi wa Wakala hiyo kuwa Serikali
inatambua na kuthamini mchango wao na umuhimu wa wahandisi wa ndege na
marubani wa kupata nafasi ya kuendesha ndege na kozi za mafunzo mbali
mbali kuendana na taaluma zao ambapo tayari makubaliano yamefanyika
baina ya Wizara na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ya kuwapatia nafasi
marubani wa ndege za Wakala wa Ndege za Serikali nafasi ya kurusha ndege
mara kwa mara ili kuendana na matakwa ya taaluma zao.
Ameongeza kuwa Serikali
inashughulikia suala la miundo ya watumishi wa umma ambapo Wakala wa
Ndege za Serikali ni mojawapo ya taasisi ambayo muundo wake unafanyiwa
kazi ili kuweza kuzingatia taaluma, kada za watumishi na maslahi yao.
“Natumaini wote mnatambua na kuelewa kuwa kipindi cha hapo nyuma kidogo
utumishi wa umma uliingiwa na baadhi ya watu wachache ambao walikuwa
wanafanya ujanja ujanja na kuharibu utumishi wa umma ambapo Serikali ya
Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais
wetu, imelifanyia kazi jambo hili na ameunda bodi maalumu ambayo
inafanyia kazi suala la muundo, kada na maslahi ya watumishi wa umma,”
amesema Mhandisi Nditiye.
Aidha, wafanyakazi wa Wakala wa
Ndege za Serikali wamemuomba Mhandisi Nditiye kuwasilisha ombi lao kwa
Serikali la kuwaongezea mishahara yao kuendana na hali ya soko la ajira
ya marubani ilivyo nchini kwa sasa.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments :
Post a Comment