Mawaziri kutoka Malawi mara baada
ya kuwasili kwenye Ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam kwa
ajili ya majadiliano kuhusu masuala ya Nishati na mwenyeji wao Waziri wa
Nishati wa Tanzania, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani). Kushoto ni
Waziri wa Maliasili, Nishati na Madini, Aggrey Masi na Waziri wa
Viwanda, Biashara na Utalii, Henry Mussa.
Waziri wa Nishati wa Tanzania,
Dkt. Medard Kalemani (kushoto) wakati wa mkutano wa kujadili masuala ya
Nishati na Mawaziri kutoka Malawi (hawapo pichani).
Ujumbe wa Mawaziri kutoka Malawi
ukiendelea na majadiliano wakati wa mkutano na Waziri wa Nishati, Dkt.
Medard Kalemani (hayupo pichani). Kutoka kulia ni Waziri wa Maliasili,
Nishati na Madini, Aggrey Masi, Waziri wa Viwanda, Biashara na Utalii,
Henry Mussa na Balozi wa Malawi nchini, Hawa Ndilowe.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani (kushoto) akizungumza jambo wakati wa mkutano na Mawaziri
kutoka Malawi. Kulia ni Waziri wa Maliasili, Nishati na Madini wa
Malawi, Aggrey Masi.
Viongozi kutoka Wizara ya Nishati
na Taasisi zilizo chini yake wakiendelea na majadiliano. Kutoka kushoto
ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamis Mwinyimvua, Kaimu
Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga,
Afisa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ally Ubwa, Kaimu
Mkurugenzi Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mhandisi
Kapuulya Musomba na Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Nishati Jadidifu,
Edward Ishengoma.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani (katikati) katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Mawaziri kutoka
Malawi. Kutoka kulia ni Balozi wa Malawi nchini, Hawa Ndilowe, Waziri wa
Viwanda, Biashara na Utalii, Henry Mussa. Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu
Wizara ya Nishati Tanzania, Dkt. Hamis Mwinyimvua na Waziri wa
Maliasili, Nishati na Madini, Aggrey Masi mara baada ya kumalizika kwa
majadiliano ya masuala ya Nishati.
Ujumbe kutoka Malawi ukiendelea na
majadiliano wakati wa mkutano wa kujadili masuala ya Nishati na Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani).
………………
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani amekutana na Ujumbe wa Mawaziri wawili kutoka Malawi na
kuzungumza kuhusu uwezekano wa Malawi kupata Gesi Asilia kutoka Tanzania
na Uendelezaji wa pamoja wa Bonde la Mto Songwe kwa ajili ya matumizi
mbalimbali ikiwemo
uzalishaji umeme.
Ujumbe wa Malawi uliongozwa na
Waziri wa Maliasili, Nishati na Madini, Aggrey Masi na Waziri wa
Viwanda, Biashara na Utalii, Henry Mussa ambao waliambatana na Balozi wa
Malawi nchini, Hawa Ndilowe na wataalam kutoka Taasisi mbalimbali
zilizo chini ya wizara zao.
Waziri Kalemani alikutana na
ujumbe huo Februari 12, 2018 katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini
Dar es Salaam ambapo alielezwa dhumuni la ziara hiyo ya Mawaziri hao
wawili kutoka nchini Malawi.
Akizungumza katika mkutano huo,
Waziri wa Nishati wa Malawi, Aggrey Masi alisema kuwa Malawi inaupungufu
mkubwa wa nishati ya umeme na kwamba jitihada mbalimbali zinafanyika
kuhakikisha kiwango cha uzalishaji umeme kinaongezeka.
Alisema umeme unaozalishwa nchini
humo kwa sasa ni Megawati 140 pekee huku idadi ya watu ikiwa ni milioni
17 kiasi ambacho alisema kimeshindwa kukidhi mahitaji.
