Wananchi wakiendelea na huduma zinazotolewa na NHIF Mkoa wa Geita.
Wananchi wamejitokeza kupata huduma za upimaji wa afya bure na usajili wa watoto kwenye huduma za NHIF.
Na Grace Michael, Geita
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF), umeendelea na mkakati wake wa kuwafikia wananchi katika maeneo
yao kwa kuwapelekea huduma zake lakini pia upimaji wa afya bure kwa
lengo la kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.
Katika wiki hii, NHIF iko katika
Mkoa wa Geita ukitoa huduma za upimaji wa afya bure kwa magonjwa
yasiyoambukiza pamoja na kampeni ya usajili wa watoto chini ya umri wa
miaka 18 mpango unaojulikana kwa jina la Toto Afya Kadi.
Huduma hizi mkoani hapa zilianza tarehe Machi 28 na zitamalizika Aprili 2, mwaka huu wakati wa kuwashwa kwa Mwenge wa Uhuru.
Akizungumza wakati wa zoezi
hilo, Meneja wa NHIF Mkoa wa Geita, Dk. Mathias Sweya amewaomba wananchi
kutumia fursa hii kujua hali ya afya zao na kupata elimu ya kujikinga
na magonjwa lakini pia faida za kujiunga na Mfuko.
“Nawahamasisha wananchi wote
wafike eneo la Soko Kuu la zamani ambapo tumeweka kituo kwa ajili ya
kutoa huduma na viwanja vya Magogo siku ya Jumatatu wiki ijayo tarehe
2/04/2018,” anasema Dk. Sweya.
Wananchi waliofika bandani hapo wameupongeza Mfuko kwa jitihada zake za kuwafikia na kuwahudumia wananchi katika maeneo yao.
“Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
mmetusaidia sana kutuletea hii huduma hapa, hii inatusaidia kujua hali
ya afya zetu lakini pia kuujua Mfuko na huduma zake ambazo ni mkombozi
kwa maisha ya kila mwananchi hivyo huduma kama hizi ziwe endelevu,”
alisema Edson Kamzola mkazi wa Geita.
No comments :
Post a Comment