Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza
Naibu Kamishina wa Polisi Ahmed Msangi amewasisitiza askari kuepuka
ubambikaji kesi kwa wananchi, rushwa na ubabaishaji pia akiwataka askari
kufanya kazi kwa utii, nidhamu na maadili kama ambavyo Jeshi la Polisi
Tanzania linavyoelekeza. Hayo yamejiri tarehe 28/02/2018 wakati Kamanda
Msangi alipokutana na askari wa Wilaya ya Sengerema katika ukaguzi
anaoendelea kuufanya katika Wilaya na Vikosi vyote hapa Mkoani Mwanza.
Amewataka askari kukomesha
vitendo vya ubabaishaji kwa wananchi na ubambikaji kesi kama vipo, mfano
kesi ya madai inabadilishwa kuwa kesi ya jinai jambo ambalo linanyima
haki wananchi na kuchafua sifa nzuri ya Jeshi la Polisi. Hivyo
ubabaishaji wa aina hiyo uepukwe na yeyote atakaye bainika anafanya
hivyo hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.
Sambamba na hilo Kamanda
Msangi amewataka askari wa kila kitengo kusimama vyema katika nafasi
zao, ambapo alisema kila askari akiwa vizuri katika utendaji kazi
hakutakuwa na malalamiko yeyote toka kwa wananchi hivyo ni jukumu la
kila askari kuhakikisha dhamana aliyopewa na serikali ya kulinda
wananchi pamoja na mali zao anaisimamia vizuri bila ubabaishaji wa aina
yeyote ile.
Pia aliwataka askari wawe na
utaratibu mzuri wa upokeaji, utunzaji na uondoshaji wa vielelezo katika
vituo vya Polisi, kwani katika baadhi ya vituo vya Polisi lipo tatizo la
utunzaji wa vielelezo hivyo hataki kuona tatizo hilo linaendelea
kuwepo. Vilelele aliwataka Maofisa wa Polisi wa Wilayani hapo kuzingatia
taratibu zilizowekwa kisheria za uondoshaji wa vielelezo katika vituo
vya Polisi.
Hata hivyo alisema hategemei kuona
mlundikano wa vielelezo katika vituo vya Polisi ambavyo vimekaa vituoni
mwaka mmoja au zaidi. Kwani madhara yake vinaweza kuharibika, kupoteza
ubora au kupotea alafu baadae liwe deni kwa Jeshi. Hivyo aliwataka
askari kutekeleza maamuzi ya mahakama haraka juu ya uondoshaji wa
kielelezo/vielelezo baada ya kesi kumalizika mahakamani.
Kwa upande wa upelelezi
alisema kumekuwa na tatizo la kuchelewesha upelelezi wa kesi nyingi.
Jambo ambalo linawanyima wananchi haki. Hivyo alimtaka Mkuu wa Upelelezi
Wilayani hapo kushughulikia suala hilo mapema lisiwepo katika himaya
yake ili haki ipatikane haraka bila uonevu wa aina yeyote.
Pia aliwapongeza askari wa
Wilaya hiyo kwa utendaji mzuri wa kudhibiti uhalifu, aliwataka waongeze
juhudi kwa yale maeneo yenye vibaka na uhalifu mwingine mdogomdogo kwani
anaamini wanaweza. Ushirikiano ulipo na Viongozi wa ulinzi na usalama
Wilaya, Wananchi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama udumishwe ili
Sengerema iwe salama zaidi kwani amani ikiwepo maendeleo yatapatikana
zaidi.
Na Oscar Msuya – Mwandishi wa Polisi Mwanza.
No comments :
Post a Comment