Na Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu Wizara ya Afya ya
Malawi Dkt. Charles Mwansambo ametembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa
Muhimbili (MOI) ili kupata uzoefu wa namna Taasisi hiyo inavyotoa huduma
za kibobezi (super specialist).
Akizungumza wakati wa ziara hiyo
leo Jijini Dar es Salaam Dkt. Mwansambo amesema ametembelea MOI ili
kuona uwezekano wa kuwaleta wagonjwa wa Malawi kupata huduma za Kibingwa
za Mifupa, Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu badala
yakuwapeleka India.
” Nimefurahi kuona kuwa tuna
huduma nzuri za kibingwa kwa jirani zetu wa Tanzania, hili ni jambo jema
na litatupunguzia gharama za kuwapeleka wagonjwa India badala yake
tunawaleta hapa MOI” amesema Dkt.Mwansambo.
Aidha, Dkt. Mwansambo alipata
fursa ya kutembelea vyumba vya upasuaji vya MOI, vyumba vya wagonjwa
walioko katika uangalizi maalum (ICU), wodi za watoto na wodi maalum za
kisasa za kulipia.
Kutokana na mafanikio ya miundo
mbinu ya kisasa yaliyopo MOI Dkt. Mwansambo ameonyesha dhamira ya dhati
ya kuleta madaktari wanafunzi hapa ili wapate ujuzi wa zaidi.
Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
MOI Mhandisi .Reginald Kimambo alimueleza Dkt. Mwansambo kwamba huduma
zinazotolewa katika hospitali hiyo zimebobea katika Mifupa, Ajali,
Upasuaji wa ubongo, mgongo, mishipa ya fahamu pamoja na kutua mafunzo
kwa madaktari bingwa wa COSESCA.
Ziara hii imekuja baada ya mkutano
wa 65 wa Mawaziri wa Afya wa Ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na
Kusini uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
No comments :
Post a Comment