
Na. Mwandishi wetu
Usimamizi mzuri na utekelezaji wa
Sera mbalimbali za kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu kujenga na
kumiliki uchumi, kumeifanya Tanzania kuibuka kinara miongoni mwa nchi
zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kuwa na Uchumi Jumuishi
(Inclusive Economy) unaokua duniani.
Taarifa iliyotolewa na Word
Economic Forum kupitia mradi wake wa mradi wa ‘The Inclusive Development
Index’, imeitaja Tanzania kushika nafasi ya kwanza kwa nchi za Kusini
mwa Jangwa la Sahara na ya 48 kati ya nchi 103 zilizofanyiwa tathmini ya
nchi zenye Uchumi Jumuishi duniani,
Katika orodha ya kumi bora, nchi
zilizofuatia na nafasi ziliyoshika kidunia ni pamoja na Ghana (52),
Cameron (53), Burundi (55), Namibia (56), Rwanda (57), Uganda (59), Mali
(60), Senegal (61) na Nigeria (63).
Takwimu za ukuaji huu zinaakisi
moja kwa moja kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
John Pombe Magufuli ambaye amekuwa akielezea kutaka uchumi wa Tanzania
umilikiwe na wananchi kwa njia mbalimbali ikiwemo kutekeleza sera ya
uchumi wa viwanda ambapo watanzania wengi hivi sasa wamekuwa
wakitekeleza sera hiyo kwa kuanzisha viwanda vikubwa na vidogo.
Mtaalamu Mbobevu wa masuala ya
Uchumi na Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa
Honest Ngowi ameeleza kuwa takwimu zilizotolewa na taasisi hiyo
zinatafsiri kuwa uchumi wa Tanzania unaelekea kumilikiwa na watu wengi
zaidi jambo ambalo litasaidia kupunguza pengo la kipato kati ya
walionacho na wasionacho.
Profesa Ngowi ameeleza kuwa uchumi
wa aina hiyo unawashirikisha wananchi kumiliki uchumi na kuwafanya watu
wengi kufaidi matunda ya ukuaji wa uchumi wa nchi.
“Taarifa hizi ni njema kwani
kitaalam tunaita broad based economy ambapo watu wengi wanashirikishwa
kumiliki uchumi na wengi wanafaidi,” alieleza Profesa Ngowi na kuongeza
kuwa kuna nchi zingine zinauchumi mzuri lakini unamilikiwa na watu
wachache na kufanya kuwa na pengo kubwa kati ya walionacho na
wasionacho.

Katika siku za hivi karibuni,
Taasisi mbalimbali duniani zimekuwa zikitoa ripoti zikiielezea Tanzania
kupaa kiuchumi ambapo ripoti za Shirika la Fedha Duniani (IMF), Benki ya
Dunia (WB) na Taasisi ya Goldman Sachs ya Marekani hivi karibuni
zilitabiri kuwa wakati uchumi wa dunia utakua kwa wastani wa asilimia
3.0 hadi 4.0, ukuaji wa uchumi wa Tanzania unatajwa kuendelea kuwa kati
ya nchi tano bora za Afrika ukitarajiwa kukua kwa asilimia 6.5 hadi 7.0
katika mwaka 2018.
No comments :
Post a Comment