MWANASHERIA WA MISUNGWI ASIMAMISHWA KAZI
*Ni baada ya kuisababishia halmashauri hasara ya sh. milioni
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwaamemsimamisha kazi Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya
Misungwi Bw. Alphonce Sebukoto na kuagiza achungunzwe na vyombo husika.
Amechukua hatua hiyo baada
Mwanasheria huyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni
pamoja na kushindwa kuishauri vema halmashauri hiyo na kuisababishia
hasara ya sh. milioni 279.
Waziri Mkuu amemsimamisha kazi
Bw. Sebukoto leo (Jumatatu, Februari 19, 2018) wakati akizungumza na
watumishi na madiwani wa halmashauri hiyo akiwa katika siku ya tano ya
ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
“Mwanasheria utasimama kazi
kuanzia leo na tuhuma zako zitachunguzwa kikamilifu na vyombo husika na
uchunguzi ukibaini kama huna kosa utarudi kazini. Hatuta kuonea lakini
hatuwezi kukuvumilia kwa utaratibu huo ulioufanya.”
Amesema mwanasheria huyo
Novemba 2017 wakati alipokuwa anakaimu nafasi ya ukurugenzi aliidhinisha
malipo ya sh.milioni 279 zilipwe katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti
wa Halmashauri hiyo Bw. Anthony Bahebe.
Waziri Mkuu amesema Bw. Bahebe
aliishtaki halmashauri hiyo akidai kulipwa fedha kwa ajili ya kazi ya
ukandarasi wa mradi wa maji Igenge uliojengwa na kampuni ya ukandarasi
ya Seekevim.
Amesema mradi huo ulianza 2014
na ulitakiwa ukamilike 2015. Mwanasheria huyo aliidhinisha malipo hayo
wakati ambao tayari hati maalumu ya uwakilishi ilikuwa imekwisha tangu
Desemba 2015.
“Mwanasheria amemlipa
Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kufanya kazi na Halmashauri baada ya
kuifikisha Halmashauri yake Mahakamani. Amemlipa fedha wakati kazi
yenyewe ilikuwa haijaisha na aliharakisha malipo hayo kipindi ambacho
Mkurugenzi hayupo.”
Waziri Mkuu amewakumbusha
watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utumishi na matakwa ya kisheria
katika utekelezaji wa majukumu yao. Amesema fedha alizolipwa Bw. Bahebe
zingeweza kutumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo
katika halmashauri hiyo.
Awali, Waziri Mkuu alifungua
mabweni ya watoto wenye mahitaji maalumu katika shule ya msingi Mitindo
iliyoko wilayani Misungwi na kisha alikagua ujenzi wa vyumba vya
madarasa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, FEBRUARI 19, 2018.
No comments :
Post a Comment