NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi(CCM), Zanzibar, Dk. Abdulla Juma Mabodi akizungumza katika
tamasha la uchangiaji wa damu iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mjini na Magharib, katika Mnara wa Kumbukumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi
ya Zanzibar ulioko Kisonge,
BAADHI ya waandaji wa tamasha la uchangiaji damu kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Wanawake na Vijana.
BAADHI ya wananchi walioshiriki
tamasha la uchangiaji damu wakifuatilia matukio mbalimbali
yanayoendelea kwenye maeneo ya Kumbukumbu ya Mnara wa miaka 50 ya
Mapinduzi ya Zanzibar ulioko Kisonge.
KATIBU Msaidizi wa Chama Cha
Mapinduzi(CCM), MKoa wa Magharib Suleiman Mzee Suleiman akichangia damu
katika tamasha hilo la uchangiaji damu
…………………
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi(CCM), Zanzibar Dk.Abdalla Juma Saadalla ‘Mabodi’ amewataka
wananchi wa visiwani humu bila ya kujali tofauti zao za kisiasa, kidini
na kikabila kuwa na utamaduni wa kuchangia damu kwa hiari ili kuokoa
maisha ya wenzao husasan wanaopata ajali na akina mama wajawazito
wakati wa kujifungua.
Wito huo umetolewa jana katika
tamasha la uchangiaji wa damu salama lililofanyika katika...
Mnara wa
Kumbukumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ulioko Kisonge, ambapo
alisema mahitaji ya damu ni ya kila siku na kwamba kuna haja ya wananchi
kuwa na uzalendo wa kujitolea kwa ajili ya maisha ya wengine.
Naibu huyo Katibu Mkuu alifafanua
kuwa nchi zilizoendelea na zinazoendelea zimekuwa na viwanda vya
kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo vifaa tiba vya hospitalini, lakini
wameshindwa kutengeneza damu ya binadamu kwa ajili ya matumizi ya
kitiba
Pia, alisisitiza kuwa lazima
wananchi watambue kuwa benki ya damu ni wao wenyewe na hakuna kampuni
wala kiwanda kinachoweza kuzalisha damu hiyo.
“Wananchi sisi wenyewe ndio wenye
jukumu la kuzalisha damu kwa ajili ya kuiweka katika benki ya damu ili
itumike kwa ajili ya mtu yeyote anayehitaji huduma hiyo tena kwa
wakati,” alisema Dk.Mabodi.
Akizungumzia faida ya utoaji wa
damu kitaalamu alisema kuwa mtu anapotoa damu anapunguza vichocheo vya
hasira pia damu inapotoka mwilini inatoa fursa ya kutengeneza damu
nyingine mpya inayokuwa na uwezo mkubwa wa kiutendaji katika mzunguko wa
damu mwilini.
Hata hivyo, alisema kwamba matukio
ya ajali za aina mbalimbali pindi yanapotokea huku wa kina mama
wajawazito wanaojifungua wanahitaji damu hiyo na kwamba lazima utamaduni
wa kutoa damu upewe kipaumbele.
Naye Ofisa Uhamasishaji kutoka
Mpango wa Damu salama Zanzibar, Omar Said Omar amezipongeza taasisi
zilizoandaa tamasha hilo la kuchangia damu na kwamba litasaidia
kupunguza vifo vinavyotokana na ukosefu wa damu.
Alisema matarajio ya kitengo
hicho ni kupata zaidi ya chupa za damu 1,000 ambazo kwa matumizi yake
chupa moja utumika kwa watu watatu ambao wanaohitaji huduma za
kimatibabu.
Wakizungumza kwa wakati tofauti
baadhi ya wananchi, askari wa majeshi ya ulinzi na Idara maalum za SMZ
pamoja na wananchi walioshiriki kuchangia damu waliahidi kuwa mabalozi
wazuri wa kuwahamasisha wananchi wengine kujitokeza kuchangia damu.
Kwa upande wake Koplo Suleiman Ali
kutoka kituo cha Jeshi la Polisi la Ng’ambo, aliwashauri askari
wwenzake kuwa mstari wa mbele katika kuchangia damu kwa lengo la kuunga
mkono kampeni za uchangiaji wa damu.
Naye Nassor Othman Mkaazi wa
Kisauni Unguja, alieleza kuwa amekuwa ni mdau wa kuchangia damu kwa
miaka Sita na wakati mmoja kati ya familia yake wanapohitaji damu
wanapata huduma hiyo bila tatizo.
No comments :
Post a Comment