Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akihutubia wahitimu na wageni waalikwa
katika mahafali ya 31 ya Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP)
mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akiwashudia wahitimu wakiwa wanavaa kofia
(hawapo pichani) baada ya kuwatunuku tuzo za fani mbalimbali kwenye
mahafali ya 31 ya Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) mjini
Dodoma.
Wahitimu wa Chuo Cha Mipango ya
Maendeleo Vijijini (IRDP) wakivaa kofia zao mara baada ya kutunukiwa
tuzo mbalimbali katika mahafali ya 31 ya Chuo hicho mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akimtunuku mhitimu Felista Mayunga Shahada
ya Uzamili katika Uchumi wa Maendeleo katika mahafali ya 31 ya Chuo Cha
Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati) akiwa na viongozi wa Chuo na
wageni waalikwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa Stashahada za
Uzamili na Shahada za Uzamili katika mahafali ya 31 ya Chuo Cha
Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) mjini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)
……………………………………………………………..
Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amewataka Wahitimu 3108 wa Chuo
Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) waliotunukiwa tuzo zao
katika Fani mbalimbali kwa mwaka 2016/2017 kuwa ...
sehemu ya suluhisho
katika changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi nchini pindi
watakapoanza kuwatumikia wananchi hao na siyo kuwa sehemu ya matatizo
katika jamii.
Akizungumza katika mahafali hayo
ya 31 ya Chuo hicho yaliyojumuisha Kampasi ya Dodoma na Mwanza
yaliyofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere
Chuoni hapo Maeneo ya Miyuji
mjini Dodoma Dkt. Kijaji amesema kuwa elimu waliyoipata wakaifanyie kazi
kwa uhalisia wa maisha ya Wananchi waliopo maeneo mbalimbali ili
kuliwezesha Taifa kufikia uchumi wa kati hata kabla ya 2025 kama Dira ya
Taifa linavyotuelekeza.
‘Wahitimu wetu wana deni, deni
hilo ni utumishi uliotukuka. Nendeni mkawatumikie Watanzania nendeni
mkairejeshe imani ya Watanzania iliyoanza kupotea kwa Wataalam wa fani
ya Mipango ya Maendeleo Vijijini’. alisema Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji aliongeza kwa
kuwataka Wahitimu hao kwenda kuwafundisha Watanzania kwa vitendo mipango
na mbinu thabiti ili waweze kuzalisha kwa tija kwa ajili ya maendeleo
ya Taifa letu na ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Aidha Dkt. Kijaji alisema kuwa
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli
haitokuwa tayari kuwavumilia Wataalamu wazembe makazini na kuwataka
wakafanye kazi kwa weledi mkubwa kwa manufaa ya Taifa.
Dkt. Kijaji amefafanua kuwa
Serikali itaendelea kuhakikisha watoto wa kitanzania wanapata elimu bora
itakayowaongezea maarifa ili kuwa chachu katika Maendeleo ya Taifa.
‘Serikali inatekeleza majukumu
yake kwa vitendo, ndiyo maana mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu
inapewa kipaumbele cha kwanza (first charge). Alisema Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji ametoa wito kwa
Taasisi za Elimu ya Juu zote Nchini kutoa mafunzo yatakayowawezesha
Wahitimu mbalimbali kuweza kujiajiri pindi wamalizapo masomo yao ili
kuongeza kasi ya uchumi nchini.
Katika hatua nyingine Dkt. Kijaji
amekipongeza Chuo hicho kwa utoaji wa elimu bora katika fani mbalimbali
kwa kuwa idadi ya wanachuo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka na
kwamba huo ni mfano tosha kuwa taaluma inayopatikana katika Chuo hicho
ni nzuri na kutoa rai kwa wananchi wengine kuleta watoto wao kupata
taaluma mbalimbali.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa
Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Prof. Hozen Mayaya amesema
kuwa wameendeleza, kuboresha na kudumisha mahusiano bora kati ya Chuo
na wadau mbalimbali.
Prof. Mayaya aliongeza kuwa
ushirikiano mzuri wa wadau wao umekuwa kichocheo kikubwa katika
kutekeleza majukumu yao makuu ya kufundisha, kufanya utafiti na kutoa
huduma za ushauri na uelekezi kwa wadau mbalimbali.
‘Chuo kinajivunia kuongeza
udahili wa Wanafunzi 6,129 kwa mwaka 2016/17 kutoka wanafunzi 4,916 kwa
mwaka 2015/16 ikiwa ni ongezeko la asilimia 24’. aliongeza Prof. Mayaya.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la
Uongozi wa Chuo hicho Prof. Razack Lokina katika hotuba yake ya
kumkaribisha Mgeni Rasmi amesema kuwa Uongozi wa Chuo umeendelea
kutekeleza wajibu wake wa kuandaa wataalamu wa mipango ya maendeleo hasa
vijijini ambako watanzania wengi wanaishi.
‘Utekelezaji wa wajibu huu
umeendana sambamba na kuongeza uwezo wa Chuo katika kutoa mafunzo
yanayozingatia umahiri, kufanya tafiti na kutoa huduma za uelekezi
katika Nyanja zote za mipango ya maendeleo’. aliongeza Prof. Lokina.
Katika mahafali hayo ya 31 ya
Chuo hicho jumla ya wahitimu 3,108, wanawake 1,631 wanaume 1,477
wamehitimu ngazi ya Astashahada, Stashahada, na Shahada za Uzamili.
No comments :
Post a Comment