Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na kiongozi na mbashiri mkuu wa Jumuiya ya
waislamu wa Ahmadiya Tanzania,Tahir Mahmood, kabla ya kufungua mkutano mkuu wa
48 wa jumuiya hiyo Mbande, Temeke, Jijini Dar es salaam Oktoba 1, 2017.
NA OWM, DAR ES SALAAM
WAZIRI
Mkuu Kassim Majaliwa amewaomba Viongozi wa Jumuiya na Taasisi zote za kidini
nchini wahakikishe wanawapiga vita watu wote wanaopanga na kutaka kuvuruga
amani na utulivu uliopo nchini kwa sababu watakwamisha maenendeleo.
Amesema
Serikali inaelewa kwamba dini ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya maendeleo ya
ustaarabu wa mwanadamu kwani inatoa elimu ya maadili mema yenye kuwafanya
waumini waepukane na maovu mbalimbali.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumapili Oktoka 01, 2017) wakati akifungua mkutano
Mkuu wa mwaka wa 48 wa Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya uliofanyika katika eneo
la Kitonga kata ya Msongola wilayani Ilala, Dar es Salaam.
Amesema
kila Mtanzania anatakiwa ahakikishe anadhibiti matukio yote yenye viashiria vya
uvunjifu wa amani kwa kutoa taarifa katika mamlaka husika.”Tanzania ni nchi
salama na yenye utulivu, hivyo ni lazima wote tushirikiane kuitunza.”
“Napenda
niwahakikishieni kuwa Serikali inaunga mkono juhudi za Jumuiya za kidini katika
kupiga vita maovu ya kila aina; mathalan utumiaji wa dawa za kulevya, wizi,
rushwa, uzinzi ambao husababisha madhara mengi ukiwemo ugonjwa wa UKIMWI.”
Amesema
iwapo dini zetu zitatumika vizuri tutaweza kwa haraka sana kutekeleza agizo la
Rais Dkt. John Magufuli la 'Hapa kazi tu' kwani kila mtu ataepuka uzembe
na kuwajibika ipasavyo.
Waziri
Mkuu amesema ana imani kwamba jumuiya hiyo kama zilivyo taasisi zingine za
kidini itaendeleza kazi kubwa ya kupambana na maovu katika jamii yetu kwa
kuwapatia waumini wao na wananchi kwa ujumla elimu na maarifa ya kuboresha
tabia zao na maadili yao kiroho.
Amesema
amani na utulivu uliopo nchini unatokana na mambo mengi ikiwemo na wananchi
kupata ustawi, kuweza kufanya shughuli zao vizuri na kuwa na imani na Serikali
yao, ambayo imejiwekea mikakati ya kuhakikisha wananchi hususan wanyonge
wanapata faraja ndani ya nchi yao.
Waziri
Mkuu amesema mambo yameweza kupatikana baada ya Serikali kupambana na rushwa na
ufisadi pamoja na kuimarisha maadili ya watumishi wa umma, ambayo vimekuwa ni
vyanzo vya kupotea kwa amani na utulivu katika baadhi ya nchi.
“Serikali imeweka mikakati
madhubuti ya kupambana na ufisadi, kupitia mikataba mibovu na kuimarisha
maadili ili kujenga imani kwa wananchi, kuondoa migongano na tofauti ya kipato,
kuwa na matumizi mazuri ya rasilimali za umma, kuleta tija kwa kuongeza thamani
ya huduma na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.”
Awali, Amir na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu
Waahmadiyya Tanzania, Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry amesema Jumuiya hiyo
imekuwa ikifanya mikutano kila mwaka kwa lengo la kukumbushana misingi sahihi
ya dini tukufu ya kiislam pamoja na kukuza undugu wao.
Sheikh Chaudhry amesema
mkutano wa mwaka huu umejumisha watu zaidi ya 4,000 kutoka mikoa yote ya
Tanzania Bara na Visiwani pamoja na wageni kutoka nchi za Uingereza, Canada,
Rwanda, Uganda, Ujerumani, Kenya, Burundi, Malawi na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya
Congo (DRC).
Amesema Jumuiya hiyo mbali na
masuala ya kidini pia inatoa huduma mbalimbali za kijamii kama elimu, maji na
afya kwenye mikoa tofauti tofauti nchini.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea kitabu kutoka kwa Katibu wa Malezi Jumuiya ya
waislamu wa Ahmadiya Tanzania, Mahmood Hamsin, baada ya kufungua mkutano mkuu
wa 48 wa jumuiya hiyo Mbande, Temeke, Jijini Dar es salaam Oktoba 1, 2017.
(kulia) ni. kiongozi na mbashiri mkuu wa Jumuiya ya waislamu wa Ahmadiya
Tanzania,Tahir Mahmood.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na waumini wa Jumuiya ya waislamu wa Ahmadiya
Tanzania, kabla ya kufungua mkutano mkuu wa 48 wa Jumuiya hiyo huko Mbande,
Temeke, Jijini Dar es salaam Oktoba 1, 2017. (PICHA NA OFISI
YA WAZIRI MKUU)
No comments :
Post a Comment