Mkurugenzi Mkuu wa WCF Masha Mshomba
(kulia), akimkabidhi Dk.Arnold Mtenga, cheti cha ushiriki wa mafunzo ya tathmini ya ajali na majeraha
kwa mfanyakazi aliyeumia wakati akitekeleza majukumu yake mahala pakazi.
Na Christian Gaya. Mtanzania, Alhamis, Agosti 3, 2017
Watu wenye kipato cha
chini hutumia muda mwingi mahali pa kazi huku kipato kikiwa hakitoshi kumudu
maisha. Katika nchi yoyote ile uhalali au kukubalika kwa uchumi kunategemea
haki za msingi za ajira, sawa na uwezo wa ...
kufanya kazi unaohitajika ili uchumi
kukua.
Pia kuimarika kwa
haki za kazi na za kijamii kunategema soko la kiuchumi lenye ufanisi na
linalofanya kazi vizuri. Hii inaendana na kubadili mtindo wa siku zote wa
uzalishaji duni, mapato ya chini na kuhatarisha maisha kazini na nafasi yake
kuchukuliwa na utekelezaji wa kanuni za kimsingi za haki mahali pa kazi pamoja
na ajenda ya mazingira bora ya kazi, pamoja na mkakati wa kuhakikisha usalama
na fursa kwa wafanyakazi.
Dira iliyowekwa na
shirika la kazi duniani inasema “Iwapo mazingira ya kazi yaliyopo yanajumuisha
udhalimu, ugumu wa maisha na ufukara kwa idadi kubwa ya watu na hivyo
kusababisha vurugu kubwa sana kiasi kwamba yanahatarisha amani na utulivu
duniani; uboreshaji wa mazingira hayo unahitajika kwa haraka sana”.
Shirika la kazi
duniani limeingiza dira hii katika ajenda ya kazi zenye staha ambayo
inajumuisha matamanio ya watu ya kuwa na ajira ya kudumu yenye kuzalisha kipato
ambayo inatoa kipato kwa haki, usalama mahali pa kazi na ulinzi wa kijamii,
uhuru wa watu kueleza matatizo yao, kuandaa na kushiriki katika maamuzi ambayo
yanaathiri maisha yao na kupata fursa usawa na kuwatendea haki.
Ili kukidhi matakwa ya
mikataba ya kimataifa kuhusu fidia kwa wafanyakazi, Serikali ya Tanzania
imeunda mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi (WCF) ambao ni Taasisi ya Hifadhi ya
Jamii.
Mkurugenzi mkuu wa WCF Masha
Mshomba anasema Lengo la kuanzishwa kwa mfuko huu ni kushughulikia masuala ya
Fidia kwa Wafanyakazi waliopo katika sekta ya umma na binafsi Tanzania bara
ambao wataumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi wanazozifanya kwa mujibu
wa mikataba ya ajira zao.
"Malengo yake ni
kukidhi matakwa ya mikataba ya kimataifa kuhusu fidia kwa wafanyakazi kwa
kulipa fidia stahiki pale mfanyakazi atakapoumia, kuugua ama kufariki,
kutekeleza matakwa ya sera ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2003, na kutekeleza
matakwa ya kifungu cha 5 cha sheria ya fidia kwa wafanyakazi sura 263 marejeo
ya mwaka 2015" anasema Mshomba.
Mfuko wa WCF una utaratibu wa
kuwezesha kuharakisha malipo ya fidia kwa wafanyakazi ama wategemezi wao, una
utaratibu mzuri wa kupokea michango
kutoka kwa waajiri na kufanya malipo.
"Kukuza na kuendeleza
mbinu za kuzuia ajali, magonjwa ama kifo mahali pa kazi, kutoa huduma za ukarabati
na ushauri nasaha na kukidhi matakwa ya kimataifa kuhusu fidia kwa wafanyakazi
ndiyo baadhi ya malengo ya WCF", anasema.
Majukumu ya WCF ni kusajili
waajiri wote, kufanya tathmini ya mazingira mahali pa kazi, kukusanya na
kupokea michango kutoka kwa waajiri, na kuwekeza michango iliyokusanywa kwenye
vitega uchumi.
"Mfuko hulipa fidia
stahiki, hukuza mbinu za kuzuia ajali, magonjwa ama vifo vinavyotokana na kazi,
hutoa elimu ya umma juu ya mfuko na hutunza kumbukumbu za matukio ya ajali, magonjwa
ama vifo kutokana na kazi" Mshomba anataja zaidi majukumu ya mfuko.
Anasema mfuko huu wa fidia
kwa wafanyakazi unatoa mafao ya huduma
ya matibabu, malipo ya ulemavu wa muda, malipo ya ulemavu wa kudumu, malipo kwa
anayemhudumia mgonjwa, huduma za ukarabati na ushauri nasaha, msaada wa mazishi
na malipo kwa wategemezi endapo mfanyakazi atafariki.
Christian
Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni Tanzania, mshauri na mtaalamu wa
masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi: gayagmc@yahoo.com unaweza kutembelea www.hakipensheni monitor
online na hakipensheni blog Simu
+255 655 13 13 41 info@hakipensheni.co.tz
No comments :
Post a Comment