*Waziri Mkuu ataka wampe maelezo ya kina upotevu wa mali za mabilioni
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewanusuru viongozi 19 wa vyama vikuu vya
ushirika vya mikoa ya Shinyanga (SHIRECU) na Mwanza (NCU) kwenda selo na
badala yake amewapa siku 23 wampe maelezo yatakayomridhisha juu ya
mahali zilipo mali za vyama hivyo viwili.
Amefikia
uamuzi huo leo (Ijumaa, Desemba 22, 2017) wakati akifunga kikao cha
siku moja cha wadau wa zao la pamba alichokiitisha mkoani Shinyanga.
Viongozi hao wanatuhumiwa kwa upotevu wa mali zilizokuwa zikimilikiwa na
vyama hivyo vya ushirika.
“Nataka
kila mtu akaandae taarifa kuhusu mali za ushirika zilipo, au zimeenda
wapi na kama mlizikopea, mseme ni wapi, lini na kwa ridhaa ya nani.
Nataka maelezo ya kutosha kuniridhisha mali za ushirika zimeenda wapi,”
alisema Waziri Mkuu.
“Hawa
nitakaowataja walipaswa kuchukuliwa na RPC, wakatoe maelezo yao na
hatua dhidi yao zichukuliwe. Sasa nataka nikutane nao Dodoma ifikapo
Januari 15, 2018 saa 3:30 asubuhi ofisini kwangu,” alisisitiza.
Kuhusu
tuhuma za viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mwanza (Nyanza
Cooperative Union – NCU), Waziri Mkuu alisema chama hicho kati ya mwaka
2001 na 2017, kilikuwa jumla ya mali 10 ambazo ziliuzwa kinyemela
katika mazingira yenye utata na kwa bei ndogo ikilinganishwa na thamani
halisi ya mali hizo zilizopo jijini Mwanza.
Aliwataja viongozi waliohusika na upotevu huo ambao wanatakiwa kutoa maelezo yao kuwa ni Murtazar
Alloo ambaye ni mnunuzi wa maghala matatu mali ya NCU, Bw. Samson
Ng’halida (mnunuzi wa New Era Oil Mills), Bw. Amos Njite Lili (mnunuzi
wa ghala la Igogo), Bi. Antonia Zacharia (mnunuzi wa jengo la KAUMA),
Bw. Timothy Kilumile (mnunuzi wa jengo la KAUMA), Bw. Robert Kisena
(mnunuzi wa pili wa New Era Oil Mills), Bw. Peter Ng’hingi (aliyekuwa
Mjumbe wa Bodi), Bw. Daniel Lugwisha (aliyekuwa Mhasibu Mkuu – NCU), Bw.
George Makungwi (aliyekuwa Afisa Miliki – NCU) na Bw. Sospeter Ndoli
(aliyekuwa Afisa Utumishi -NCU).
Kuhusu
mali za Nyanza zinazoshikiliwa na benki ya CRDB. Waziri Mkuu alisema
benki hiyo inaidai NCU mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 2.123 na
kwamba benki hiyo inashikilia mali 16 zenye thamani ya sh. bilioni
18.132. Alitaka vyombo vya dola vifanye uchunguzi ili kubaini uwiano wa
mikopo na mali zinazoshikiliwa na benki ya CRDB.
Kwa
upande wa viongozi wa SHIRECU, Waziri Mkuu alisema wanatuhumiwa kwa
upotevu wa zaidi ya sh. bilioni 11 ambazo wanadaiwa na benki ya TIB
yakiwemo madeni ya mishahara ya watumishi ambayo yanafikia sh. bilioni
1.2.
“SHIRECU kwa sasa haina mali zozote kwa sababu mali zote zinashikiliwa na TIB kutokana na mikopo,” alisema.
Aliwataja viongozi wa SHIRECU ambao wanatakiwa kutoa maelezo yao kuwa ni Bw. Joseph
Mihangwa (Meneja Mkuu), Bw. Sillu Mbogo (Kaimu Mhasibu Mkuu), Bw.
Maduhu Nkamakazi (Kaimu Mkaguzi wa Ndani), Bw. James Kusekwa (Kaimu
Meneja Uendeshaji) na wajumbe wa Bodi ya SHIRECU.
Wajumbe
hao wa Bodi ni Bw. Robert Mayongela (Mwenyekiti), Bi. Mary Mabuga
(Makamu Mwenyekiti), Bw. Sigu Maganda (Mjumbe), Bw. Clement Bujiku
(Mjumbe) na Bw. Charles Lujiga.
Waziri
Mkuu ambaye aliwasili mkoani humo leo asubuhi, alikwenda kwanza kukagua
kiwanda cha kutengeneza nyuzi cha JOC na kisha kurejea ukumbini
kuendelea na kikao cha wadau wa pamba ambacho kimeshirikisha wakuu wa
mikoa 16, wabunge, ma-RAS, wakuu wa wilaya, wakulima, wanunuzi wa pamba
na wenye viwanda.
Waziri Mkuu ameondoka Shinyanga kuelekea Ruvuma ambako atakuwa na ziara ya siku moja.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, DESEMBA 22, 2017
No comments :
Post a Comment