Mwandishi Wetu – MAELEZO
Kufuatia wito wa Rais John Pombe
Magufuli alioutoa hivi karibuni, hadi kufikia jana tarehe 01 Agosti,
2017 jumla ya wakimbizi 6,700 raia wa Burundi wameshajiorodhesha kurejea
nchini mwao kwa hiari.
Kufuatia hatua hiyo, Mkutano wa
pande tatu utakaojumuisha Serikali za Tanzania, Burundi na Shirika la
Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) unatarajiwa kufanyika mwishoni wa mwezi huu
kujadili namna ya kuwarejesha nchini mwao wakimbizi hao kwa kuzingatia
sheria za ...
kimataifa zinazohusu wakimbizi.
Katika mahojiano na mwandishi
wetu ofisi kwake jana, Mkurugenzi Idara ya Huduma za Wakimbizi katika
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bwana Harrison Mseke alieleza kuwa
tangu kutolewa kwa wito huo, Wizara imekuwa ikiwamahasisha wakimbizi hao
wa kujiorodhesha kwa hiari ili waweze kurejea nyumbani.
Akiwa katika ziara yake kwenye
mikoa ya Kanda ya Ziwa, Rais Magufuli alitoa wito kuwataka wakimbizi
raia wa Burundi kurejea nyumbani kwa hiari kwa kuwa hali ya usalama
nchini mwao ni nzuri ambapo wakati akitoa wito huo tarehe 20 Julai, 2017
huko Ngara aliambatana na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunzinza ambaye
nae aliwahakikishia wakimbizi hao kuwa hali ni shwari nchini Burundi.
Kwa mujibu wa Bwana Mseke, hivi
sasa kuna wakimbizi raia wa Burundi 276,692 kati ya wakimbizi 348,019
walioko nchini. Wengine ni wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo (DRC) 70,840, Wasomali 150, na wengine (mchanganyiko) 337.
Alifafanua kuwa kati ya idadi
hiyo ya wakimbizi raia wa Burundi 242,340 waliingia nchini baada ya
mwezi Aprili, 2015 kufuatia machafuko ya kisiasa nchini humo.
Akizungumzia mwendo wa uingiaji
wakimbizi kutoka Burundi, alieleza kuwa kwa sasa kasi imepungua kutoka
wastani wa wakimbizi 1,000 kwa siku kati ya mwezi Agosti hadi Disemba,
2016 hadi wastani wa wakimbizi kumi kwa siku katika miezi ya hivi
karibuni.
“Mwezi Januari mwaka huu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alifuta tamko la Primafacie
alilolitoa mwezi Mei, 2015 ambalo linataka wakimbizi wanaokimbia
machafuko nchini kwao waruhusiwe kuingia kwa makundi bila ya
utambuzi,”alieleza Bwana Mseke.
Alibainisha kuwa, bila ya tamko
hilo “Kwa wastani wa wakimbizi 1000 kwa siku kuanzia Januari, 2017,
tungekuwa tunapokea wastani wa wakimbizi 30,000 kwa mwezi na hadi
kufikia sasa tungekuwa tumepokea wakimbizi wapatao 240,000”.
Aliongeza kuwa hatua hiyo ya
Waziri kufuta tamko hilo ilizingatia hali halisi ya utulivu na usalama
nchini Burundi ambapo ilikuwa imetengamaa na maisha yamerejea katika
hali ya kawaida.
Mkurugenzi huyo wa Huduma za
Wakimbizi alieleza kuwa raia wa Burundi ambao walikuwa wakiingia nchini
mwaka jana wengi walikuwa wakikimbia hali ya upungufu wa chakula nchini
humo tatizo ambalo lilizikumba pia baadhi ya nchi nyingine katika ukanda
huu.
Wakati akitoa wito huo, Rais
Magufuli aliiagiza pia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kusitisha mara
moja kuwapatia uraia wakimbizi raia wa Burundi.
Bwana Mseke alibainisha kuwa
serikali tangu Awamu ya Kwanza imekuwa ikiwapatia uraia wakimbizi
kutokana na hali halisi ambapo mwaka 1983 wakimbizi 32,000 raia wa
Rwanda walipewa uraia. Kati ya mwaka 1995 na 2012 wakimbizi wa kisomali
wenye asili ya kibantu 3,000 walipewa uraia na mwaka 2014 wakimbizi raia
wa Burundi 162,156 walipewa uraia.
Agizo hilo la Rais la kusitisha
utoaji uraia kwa wakimbizi linatarajiwa kusaidia kupunguza idadi ya
wakimbizi nchini kwa kuwa imeibainika baadhi yao huja nchini kwa nia ya
kujipatia uraia.
No comments :
Post a Comment