Thursday, March 29, 2018

MAONYESHO YA KILIMO KUFANYIKA KATIKA BONDE LA CHEJU MKOA WA KUSINI UNGUJA

 
Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiaolon akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar. Picha na – OMPR – ZNZ.

Ubalozi wa China Nchini Tanzania kwa kushirikiana na Wizara inayosimamia Sekta ya Kilimo Zanzibar unatarajiwa kuzindua Maonyesho ya Kilimo yanayotarajiwa kuanza mnamo Tarehe 9 Aprili 2018 katika Bonde la Cheju Mkoa Kusini Unguja kwa lengo la kuwaandaa Wakulima kuendesha Kilimo katika njia na misingi ya teknolojia ya Kisasa.

Maonyesho hayo yatakwenda sambamba na Ubalozi wa Jamuhuri ya China Nchini Tanzania kugawa Vifaa vya kilimo kwa Wakulima wa Zanzibar ambapo Wataalamu watakaosimamia Maonyesho hayo wanatazamiwa kuingia Nchini wakati wowote kuanzia leo.

Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China hapa Zanzibar Bwana Xie Xiaolon alisema hayo wakati akitoa Taarifa kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Xie Xiaolon alisema Zanzibar ni miongoni mwa maeneo mengi yaliyotengwa Nchini Tanzania yatayofaidika na Mpango wa upandaji bora wa Mpunga kwa kutumia Teknolojia ya Kisasa ambao utatolewa ufafanuzi katika Maonyesho hayo.

Alisema hatua ya kuandaliwa kwa maonyesho hayo imetokana na ushirikiano wa Kihistoria uliopo katika ya China na Tanzania ikiwemo Zanzibar kwa ujumla hasa katika Nyanja za Kilimo na maeneo mengine ya Maendeleo ya Kiuchumi na Ustawi wa Kijamii.

Balozi Mdogo wa China hapa Zanzibar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba utafiti uliofanywa kupitia Mpango huo wa Upandaji wa Mpunga kwa kutumia njia na mfumo wa Teknolojia ya Kisasa unawezesha Eka moja kutoa zaidi ya Tani Saba hadi Tisa za Mpunga jambo ambalo linaweza kuleta ustawi wa haraka kwa Wakulima wa Zanzibar.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alimueleza Balozi Mdogo wa China aliyepo hapa Zanzibar kwamba Maonyesho hayo yatasaidia Wananchi walio wengi hapa Nchini.

Balozi Seif alisema Wananchi wengi wa Visiwa vya Unguja na Pemba wanaishi Vijijini na mategemeo yao makubwa katika kujipatia riziki na Maendeleo yao yanatokana na Sekta Mama ya Kilimo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza na kuishukuru China kwa juhudi inayoendelea kuchukuwakwa kusaidia ufadhili wa Miradi mbali mbali ya Maendeleo na Kiuchumi akitolea Mfano mradi wa Ujenzi wa Skuli Pangawe, Ujenzi wa Uwanja wa Michezo ya Mao Tse Tung uliopo Mperani Kikwajuni pamoja na Ukamilishaji wa Jengo la Abiria la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume.

Alisema Jengo hilo lililokwenda sambamba na ujenzi wa na eneo la kuegeshea Ndege katika Kiwanja hicho kinakamilisha mfumo na hadhi ya Kimataifa kama vilivyo viwanja vyengine Duniani kitakachoongeza kasi katika Sekta ya Utalii inayotarajiwa kupanuka zaidi wigo katika muda mfupi ujao.

Akizungumzia sekta ya Uvuvi wa Bahari Kuu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema China imeonyesha nia ya kutaka kusaidia Sekta hiyo muhimu kutokana na Visiwa vya Zanzibar kuzunguukwa na Bahari katika maeneo yake yote.

Balozi Seif alisema kitendo cha China kukubali kuwagharamia baadhi ya Viongozi Waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupata mafunzo na kujionea fursa mbali mbali za Kitaalamu zinazotokana na Sekta hiyo Nchini China ni mwanzo mzuri wa kufungua milango ya Uwekezaji katika eneo hilo pana la Uvuvi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments :

Post a Comment