Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (kulia) akielezea
Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda
hadi katika Bandari ya Tanga nchini Tanzania unaotarajiwa kuzinduliwa
Agosti 05, 2017 huko Chongoleani mkoani Tanga katika mahojiano maalum
kwenye kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Shirika la Utangazaji
la Taifa (TBC) kupitia kituo chake cha TBC1 jijini Dar es Salaam
tarehe 03 Agosti, 2017. Kushoto ni mwongozaji wa kipindi hicho, Elisha
Elia
Mwongozaji wa kipindi cha Jambo
Tanzania kutoka Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Elisha Elia
(kushoto) akifafanua jambo katika mahojiano hayo. Kulia ni Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo akielezea utekelezaji
wa Miradi ya Umeme Vijijini Awamu ya Tatu inayosimamiwa na Wakala wa
Nishati Vijijini (REA) kwenye kituo cha redio cha TBC
……………………
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo amesema kuwa Bandari
ya Tanga inatarajia kuwa ya kimataifa kabla na baada ya...
kukamilika
kwa Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini
Uganda hadi katika Bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Dkt. Pallangyo aliyasema hayo
tarehe 03 Agosti, 2017 jijijni Dar es Salaam kupitia mahojiano maalum
kwenye kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Shirika la
Utangazaji la Taifa (TBC) kupitia kituo chake cha TBC1 lengo likiwa ni
kuelezea uzinduzi wa Mradi wa Bomba hilo utakaofanyika Agosti 05,
2017.
Alisema kiasi cha Dola za
Marekani milioni 200 kinatarajiwa kupatikana kama kodi wakati wa ujenzi
na kuongeza kuwa mradi utatoa takribani ajira 10,000 kwa watanzania
hususan katika maeneo yatakayopitiwa na miundombinu ya Bomba hilo.
Alisema Serikali kupitia Wizara
ya Nishati na Madini imejipanga katika kuhakikisha kila mwananchi
aliye karibu na miundombinu ya Bomba hilo anakuwa sehemu ya uchumi wa
bomba husika kupitia ajira na utoaji wa huduma mbalimbali.
Aidha, alitoa rai kwa wananchi
husuan waliopo katika maeneo yatakayopitiwa na bomba hilo kujinga na
Jumuiya ya Watoa Huduma Katika Sekta ya Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS)
itakayokuwa na jukumu la kuwaunganisha watoa huduma wote na kuwapa
elimu ya namna bora ya kupata mikopo katika taasisi za serikali na
kutoa huduma bora kwa kampuni zitakazojenga bomba hilo.
Akielezea usalama wa bomba hilo,
Dkt. Pallangyo alisema Serikali imepanga mkakati maalum wa utoaji elimu
kwa wananchi waishio karibu na miundombinu ya Bomba ili wawe walinzi na
kufunga mfumo maalum wa usalama kwenye Bomba.
Katika hatua nyingine, akielezea
maandalizi ya Tanzania kuelekea kwenye uchumi wa Gesi na Mafuta, Dkt.
Pallangyo alisema Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imekuwa
ikitoa ufadhili kwa wataalam wake na wanafunzi wanaofanya vizuri katika
masomo ya Sayansi kwenda kusoma nje ya nchi masuala ya Mafuta na Gesi.
Aliongeza kuwa, kozi kuhusu
masuala ya Mafuta na Gesi imekuwa ikitolewa katika vyuo vikuu kama
vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM) na Chuo cha Madini Dodoma (MRI).
Akielezea utekelezaji wa Miradi ya
Umeme Vijijini Awamu ya Tatu inayotekelezwa na Wakala wa Nishati
Vijijini (REA), Dkt. Pallangyo alisema utekelezaji utahusisha
vipengele vitatu ambavyo ni pamoja na kusambaza umeme katika maeneo
ambayo hayajafikiwa kabisa na miundombinu ya umeme na kuongeza wigo wa
usambazaji umeme katika vijiji ambavyo vimefikiwa na miundombinu ya
umeme lakini baadhi ya maeneo na vitongoji havikuungwa.
Aliendelea kueleza kuwa Kipengele
cha Tatu kinahusisha usambazaji wa umeme utokanao na vyanzo vya
Nishati Jadidifu kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi hususan
visiwani.
Alisisitiza kuwa lengo la REA Awamu ya Tatu ni kuhakikisha kuwa vijiji vyote nchini vinafikiwa na umeme ifikapo mwaka 2021
Wakati huo huo, akielezea mradi wa
kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Stiegler’s Gorge wenye uwezo wa
kuzalisha Megawati 2100, Dkt Pallangyo alisema kuwa maandalizi
yameshaanza kwa timu ya wataalam kupitia tafiti mbalimbali zilizowahi
kufanywa kuhusu mradi huo na kubadilishana uzoefu na wataalam kutoka
nchi ya Ethiopia ambao ni wazoefu kwenye ujenzi wa mabwawa na mitambo
ya kuzalisha umeme kwa njia ya maji.
Alisema kukamilika kwa mradi huo
kutapelekea nchi kupata Umeme wa uhakika na kuchochea kuongezeka kwa
uwekezaji kwenye uchumi wa Viwanda.
No comments :
Post a Comment