Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof.
Ibrahim Juma akijiandaa kuanza Matembezi ya uzinduzi wa wiki ya Sheria
leo jijini Dar es salaam. Kulia kwake ni mkewe akifuatiwa na Jaji Mkuu
wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu na kushoto ni Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba
na Sheria Prof. Sifuni Mchome pamoja na Askofu wa Kanisa la Anglican
Nchini.
Gari linaloonesha Mfano wa
Mahakama inayotembea. Hivi karibuni Mahakama ya Tanzania itaanzisha
Mahakama zinazotembea (Mobile Courts) ili kupunguza mlundikano wa kesi
Mahakamani.
Jaji Mkuu akiwa ndani ya gari hilo
………………….
Na Lydia Churi-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma amewataka Watumishi wa Mahakama nchini kutoa huduma
kwa kuzingatia Maadili, kuhakikisha kesi zinamalizika kwa wakati pamoja
na kuacha vitendo vya rushwa ili kuongeza imani ya wananchi kwa Mhimili
huo.
Akizindua wiki ya Sheria na
Maonesho ya Elimu ya Sheria leo katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini
Dar es salaam, Jaji Mkuu alisema kuwa nguvu ya Mahakama ni imani ya
wananchi na imani hiyo itaongezeka ikiwa hakuna rushwa, kuna maadili
mema na kesi
zitamalizika kwa wakati.
Jaji Mkuu pia amewataka wananchi
kuacha kuilalamikia Mahakama na badala yake wachukue hatua kwa kuwataja
watumishi wasiozingatia maadili kwa uongozi wa Mahakama.
Aidha, amewashauri wananchi
kujifunza na kuelewa taratibu za mashauri Mahakamani ili kurahisisha
upatikanaji wa haki zao wanapozitafuta kwenye Mahakama mbalimbali
nchini.
“Wananchi wengi wanakwenda
kutafuta haki sehemu isiyohusika hivyo wanatakiwa kujifunza taratibu za
Mahakama ili waweze kupata haki kwa wakati kwa kuwamuda mwingi unapotea
kwa kutafuta haki mahali pasipostahili”, alisema Prof. Juma.
Alisema hivi sasa Mahakama
inaingia kwenye matumizi ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano- TEHAMA
hivyo matumizi haya yatamsaidia mwananchi kuweza kufahamu hatua zote za
shauri lake lililopo Mahakamani.
Jaji Mkuu ametoa wito kwa wananchi
kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Mnazi Mmoja ili kupata elimu
juu ya masuala mbalimbali yanayohusu Mahakama na sekta ya sheria kwa
ujumla.
Alisema, katika maonesho hayo,
wananchi watapata nafasi ya kujifunza juu ya usuluhishi nje ya Mahakama,
Mahakama inayotembea (Mobile Courts) pamoja na changamoto za
upatikanaji wa haki zikiwemo upungufu wa Watumishi, Miundombinu, pamoja
na vifaa.
Akizungumzia taratibu wa
usuluhishi wa kesi nje ya Mahakama (Mediation), Jaji Mkuu amesema wakati
sasa umefika kwa wananchi kutumia utaratibu huo unaorahisisha
upatikanaji wa haki na kuongeza kuwa Haki bora hupatikana kwa usuluhishi
majumbani.
Aidha, kabla ya kuzindua wiki ya
Sheria, Jaji Mkuu aliongoza Matembezi waliyowashirikisha watumishi wa
Mahakama, wadau pamoja na wananchi kwa ujumla yaliyoanzia katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mpaka viwanja vya Mnazi Mmoja.
Matembezi hayo pia yalihudhuriwa
na viongozi wa Serikali akiwemo Waziri wa wakati katiba na Sheria Mhe.
Prof. Palamagamba Kabudi, Katibu Mkuu wa wizara hiyo Prof. Sifuni
Mchome pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon
Mpanju.
No comments :
Post a Comment