TGNP Mtandao leo imefanya warsha
na baadhi ya wenyeviti wa halmashauri pamoja na mameya lengo likiwa ni
kujadili kwa pamoja changamoto anuai zinazoukumba mchakato wa bajati
tangu ngazi za mitaa na vijiji.
Warsha hiyo ya siku mbili
inayofanyika katika Ukumbi wa Ofisi za TGNP Mtandao Mabibo jijini Dar es
Salaam imeshirikisha viongozi hao
kutoka Wilaya nane yaani Kishapu,
Tarime, Morogoro Vijijini, Mbeya Vijijini, Kisarawe, Ilala, Ubungo na
Kinondoni.
Akiwasilisha mada kabla ya
majadiliano, Ofisa Programu Uchambuzi na Machapisho wa TGNP Mtandao, Bw.
Deogratius Temba alisema washiriki watapata fursa ya kujadili mikakati
na kuweka mipango ya namna ya kushughulikia masuala anuai ya bajeti
yenye mrengo wa kijinsia ili kuhakikisha masuala ya kijinsia yanapewa
kipaumbele katika mipango na utekelezaji wa bajeti.
Alisema zipo changamoto
mbalimbali ambazo zimeibuliwa kutokana na tafiti shirikishi ngazi za
kijamii, yakiwemo masuala ya huduma zisizo ridhisha kwenye sekta ya
afya, elimu, maji na maeneo mengine kama kilimo na uchimbaji ambapo
watajadili na kushirikishana nini kifanyike kukabiliana na changamoto
hizo.
Ufuatiliaji na tathmini ya
utekelezaji wa sera kwa mrengo wa kijinsia inayofanywa na TGNP
inawasaidia kupata taarifa zinazowawezesha kushauri watunga sera na
wafanya maamuzi na wadau mbalimbali kuhusu masuala ya jinsia hususan
kuziba mwanya wa kijinsia.
No comments :
Post a Comment