Rais wa Chama cha watoa huduma za
afya binafsi Dkt. Omary Chillo (katikati) akifafanua jambo kwa waandishi
wa habari (hawapo pichani) kuhusu kongamano la nne la kitaifa la afya,
kushoto ni Katibu wa chama hicho Dkt. Rebeca John na kulia ni Afisa
Tawala wa chama hicho Bw. Joseph Mhagama.
Afisa Tawala wa Chama cha watoa
huduma za afya binafsi Bw. Joseph Mhagama akifafanua jambo kwa waandishi
wa habari (hawapo pichani) kuhusu kongamano la nne la kitaifa la afya,
katikati ni Rais wa chama hicho Dkt. Omary Chillo na kushoto ni Katibu
wa chama hicho Dkt. Rebeca John.
Katibu wa Chama cha watoa huduma
za afya binafsi Dkt. Rebeca John (kushoto) akisisitiza jambo kwa
waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kongamano la nne la kitaifa
la afya, katikati ni Rais wa chama hicho Dkt. Omary Chillo na kulia ni
Afisa Tawala wa chama hicho Bw. Joseph Mhagama.
Picha na Eliphace Marwa – Maelezo
………………
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Taasisi ya Tanzania Health
Summit imeandaa Kongamano la Afya kwa ajili ya kujadili changamoto
mbalimbali zinazoikumba sekta hiyo na...
k utoa mapendekezo ya utatuzi wa
changamoto hizo.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar
es Salaam na Rais wa Taasisi hiyo, Dkt. Omari Chillo wakati akizungumza
na Waandishi wa Habari kuhusu maandalizi ya kongamano hilo.
Dkt. Chillo amesema kuwa
maandalizi ya Kongamano hilo yanaendelea vizuri hivyo mnamo Novemba
14-15 mwaka huu wanategemea kufanya Kongamano katika Ukumbi wa Kimataifa
wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (JNICC).
“Lengo kuu hasa la mkutano huu
ni kuchangia juhudi za Serikali katika kuboresha afya kwa kujadiliana
changamoto zinazokabili sekta ya afya na kuishia na mapendekezo
yanayoonyesha suluhisho la majadiliano hayo ambayo huandikwa kwenye
kitabu na kusambazwa kwa taasisi husika za afya na kufuatilia
utekelezaji wa yaliyoandikwa kwa taasisisi hizo,” alisema Dkt. Chillo.
Ameongeza kuwa, Kongamano la mwaka
huu litahusisha vipengele mbalimbali vikiwemo vikao vitakavyogusa mada
kama maendeleo ya huduma za afya, hotuba kutoka kwa wataalamu wazoefu wa
afya, kuwasilisha matokeo ya uchunguzi na majadiliano katika vikundi.
Vile vile kutakuwa na maonesho ya huduma na bidhaa kutoka kwa wasambazaji wa huduma za afya na mashirika ya umma na binafsi.
Dkt. Chillo amefafanua kuwa katika
siku mbili hizo za mkutano wanatarajia kupata wadau wa afya takribani
500 kutoka ndani na nje ya nchi wakiwemo manesi, madaktari, wafamasia,
watunga sera, watafiti wa magonjwa ya afya, wachumi, wasambazaji wa
vifaa tiba na dawa, wawekezaji katika sekta ya afya pamoja na wadau wote
wa maendeleo ya afya.
Kwa upande wake Katibu wa Taasisi
hiyo, Dkt. Rebeka John amesema kuwa Kongamano hilo linatoa fursa chache
za udhamini na maonyesho hivyo wanaohitaji kushiriki wanatakiwa kujaza
fomu ya maombi inayoweza kupakuliwa kupitia tovuti ya www.ths.or.tz., kutuma barua pepe kwenda info@ths.or.tz, au kwa namba ya simu +2555 684 244 377.
“Ningependa kutoa wito kwa wadau
wa afya kutoka serikalini na mashirika binafsi, mahospitali, asasi
zisizo za kiserikali, taasisi za kitaaluma, watengenezaji wa bidhaa za
afya, wasambazaji, wawekezaji na washirika wa maendeleo kushiriki
kikamilifu katika mkutano wa mwaka huu,” alisema Dkt Rebeka.
Pia, amewashukuru wadhamini wao
wakuu wa kongamano hilo wakiwemo Tindwa Medical And Health Services,
Chuo cha Mtakatifu Joseph, Gazeti la The Guardian, Chuo cha Afya
Muhimbili, Blogu ya Issa Michuzi na Medico Press.
Huu ni Mkutano wa nne kufanyika
nchini ukiwa na kauli mbiu inayosema “Ni jinsi gani tunaweza kufikia
malengo ya kuimarisha upatikanaji wa afya bora kwa kuunganisha tafiti za
kisayansi, ubunifu na sera za afya”.
No comments :
Post a Comment