MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amewataka wahandisi na watu wote
ambao wanasimamia sekta hiyo kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na
uaminifu katika kazi zao ili kuchochea Tanzania ya uchumi wa kati.
Mbarawa aliyasema hayo jana
wakati wa hafla ya kukabidhiwa...
Tuzo ya Heshima ya Rais wa Shirika la
Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA), iliyotolewa kwa Mtendaji Mkuu
wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS),Mhandisi Patrick Mfugale.
Alisema wahandisi wengi hasa
wanajihusisha na ujenzi wa miundombinu wanakosa uaminifu, uadilifu na
uwajibikaji hali ambayo inachangia ubovu katika miradi wanayosimamia.
Waziri alisema uamuzi wa JICA
kumpa tuzo ya heshima Mfugale ni jambo la kupongezwa na la kuigwa na
wataalam mbalimbali hasa katika sekta ya ujenzi.
“Napenda kutumia nafasi hii
kuwaomba wahandisi wenzako waige mfano wako katika kazi ili nao siku
moja waweze kupata tuzo hii ya heshima ya JICA ambayo umeipata kutokana
na jitihada zao katika kusimamia majukumu yako,” alisema.
Waziri Mbarawa alisema tangu
aingie katika wizara hiyo amekuwa akijifunza mambo mengi kupitia kwa
Mfugale hivyo anaamini tuzo hiyo imetolewa kwa mtu sahihi.
Akizungumza katika hafla hiyo
Mwakilishi Mkazi wa JICA, Toshio Nagase alisema shirika hilo limetoa
tuzo hiyo kwa Mfugale kutokana na uwajibikaji wake kwenye sekta ambayo
anaisimamia.
“Hii ni tuzo ya 13 ya Rais wa
JICA ambayo ni ya utambuzi wa heshima kwa watu binafsi wataalam,
wataalam washauri, wafanyakazi wa kujitolea na miradi kwa mchango wao wa
kufanikisha katika Nyanja za rasilimali watu na Mfugale amefanya hilo,”
alisema.
Alisema katika tuzo hiyo ya
heshima ya Rais wa JAICA ya mwaka huu watu binafsi 26 kote duniani
wamepata mmoja wapo akiwa Mfugale kutoka Tanzania, vikundi sita miradi
tisa na wafanyakazi wakujitolea watatu.
Nagase alisema mchango wa Mfugale
katika miundombinu umeanza tangu mwaka 1977 wakati alipoajiriwa wizara
ya ujenzi kama mtaalam msaidizi huku akisimamia miradi ya JAICA tangu
mwaka 2007.
Kwa upande wake Balozi wa Japani
nchini Masaharu Yoshida alisema uamuzi wa JAICA kutoka tuzo hiyo kwa
Mfugale ni ishara tosha kuwa Tanzania inaushirikiano mzuri na Japani.
Yoshida alisema nchi yake
itaendelea kusaidia Tanzania katika sekta mbalimbali huku akiwata
wasimamizi wa miradi mingine ambayo inapata msaada wa JIICA kuuiga mfano
wa Mfugale.
Akizungumzia tuzo hiyo Mhandisi
Mfugale alisema ameipokea kwa heshima kunbwa huku akiweka bayana kuwa
tuzo hiyo inatokana na mchango mkubwa wa wizara, wafanyakazi wenzake na
JAICA kwa ujumla.
Mtendaji mkuu huyo wa TANROADS
aliwataka wafanyakazi wenzake kuongeza jitihada kazini ili siku nyingine
tuzo hiyo ya heshima ya Rais wa JAICA wapewe wao.
“Siamini kuwa nina kitu cha ajabu
ila naamini kuwa ushirikiano baina yetu ndio mafanikio yangu hivyo ni
wakati muafaka kwa kila mmoja kusimamia eneo lake kwa faida ya nchi na
wananchi,” alisema.
Mfugale alisema iwapo kila mmoja
atasimamia nafasi yake kikamilifu upo uwezekano wa Tanzania ya viwanda
kufikiwa ifikapo 2025 kama lilivyolengo la Serikali na Rais John
Magufuli.
No comments :
Post a Comment