Jonas Kamaleki- MAELEZO
TMS Consultants Ltd imejiandaa
kutoa ajira 6000 nchini katika juhudi za ujenzi wa viwanda na kupunguza
tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.
Hayo yameelezwa leo jijini Dar es
Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya TMS Consultants Ltd,
Sebatian Kingu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Akifafanua kuhusu ajira hizo,
Kingu amesema kuwa kampuni yake itajenga mtandao wa matawi 6,000 nchi
nzima ya Tanzania hivyo kufikisha huduma zake hadi vijijini badala ya
kuishia mijini.
“Kwa kutumia mtandao wa matawi
yetu ya mtindo wa Franchasing, TMS kwa makubaliano ya kimkataba na
taasisi ka za Mifuko ya Hifadhi za jamii kama vile NSSF, PPF, PSPF,
LAPF, tutaweza kuzifikisha huduma huduma hadi vijijini ambapo wao hawana
ofisi lakini wana huduma za wakulima, wavuvi, wafugaji na wajasiriamali
wengine wadogo wadogo”, alisema Kingu
Kingu amesema matawi hayo yatamilikiwa na wananchi wenyewe ambao watakuwa wanatoa faida kwa TMS.
Bwana Kingu amesema kuwa ipo
mitaji ya kutosha kwa wale wanotaka kuwekeza katika viwanda vidogo, vya
kati na vikubwa na kwamba kinachohitajika ni kuingia ubia na wenye
mitaji.
“Tunashirikiana na kampuni 10,000
Duniani ambazo ziko tayari kutoa mitaji kwa njia ya ubia na watanzania,
hivyo hatuna shaka na fedha za mtaji”, alisema Kingu.
Amewashauri wananchi watumie hiyo fursa ili azima ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda iweze kutimia.
Aidha Kingu amempongeza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa
jitihada zake za kukuza uchumi kwa kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa
ikiwemo ya ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge), kufufua Shirika
la Ndege la Tanzania (ATCL) ambalo sasa linazo ndege tatu na utekelezaji
wa mradi mkubwa wa umeme wa Steglers Gorge ambao utazalisha megawatt
2100 na kuondoa tatizo la umeme nchini.
Pia Rais amepongezwa kwa vita yake
ya uchumi hasa kupambana na ufisadi, kulinda rasilimali za taifa
ikiwemo madini na maliasili nyinginezo na kurudisha nidhamu katika
utumishi wa umma.
Amewataka watanzania kumuunga
mkono Rais Magufuli kwa kuwekeza katika viwanda ambavyo vitatumia
rasilimali za humu nchini na hivyo kupanua wigo wa ajira.
Kingu amesema kuwa zipo huduma
mpya za Bima amabazo zimewalenga wakulima na wafugaji ambao wanafanya
shughuli za kibiashara lakini haziwafikii.
Ameongeza kuwa huu ni wakati
muafaka kwa mfumo uliojengwa kwa kipindi kirefu, takriban miaka 25
kuwezesha upatikanaji wa huduma hizo kuwa endelevu badala ya kumtegemea
mwanzilishi, hivyo mfumo wa matawi hayo utakuwa na uwezo wa kujiendesha
wenyewe.
Katika Mpango wa Maendelo ya miaka
mitano wa 2016/17-2020/21 inakadiriwa kuwa Miradi ya Maendeleo ya
Serikali itahitaji kiasi cha TZS. trililioni 107. Kati ya hizo TZS
trililioni 59 ambazo ni 55% zinategemewa zitokane na vyanzo vya Serikali
na trililioni 48 sawa na 45% zinategemewa zitokane na Sekta binafsi kwa
mtindo wa ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi (PPP)
No comments :
Post a Comment