Saturday, December 30, 2017

BALOZI SEIF AFUNGUA MKUTANO MKUU WA CCM MKOA WA MAGHARIBI

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Viongozi wa CCM Mkoa Magharibi alipofika kuufungua Mkutano wao wa Uchaguzi uliofanyika katika Ukumbi wa Zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni.
Balozi Seif akiufunguza Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Mkoa wa Magharibi wa kuwachaguwa Viongozi wao wa kuwaongoza katika kipindi cha miaka Mitano ijayo kuanzia 2017 – 2022.
Baadhi ya Wajumbe wa Makutano Mkuu wa CCM Mkoa Magharibi wakiwa katika mchakato wa kuwachagua Viongozi wa Kuuongoza Mkoa huo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Baadhi ya Wajumbe wa Makutano Mkuu wa CCM Mkoa Magharibi wakiwa katika mchakato wa kuwachagua Viongozi wa Kuuongoza Mkoa huo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mwenyekiti WA CCM Mkoa Magharibi aliyemaliza Muda wake Nd. Yussuf Mohad Yussuf akitoa nasaha na kuwashukuru wanachama na Viongozi wa Mkoa huo alioshirikiana nao na kumuwezesha kutekeleza majukumu yake katika muda wake wa utumishi wa Miaka 15 kwenye nafasi hiyo.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi amesema wakati umefika kwa Wananchama wa Chama cha Mapinduzi kutowapa nafasi za Uongozi wanachama wenye tabia ya kuhama Jimbo moja na kuhamia Jimbo jengine.

Alisema Wanachama hao hufikia uamuzi wa kuyakimbia Majimbo yao ya zamani na kutaka kuhamia majimbo mapya baada ya kujibaini kutowatumikia vyema Wanachama na Wananchi wao katika kipindi walichoomba ridhaa ya kuwawakilisha katika nafasi za Ubunge na Uwakilishi kwenye vipindi vya awali.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Magharibi wa kuwachagua Viongozi watakaouongoza Mkoa huo kwa kusaidiana na viongozi wengine katika kipindi cha Miaka Mitano ijayo 2017 – 2022 ambao ulifanyika katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Alisema uzoefu umebainisha wazi kwamba Wawakilishi na Wabunge wanaoendelea na majukumu yao ndani ya Majimbo yao hukumbwa na matatizo ukiwemo ushawishi, fitna na majungu yanayobuniwa na wale wanaotaka nafasi hizo jambo ambalo huchangia kukosekana kwa uwajibikaji.

Akigusia suala la Uchaguzi ndani ya Chama Balozi Seif alisema Wanachama wenye kufaa kuchaguliwa ndani ya Chama cha Mapinduzi ni wale waliojaa sifa za ziada kupita wengine katika kujenga Umoja na Mshikamano kwenye Taasisi hiyo ya Kisiasa.

Alisema sifa hiyo ya Wanachama lazima iende sambamba pia na uwezo wa Kiongozi huyo wa kuwashawishi wasiokuwa Wanachama kujiunga na Chama hicho katika kukijengea nguvu za kuendeleza ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa Mwaka 2020.

Alieleza kazi ya Chama chochote cha Siasa ni kushika Dola. Hivyo kwa Mantiki hiyo Chama cha Mapinduzi katika mabadiliko makubwa kinachoendelea kuyafanya katika kupanga safu za Uongozi kuanzia ngazi ya Shina hadi Taifa kinahitaji Viongozi watakaokiletea ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu huo.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Wanachama wanapaswa kuzingatia muelekeo wa Viongozi wa Chama chao katika kuwachagua Wanachama watakaowapeleka huo kwenye chaguzi zilizobakia hata kama watakuwa na sura mbaya.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliwanasihi Viongozi watakaochaguliwa kuwa wabunifu hasa katika kukifanya chama hicho kuwa na nguvu za ziada za kujitegemea kifedha badala ya kusubiri kutembeza bakuli kwa wahisani.

Balozi Seif alitahadharisha wazi kwamba utegemezi siku zote unawajengea nguvu wale wanaowategemea, jambo ambalo baadhi ya wahisani hao wanaweza kutumia fursa hiyo kukiyumbisha Chama kirahisi.

Alitoa wito kwa Uongozi utakaochaguliwa uelewe fika kwamba utakuwa na jukumu la kusimamia na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020 kwa kivitendo kama inavyoelezwa katika Sura ya Nane.

Aliwapongeza Viongozi hao wa Mkoa Magharibi kwa kutekeleza Katiba ya CCM ya Mwaka 1977 toleo la 2017 Ibara ya 87 {4} ya kufanya Uchaguzi wa kuchagua Viongozi wao wa CCM Mkoa unapofikia wakati wa uchaguzi.

Akizungumzia shamra shamra za kuadhimisha miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar zinazoanza rasmi Jumapili ya Tarehe 31 Disemba Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Viongozi, Wanachama na Wananchi wote Nchini kushiriki kwenye sherehe hizo.

Alisema itapendeza kuona Wananchi wote wanaendelea kushiriki kila mwaka kwa kuungana na Watendaji wa Serikali sambamba na kujitokeza kwa wingi kwenye kilele cha sherehe za maadhimisho hayo zitakazofikia kilele chake katika Uwanja wa Michezo wa Amani Mjini Zanzibar.

Akisoma Risala ya Mkoa wa Magharibi Katibu wa CCM wa Mkoa huo Bibi Aziza Ramadhan Mapuri alisema Chama cha Mapinduzi Mkoani humo kimepata mafanikio makubwa katika kujenga upendo miongoni mwa Wanancha.

Alisema upendo huo umeuwezesha Uongozi wa Mkoa huo kuisimamia vyema Serikali kwenye ngazi ya Mkoa katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 – 2020.

Bibi Aziza alifahamisha kwamba katika kipindi cha Miaka Mitano inayomalizika hivi sasa CCM Mkoa wa Magharibi umefanikiwa kupata eneo kwa ajili ya Ujenzi wa Ofisi ya Kisasa ya Mkoa itakayoambatana na uwepo wa vitega uchumi vitakachouwezesha Mkoa huo kujitegemea wenyewe na kujiepusha na utegemezi.

Akigusia changamoto zinazoukabili Mkoa huo Katibu huyo wa CCM Mkoa Magharibi alisema uhamiaji mkubwa unaokwenda sambamba ujenzi holela ndani ya eneo hilo umeleta athari kubwa hata za kimazingira.

Alisema ujenzi huo wa makaazi usiozingatia athari za kimazingira hasa katika maeneo ya kilimo na vianzio vya Maji unastahiki kuangalia vyema na Serikali Kuu katika hatua za kukabiliana nayo ikiwemo kuwachukuliwa hatua za kisheria wale waliohusika na uharibifu huo.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi aliyemaliza muda wake Ndugu Yussuf Moh’d Yussuf alisema chaguzi zilizokuwa zikiendelea ndani ya chama kuanzia ngazi ya Shina hadi Mkoa ni matukio muhimu ya kuendeleza Demokrasia ndani ya Chama.

Ndugu Yussuf alisema katika kipindi chake cha utumishi wa nafasi hiyo katika kipindi cha Miaka 15 ameshuhudia mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Chama cha Mapinduzi ndani ya kipindi kifupi jambo ambalo wanastahiki kupongezwa Viongozi pamoja na Wanachama wenyewe.

No comments :

Post a Comment