Tunapenda kuukumbusha umma wa
Watanzania kwamba maambukizi ya VVU na UKIMWI bado ni tatizo katika nchi
yetu. Takriban watu 1,400,000 wanakadiriwa kuwa na VVU. Hivyo katika
mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI Serikali inaendeleza afua mbalimbali ili
kuzuia maambukizi mapya. Asilimia 40% ya maambukizi mapya yanatokea
miongoni mwa vijana wenye umiri wa miaka 15-24. Aidha makundi maalum
kama vile wanaojidunga madawa ya kulevya, wanaofanya biashara ya ngono
na wale wanaoamiiana wa jinsia moja wako katika hatari kubwa ya kupata
maambukizi. Makundi mengine ya walio katika hatari ni waendesha magari
ya masafa marefu, wavuvi na wananchi wa kwenye migodi.
Wizara inatekeleza afua mbalimbali
ikiwa ni pamoja na ushauri nasaha na kupima uwepo wa VVU, na kisha
kuanza tiba na matunzo, pamoja na kutoa dawa za kufubaza kwa watakao
kuwa na maambuzi ya VVU. Kuna afua pia za kuzuia maambukizi ya mama
kwenda kwa mtoto, kutoa elimu ya VVU/UKIMWI na afya uzazi kwa vijana,
elimu kuhusu VVU/UKIMWI kwa jamii na tohara kwa wanaume. Matumizi ya
kondom ni moja wapo ya afua katika kuzuia maambukizi mapya. Hata hivyo
utafiti wa viashiria vya Malaria na UKIMWI wa mwaka 2011/12 umebaini
kuwa kuna matumizi duni ya kondom, kwani ni asilimia 27 tu ya watu wenye
wenza zaidi ya mmoja waliokiri kutumia kondom mara ya mwisho
walipofanya ngono. Hivyo Serikali itaendelea kununua na kusambaza kondom
kwa lengo la kuzuia maambukizi ya VVU, magonjwa ya ngono na mimba
zisizo tarajiwa ikiwa ni mojawapo ya afua hizo za kudhibiti maambukizi
ya VVU.
Tunasisitiza kuwa Wizara na wadau
wake inaendelea kutoa elimu ya kondom sambamba na elimu ya kusubiri
kufanya ngono kwa wale ambao hawajaanza na wale ambao wameanza lakini
wanapaswa kusubiri (Abstinence) na elimu ya kuwa waaminifu kwa mwenza
mmoja aliye mwaminifu na anaejua hali yake ya maambukizi ya VVU (Be
faithfull). .
Hivi sasa nchini kuna vyanzo vya
upatikanaji wa kondom vya aina tatu. Kwanza ni kondom zinazopatikana
kupitia sekta ya umma ambazo husambazwa na Serikali kwa wananchi bila
malipo. Pili, kuna kondom zinazosambazwa na wadau ambazo zinauzwa kwa
bei ya chini kwa kuwa wadau wamechangia. Mfano kondom za Salama na Dume,
na chanzo cha tatu ni kondom za kibiashara ambazo zinauzwa kwa bei ya
kati na ya juu.
Kondom za sekta ya umma husambazwa
kupitia vituo vya kutolea huduma za afya na huduma za mkoba ngazi ya
jamii, Kondom za wadau na zile za biashara husambazwa katika maduka ya
dawa, maduka ya bidhaa mbambali, baa na nyumba za wageni.
Kwa mwaka 2016/17 Serikali
iliboresha kondom zinazopatikana kupitia ya sekta ya umma kwa kuipa
kifungashio kipya na jina la ZANA, ambapo kondom 36,916,911
zilisambazwa. Kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2018 hadi 2020
Serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa Dunia wa kudhibiti malaria, UKIMWI
na Kifua Kikuu inatarajia kununua kondom za kiume takribani
500,000,000. Kondom hizi zitasambazwa kupitia vituo vya kutolea huduma
za afya na katika maeneo hatarishi yanayoaminika kuwa na watumiaji
wengi. Aidha, kwa vile imebainika kuwa watu ambao hawaumwi hawaendi
vituo vya afya kwa ajili ya kuchukua kondom tu na hivyo kupelekea
kutofikia walengwa, usambazaji na ugawaji huu utalenga maeneo ambayo
Kunamatukio ambayo yanaendana na
ngono na yana walengwa wa afua za kondom. Maeneo haya ni kama baa,
nyumba za kulala wageni, maeneo yenye mikusanyiko ya magari ya masafa
marefu, maeneo ya uvuvi na migodini.
Aidha ikumbukwe kwamba nchi yetu
ina sera sheria, mila, desturi na maadili yetu kama watanzania, Hivyo
kondom zote haziruhusiwi kusambazwa bila kufuata miongozo ya Wizara, ili
kulinda zisifike kwa wasiolengwa.
Hivyo basi, iwapo tunataka kuzuia
na kumaliza maambukizi ya VVU na UKIMWI ifikapo 2030 tunapaswa kama nchi
kuwekeza katika kuzuia maambukizi mapya. Matumizi ya kondom, ununuzi wa
vifaa tiba, vitendanishi, dawa za ARV na za magonjwa nyemelezi ni afua
muhimu. Tunaomba wanahabari na wananchi waunge mkono juhudi hizi kwa
kuwa tunahitaji watanzania wenye afya bora na uwezo wa kuzalisha ili
kuijenga Tanzania ya Viwanda.
Imetolewa na:
KATIBU MKUU – AFYA
30 Novemba, 2017
No comments :
Post a Comment