Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (kulia) akimsikiliza Mkurugenzi wa Kampuni Nyamigogo Grand
Vezir Holdings Ltd Hussein Amar (kushoto) akielezea mtambo wa kuchenjulia
dhahabu wakati wa ziara yake kwenye mradi wa kuchenjua dhahabu wa kampuni hiyo.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (kushoto) akikagua eneo linalojengwa mitambo ya kusagia
mawe kwa ajili ya kuchenjua dhahabu katika mgodi wa Nyamigogo Grand Vezir
Holdings Ltd uliopo Wilayani Nyang’hwale Mkoani Geita.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (katikati) alipofanya ziara kwenye mradi wa kuchenjua
dhahabu wa Kampuni ya Nyamigogo Grand Vezir Holdings Ltd uliopo Wilayani
Nyang’hwale Mkoani Geita. Kushoto ni Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Hussein Amar.
NAIBU Waziri wa
Madini, Doto Biteko ameipongeza Kampuni ya Mzawa ya Nyamigogo Grand Vezir
Holdings Ltd inayojishughulisha na uchenjuaji dhahabu kwa kuthubutu kuanzisha
mradi huo na aliahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano ili kuona
manufaa zaidi yakipatikana.
Alitoa pongezi hizo
Machi 6, 2018 alipofanya ziara kwenye mgodi huo uliopo Wilayani Nyang’hwale
Mkoani Geita ili kujionea shughuli ziazoendelea sambamba na kuzungumza na
watendaji wake.
Biteko aliitaka
kampuni hiyo kuendelea kufuata maelekezo ya Serikali ikiwemo kufuata sheria,
kulipa kodi na tozo mbalimbali za Serikali sanjari na kutunza takwimu za
uendeshaji wa shughuli zao kwa mujibu wa matakwa ya sheria.
Mara baada ya
kupokea taarifa ya mgodi huo, Biteko aliahidi kushughulikia changamoto
mbalimbali zinazoukabili mgodi huo ikiwemo suala la maeneo ya uchimbaji na
upatikanaji wa huduma ya nishati ya umeme.
“Suala la umeme nitalifikisha;
tunahitaji kuona maendeleo. Tunahakikisha tunaandaa mazingira mazuri kwa
wawekezaji wote wa ndani na nje,” alisema
Biteko.
Kuhusu suala la maeneo,
Biteko alisema wenye maeneo ambayo hawayaendelezi watafutiwa leseni na maeneo
hayo kugawiwa upya kwa wenye nia ya dhati ya kufanya maendeleo ikiwemo kampuni
hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Kampuni, Hussein Amar alimueleza Naibu Waziri Biteko mafanikio yaliyofikiwa
tangu mradi huo uanze kufanya kazi Mwaka 2013 ikiwemo ajira kwa wananchi wa
maeneo ya karibu na Watanzania kwa ujumla ambapo alisema mradi umeajiri wafanyakazi
wapatao 60.
Amar aliongeza kuwa
mradi huo unaunga mkono jitihada za maendeleo ikiwemo kuchangia ujenzi wa
vyumba vya viwili vya madarasa katika Sekondari ya Izunya, ujenzi wa Zahanati,
ujenzi wa Ofisi ya Mtendaji Kitongoji cha Ibalangulu na uanzishaji wa mradi wa
ufugaji nyuki kwa wananchi wanaozunguka mradi.
Aidha, Amar
alizungumzia changamoto mbalimbali zinazoukabili mradi huo ikiwemo ukosefu wa
maeneo ya uchimbaji hasa ikizingatiwa kuwa mradi huo unafunga mitambo ya
kuchenjulia dhahabu yenye uwezo wa kusaga mawe kiasi cha Tani 500 kwa Saa 24 na
kwamba inahitaji maeneo ili kufanya uchimbaji utakaokidhi mahitaji ya
uendeshaji wa mitambo hiyo.
Aliomba kusogezewa
huduma ya nishati ya umeme kwakuwa gharama kubwa inatumika kununulia mafuta kwa
ajili ya kuzalisha umeme hasa ikizingatiwa kuwa shughuli nyingi zinazofanyika
mgodini hapo zinahitaji nishati ya umeme.
Alisema endapo
huduma hiyo ya nishati itapatikana, mgodi utazalisha ajira zaidi kwani
uendeshaji wake utakuwa wa muda mrefu kwa kuwa na awamu nyingi (work shifts
addition) na kwamba mgodi huo kwa sasa umeajiri wafanyakazi 60.
“Tunazalisha umeme
wetu kwa kutumia mafuta; hii inasababisha gharama za uendeshaji kuwa kubwa.
Tunaomba Serikali itusogezee huduma ya nishati ili kupunguza gharama za
uendeshaji,” alisema Amar.
Naibu Waziri Biteko
amekamilisha ziara yake Mkoani Geita ambapo alitembelea maeneo mbalimbali ya
uchimbaji ili kujionea shughuli zinazofanyika na kuzungumza na wachimbaji kwa
utatuzi wa pamoja wa changamoto mbalimbali zinazowakabili.






No comments :
Post a Comment