Saturday, January 20, 2018

SEKTA BINAFSI YARIDHISHWA NA UHUSIANO WAKE NA SERIKALI


IMG_9340
Baadhi ya Wawekezaji na wageni kutoka Taasisi za Kimataifa walioshiriki Mkutano wa tatu wa majadiliano kati ya wadau wa Sekta Binafsi na Sekta ya Umma uliofanyika mjini Dodoma.
IMG_9354
Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Bw. Salum Shamte, akizungumza wakati wa mkutano wa tatu kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma uliojadili namna ya kuboresha masuala ya biashara na uwekezaji nchini, mjini Dodoma.
IMG_9365
Baadhi ya Wafanyabiashara na Wawekezaji  walioshiriki Mkutano wa tatu wa majadiliano kati ya wadau wa Sekta Binafsi na Sekta ya Umma uliofanyika mjini Dodoma.
IMG_9366
Baadhi ya Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu na Maafisa wengine kutoka Wizara mbalimbali wakifuatilia mkutano kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma, Mjini Dodoma.
IMG_9384
Baadhi ya Wafanyabiashara na Wawekezaji  walioshiriki Mkutano wa tatu wa majadiliano kati ya wadau wa Sekta Binafsi na Sekta ya Umma uliofanyika mjini Dodoma.
IMG_9393
Sehemu ya wadau mbalimbali wakiwemo wabunge, wawekezaji na viongozi wa Serikali walioshiriki mkutano kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma, Mjini Dodoma.
IMG_9431
Baadhi ya wabunge wakifuatilia kwa makini mkutano wa tatu wa wadau wa Sekta Binafsi na Sekta ya Umma uliofanyika mjini Dodoma
IMG_9460
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akifungua mkutano wa tatu kati ya Sekta Binafsi na Serikali uliofanyika mjini Dodoma.
IMG_9506
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Elisante Ole-Gabriel, akionesha kabrasha lenye maelezo ya utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yaliyotekelezwa na yanayoendelea kutekelezwa baada ya mikutano miwili ya awali kufanyika Mjini Dodoma na Jijini Dar es Salaam.
IMG_9517
Baadhi ya Maafisa wa Serikali wakishiriki Mkutano wa tatu wa wadau kutoka Sekta Binafsi na Sekta ya Umma uliojadili namna ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini, mjini Dodoma
…………………………………………………………………………..
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Sekta Binafsi nchini imekiri kuwa uhusiano kati yake na Serikali umezidi kuimarika kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji na ufanyajibiashara hapa nchini kuliko ilivyokuwa hapo awali na kwamba hatua hiyo itachochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kauli hiyo imetolewa mjini Dodoma na Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Bw. Salum Shamte, wakati wa mkutano wa tatu kati ya Sekta Binafsi na Sekta
ya Umma uliojadili namna ya kukuza ushiriki wa Sekta Binafsi katika kukuza uchumi wa viwanda nchini.
“Sekta binafsi imenituma kuleta pongezi kwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutekeleza kwa vitendo utambuzi wa kwamba Sekta Binafsi ni mbia muhimu wa maendeleo ya Taifa letu” alisema Bw. Shamte.
Aliyataja baadhi ya mafanikio yanayo onekana bayana kuwa ni pamoja na kuinusuru Bandari ya Dar es Salaam kwa mabadiliko ya sheria ya fedha ya mwaka 2017 hasa kuondoa VAT kwenye biashara ya mizigo ya kimataifa na kuondokana na umoja wa forodha ambao ulipunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Bw. Shamte alisema kuwa majadiliano hayo kati ya Serikali na Sekta Binafsi kumeikoa sekta ya utalii hasa kwa kuondokana na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye leseni mbalimbali hatua ambayo imerejesha msisimko wa sekta hiyo.
“Serikali imepunguza pia  mlolongo wa kodi kwa wakulima, japokuwa – kazi haijakamilika lakini mwanzo ni mzuri” aliongeza Bw. Shamte
Alieleza kuwa jitihada mpya na nzuri za kutatua changamoto za kodi kwa kampuni zinazojihusisha na biashara kati ya Tanzania Bara na Visiwani, na kuanza kufanya malipo kwa wakandarasi na watoa huduma wa ndani hatua ambayo wanaamini itakuza matumizi ya ndani na mzunguko wa fedha.
Makamu mwenyekiti huyo wa TPSF alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni sikivu na kwamba kwa mara ya kwanza, wanatarajia kushuhudia Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2018/2019 ikiwa bora zaidi kwa kubeba mapendekezo yao mengi yatakayosaidia kukuza sekta hiyo na pia kuboresha masuala ya kodi na mapato ya Serikali.
Wakizungumza kwenye mkutano huo, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Bw. Charles Mwijage, wamesema kuwa Serikali inathamini mchango wa Sekta Binafsi katika maendeleo ya uchumi wa viwanda na kwamba itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta hiyo ikiwemo masuala ya kodi.
“Sekta Binafsi ndiyo mhimili wa uchumi kwa hiyo ni muhimu tuhakikishe upande wa Serikali tunafanya wajibu wetu kuiweesha Sekta hiyo iwe imara zaidi na iweze kukua kwa sababu tutapata ajira, bidhaa bora na huduma mbalimbali hatimaye kukuza uchumi wetu wa viwanda” alisisitiza Dkt. Mpango
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naye aliongeza kuwa Sekta Binafsi ndiyo itakayojenga viwanda wakati Serikali itakuwa mwezeshaji ndio maana wameamua kukaa  pamoja kujadili changamoto zinazozikabili pande zote mbili na kwamba baadae watajielekeza kujadili na kila Sekta ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi.
Wametoa wito kwa Sekta binafsi nchini kujenga uaminifu na kufuata sheria na kanuni za ufanyajibiashara na uwekezaji nchini ikiwemo kulipa kodi stahiki.
Akizungumza katika mkutano huo wa tatu uliojumuisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) hapa nchini, Bw. Andy Karas, ameimwagia sifa Tanzania kwa kukuza uchumi wake kwa wastani wa asilimia 7 na kushauri kuwa uchumi huo sasa uelekezwe kutatua changamoto za wananchi hususan kukuza sekta ya kilimo inayoa ajiri idadi kubwa ya watanzania.

No comments :

Post a Comment