Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Chisichili Kata ya Mkonze
mkoani Dodoma wakati wa ziara yake kujionea hali ya upatikanaji wa
umeme.
Mbunge wa Dodoma Mjini ambaye pia ni
Naibu Waziri kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira
na Vijana, Antony Mavunde (aliyesimama), akizungumza wakati wa ziara ya
Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (wa pili kutoka kulia), kujionea
hali ya upatikanaji wa umeme katika maeneo mbalimbali ya Dodoma Mjini.
Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu
(kulia) akibadilishana mawazo na wananchi wa Mtaa wa Chisichili, Kata
ya Mkonze mkoani Dodoma wakati wa ziara yake kujionea hali ya
upatikanaji wa umeme. Kulia kwake ni Mbunge wa Dodoma Mjini Antony
Mavunde.
Wananchi wakimsikiliza Naibu Waziri
Subira Mgalu (hayupo pichani) wakati wa ziara yake kujionea hali ya
upatikanaji wa umeme katika maeneo mbalimbali ya Dodoma Mjini.
Wananchi wakiuliza maswali na kutoa
maoni mbele ya Naibu Waziri Subira Mgalu (hayupo pichani) wakati wa
ziara yake kujionea hali ya upatikanaji wa umeme katika maeneo
mbalimbali ya Dodoma Mjini.
Na Veronica Simba – Dodoma
Serikali imebainisha kuwa jumla ya
shilingi bilioni 499 zimeidhinishwa na Bunge kwa ajili ya kutekeleza
miradi ya umeme nchini kote katika mwaka huu wa fedha unaoendelea.
Hayo yalisemwa jana, Januari 24 na
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiwa katika ziara katika maeneo
mbalimbali ya Dodoma Mjini kwa ajili ya kujionea hali ya upatikanaji wa
nishati hiyo muhimu pamoja na kuzungumza na wananchi.
Naibu Waziri Mgalu, ambaye
aliambatana na Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde aliwaambia
wananchi wa maeneo aliyotembelea kuwa, kiasi hicho cha fedha ni kikubwa
na kitawezesha utekelezaji wa miradi hiyo ya umeme katika vijiji vyote
7873 vilivyosalia nchi nzima.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais John
Magufuli pamoja na Bunge la Jamhuri kutuidhinishia kiasi hicho cha
fedha. Kazi yetu sisi wasaidizi wake katika Wizara ya Nishati ni
kuhakikisha tunatekeleza jukumu alilotutuma la kuwapelekea wananchi kote
nchini nishati ya umeme wa uhakika. Tunaahidi hilo litafanyika kwa
ukamilifu.”
Akizungumzia umuhimu wa nishati ya
umeme, Naibu Waziri alisema kuwa, sekta zote zinategemea umeme ili
zifanye kazi kwa ubora. Alitoa mfano wa sekta ya afya ambayo pasipo
umeme wa uhakika haiwezi kutoa huduma bora. “Vivyo hivyo kwa sekta ya
elimu, kilimo, viwanda na nyinginezo,” alisisitiza.
Aidha, Naibu Waziri Mgalu alitoa
maagizo kwa uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha
Wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo wanatoa kipaumbele kwa taasisi za
kijamii kama vile shule, vituo vya afya, nyumba za ibada, miradi ya maji
na nyinginezo. Hata hivyo alisema Wakandarasi lazima wahakikishe hakuna
mtu au eneo linalorukwa wakati wa kutekeleza mradi huo.
Vilevile aliwataka wananchi kufanya
maandalizi ya kuunganishiwa umeme katika makazi yao na katika miradi na
taasisi mbalimbali. “Tunataka zoezi la kupitisha umeme katika maeneo
yenu likikamilika tu nanyi bila kuchelewa mnaunganishiwa katika nyumba
zenu, hivyo anzeni kufanya maandalizi sasa.”
Awali, akizungumza katika ziara hiyo,
Mbunge Mavunde ambaye pia ni Naibu Waziri kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, alisema kuwa wananchi wa Dodoma
ni wakulima wazuri wa zabibu na mazao mengine mbalimbali, hivyo
wanahitaji huduma ya umeme wa uhakika ili kuboresha kazi zao za kilimo
kwa kuanzisha viwanda vya usindikaji ili kuongeza thamani.
Meneja wa Tanesco Mkoa wa Dodoma,
Mhandisi Zakayo Temu alisema zoezi la kufanya tathmini ya awali kwa
ajili ya kutekeleza Mradi huo katika maeneo yaliyosalia litaanza mapema
mwezi Februari mwaka huu.
Ziara ya Naibu Waziri Mgalu ilihusisha Kata za Mpunguzi, Matumbulu, Mkonze, Nala na Ipagala zilizopo Dodoma Mjini.
No comments :
Post a Comment