Monday, December 4, 2017

KANUNI ZA MAADILI YA TAALUMA YA MAWASILIANO KWA UMMA KUANDALIWA


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bw.Nicolaus William(kushoto) na Rais wa Chama cha Uhusiano wa Umma Tanzania (PRST)  Bw.Loth Makuza (kulia) wakionyesha Katiba ya chama hicho kwa wanataaluma ya mawasiliano kwa umma waliyohudhuria uzinduzi wa chama hicho (hawapo pichani)   leo jijini Dar es Salaam.
NA ANITHA JONAS – WHUSM
Idara ya Habari Maelezo pamoja na Chama cha Uhusiano wa Umma Tanzania (PRST) wametakiwa  kuungana kwa pamoja na kuandaa Kanuni za Maadili ya Taaluma ya Mawasiliano kwa Umma kwa kuzingatia maslai ya taifa.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bw.Nicolaus William alipokuwa akizindua chama cha PRST chenye lengo la kuongeza ueledi kwa wanataaluma ya mawasiliano kwa umma nchini .
“Ningependa kuona chama hichi kinakuwa mstari wa mbele katika kutoa mafunzo mbalimbali kwa wanataaluma wake kama lilivyolengo kuwa chama kitajikita zaidi katika kuongeza weledi kwa wanatansia pamoja na kuleta mabadiliko ya kiutendaji katika sekta ya mawasiliano nchini kwa kulingana na mahitaji ya soko,”Bw.William.
Akiendelea kuzungumza katika uzinduzi huo Naibu Katibu Mkuu huyo alisisitiza kuwa ni vyema wadau wote wa taaluma ya mawasiliano kwa umma watambue umuhimu wa chama hichi kwani wao ndiyo wenye dhamana ya kukikuza,kukiendeleza na kukijengea misingi imara itakayodumu na kuleta tija ndani ya taifa.
Kwa upande wa Mwakilishi wa Msemaji Mkuu wa Serikali kutoka Idara ya Habari Maelezo Bw.Jonas Kamaleki alieleza kuwa serikali inaunga mkono jitihada za kuanzishwa kwa PRST na iko tayari kutoa ushirikiano wakati wote.
“Serikali ingependa chama hichi kuwa na mikakati madhubuti na utekelezaji  wenye tija na hata kuwa mfano kwa Afrika Mashariki bila ya kujali kuchelewa kwa kuanzishwa kwake,”Bw.Kamaleki.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Shule ya Habari na Mawasiliano kwa Umma Dkt.Dietrick Kaijanangoma alitoa nasaha kwa Maafisa Uhusiano wa taasisi mbalimbali nchini ya kuwataka kuwa wabunifu na kufanya tafiti ndogo na kubwa kwa ajili ya kuimarisha taasisi zao na zaidi kujifunza kwenda na wakati kwa kutambua mahitaji ya umma.
Pamoja na hayo nae Rais PRST Bw.Loth Makuza alitoa shukrani kwa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania  Awamu ya Tatu Mhe.Benjamin William Mkapa kwa kuanzisha sekta ya habari nchini
Halikadhalika Bw.Makuza alitoa ombi kwa taasisi mbalimbali kuunga mkono uanzishwaji wa chama hicho  pamoja na wanataaluma kujitokeza kwa wingi na kujiunga na chama utaratibu wa kujiunga unapatikana kupitia tovuti ya www.prst.or.tz.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bw.Nicolaus William (watatu kushoto) akikata utepe wa Katiba ya Chama cha Uhusiano wa Umma Tanzania (PRST) kuashiria kuzinduliwa kwa chama hicho leo jijini Dar es Salaam,aliyeshika Katiba hiyo (kulia) ni Rais wa PRST Bw.Loth Makuza.

 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bw.Nicolaus William(wanne kushoto)akimkabidhi cheti  Bw.Innocent Mungy kilichotolewa na uongozi wa chama Chama cha Uhusiano wa Umma Tanzania (PRST)  kwa kutambua mchago wake katika kuanzishwa kwa chama hicho mara baada ya uzinduzi  wake jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya viongozi wa Chama cha Uhusiano wa Umma Tanzania (PRST) wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bw.Nicolaus William(aliyeketi wanne kushoto) mara baada ya uzinduzi wa chama hicho leo jijini Dar es Salaam na  watatu kutoka kulia) ni Rais wa PRST Bw. Loth Makuza.

No comments :

Post a Comment