Thursday, August 3, 2017

UNICEF KUBORESHA MASUALA YA WATOTO HAPA NCHINI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira  na Watu Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akiwa kwenye mazungumzo na Mwakilishi Mkazi UNICEF Tanzania Bi. Maniza Zaman, (kushoto), Ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Agosti 3, 2017. Mazungumzo hayo yalijikita katika uboreshaji wa huduma za watoto nchini.


NA OWM, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Mb) Jenista Mhagama akutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa UNICEF Tanzania Ms. Maniza Zaman Ofisini kwake na kuzungumzia masuala mtambuka juu ya kuboresha huduma za watoto Jijini Dar es Salaam Agosti 3, 2017.
Waziri Jenista pamoja na masuala mengine amelishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa (UNICEF) kwa kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Tano katika utekelezaji wa Programu ya Kitaifa ya Masuala ya Kijamii (National Frame -work Social Protection) na mapitio ya utengenezaji wa Sera ya Hifadhi ya Jamii (Social Security Policy) na kueleza kuwa Serikali imeguswa na jitihada za UNICEF kwa kuunga mkono jitihada za serikali katika Nyanja hii.
Ms. Maniza amesema “UNICEF ina mipango mbalimbali inayotaka kutekeleza kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania mipango hiyo ni pamoja na kuboresha masuala ya Elimu kwa watoto, Masuala ya Lishe, Watu Wenye Ulemavu, UKIMWI kwani huduma hizi ni za msingi  hivyo UNICEF itaangalia namna ya kutekeleza mipango hii kwa Tanzania”.
“Tumeweza kuandaa makongamano na majukwaa ya wahariri kutoa elimu kupitia Vyombo vya Habari, Viongozi wa Dini kuhusu masuala ya watoto nchini Uganda na Brazil ambayo imefanikiwa kwa asilimia 80 hivyo tunaamini Tanzania pia inaweza kuanzisha majukwaa kama hayo katika kuboresha masuala ya watoto hapa nchi kwa kushirikiana na UNICEF” alisisitiza Ms. Maniza.
Jenista amemuahidi Mwakilishi Mkazi Ms. Maniza kuandaa mazungumzo ya pamoja kwa kushirikiana na Wizara na sekta nyingine ili kuweza kuzungumzia masuala ya watoto na masuala mengine mtambuka kwa ajili ya kuleta mabadiliko na kuboresha masuala ya watoto hapa nchini.

No comments :

Post a Comment