“Sasa hivi tumebaki na megawati
140 peke yake, hali siyo shwari; suluhisho la haraka linahitajika ili
kuweka mambo sawa. Imani yetu ni kwa Tanzania kutazama namna ya kusaidia
katika hili,” alisema.
Alibainisha kwamba chanzo kikuuu
cha uzalishaji wa umeme nchini humo ni maporomoko ya maji na kwamba
kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, chanzo hicho kimeshindwa kuzalisha
umeme wa kutosha kukidhi mahitaji ya kila siku.
Aliongeza kwamba Serikali ya
Malawi imeamua kuwa na vyanzo mbadala vya kuzalishia umeme ikiwemo Gesi
Asilia hata hivyo alisema hakuna Gesi Asilia inayozalishwa nchini humo
na kwamba matarajio yao ni kupata Gesi Asilia kutoka nchini Tanzania.
“Tumefarijika, tumepokelewa
vizuri, lengo la ujio wetu ni kubaini uwezekano wa kupata Gesi Asilia
kwa ajili ya kuzalisha umeme,” alisema Masi.
Alisema kwamba baada ya tathmini
waliyoifanya wamebaini kwamba chanzo cha haraka kinachoweza kuwasaidia
kuvuka kwenye upungufu mkubwa wa umeme uliyoikumba nchi hiyo kwa sasa ni
Gesi Asilia kutoka nchini Tanzania.
Aliongeza kuwa tayari mwekezaji
amepatikana ambaye atazalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia na kwamba
atajenga mitambo yake kwenye eneo la Kalonga mpakani mwa Tanzania na
Malawi.
Kwa upande wake Waziri Kalemani
alisema suala hilo linaweza kujadiliwa baada ya wataalam wa Tanzania
kujiridhisha uwezekano wake.
“Tupo tayari kushirikiana,
kinachohitajika hapa ni majadiliano ya kitaalam na wataalam wetu waliopo
hapa ili kuelewa mwelekeo,” alisema Waziri Kalemani.
Dkt. Kalemani aliwasisitiza
wataalam hao kabla hawajafanya majadiliano wanapaswa kuelewa mambo makuu
matatu ambayo wingi wa Gesi Asilia iliyopo kwa sasa, matakwa ya Sera ya
Nishati na namna ambavyo Gesi hiyo inaweza kusafirishwa hadi huko
Kalonga.
“Je tunayo gesi ya kutosha
kugawana ama ni ya kutosha kwa matumizi yetu tu? Je Sera inaruhusu suala
hilo? Na kama masuala hayo yanakubalika, Je ni vipi tutaifikisha hiyo
Gesi huko mpakani?” alihoji Dkt. Kalemani.
Aliueleza ujumbe huo kuandaa
mpango wa ombi lao kimaandishi pamoja na kuandika ombi rasmi na
kuwasilisha katika utaratibu maalum wa Kiserikali ili majadiliano
yafanyike.
Aidha, suala la Uendelezaji wa
pamoja wa Bonde la Mto Songwe, Mawaziri hao kwa pamoja walikubaliana
kupitia taarifa ya Tume ya Uendelezaji wa Bonde hilo ambayo inaundwa na
nchi hizo mbili ili kubaini hatua za kuchukua kwenye kipengele cha
kuzalisha umeme.
Miradi inayotarajiwa kutekelezwa
katika bonde hilo ni pamoja na ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme kiasi
cha Megawati 180 ambazo zitagawanya sawa kwa nchi hizo, kilimo cha
umwagiliaji, (hekta 6,200) usambazaji wa maji kwa wananchi, ujenzi wa
miundombinu ya jamii (bararabara, shule, na vituo vya afya).
Miradi mingine ni uanzishaji wa
viwanda vidogo na vya kati, uvuvi, utalii na uboreshaji wa mazingira,
hususan kuimarisha kingo za mto ambao ni mpaka wa Tanzania na Malawi.
No comments :
Post a Comment