WANANCHI 365 wa kijiji cha Chongoleani watafidiwa
shilingi bilioni 3,035 kwa ajili ya kutoa
maeneo yao, ili kupisha ujenzi wa bomba la mafuta linalojengwa kutoka Hoima
nchini Uganda mpaka Tanga.
Hayo yamesemwa
na Meneja Mawasiliano wa Shirika la Usimamizi wa Bandari Tanzania TPATanga,
Bibi Janeth Rwuzangi katika mahojiano maalum na Idara ya Habari (MAELEZO) leo.
Bi Ruzangi amesema
kuwa kwa hapa Chongoleani mradi una
ukubwa wa hekta 200 zikiwemo hekta 100 zitakazotumiwa kuweka miundombinu ya
mafuta ghafi. Hekta 100 zilizosalia zitatumika kwa ajili ya shughuli za TPA)
kuwekeza miundombinu ya kupokea mafuta yaliyosafishwa. Vile vile eneo hili
limezingatia maendeleo endelevu ya biashara ya mafuta na gesi katika siku
zijazo.
Aliongeza kuwa
TPA itakuwa na wajibu wa kuhudumia meli, kuhakikisha usalama wa bidhaa, vyombo
na watu pamoja na kusimamia masuala ya afya bandarini. Aidha, Majukumu la TPA yanatarijiwakujikita katika shughuli za
uendeshaji wa majini ikiwemo kuwa na vyombo na boti maalumu kwa ajili ya
kuongozea meli wakati wa kuingia na kutoka kwenye gati la mafuta ghafi.
Akitoa ufafanuzi,
Bi Ruzangi amesema vile vile, TPA ina jukumu la kuhakikisha inahudumia shehena
ya vifaa vyote vya ujenzi katika Bandari ya Tanga kwa kushirikiana na Bandari
Kuu ya Dar es Salaam. Shughuli nyingine ni pamoja na ulinzi wa miundombinu ya
majini pamoja na usalama wa eneo la Bandari ambalo limegawanyika katika sehemu
kuu mbili; ardhini kwenye gati la mafuta na majini kwenye lango la kuingilia
meli na nangani.
Kwa upande wa
ajira za TPA Ruzangi amesemawafanyakazi ambao wataajiriwa ni pamoja na
mabaharia, wahandisi, mafundi, wahasibu, wachumi, watakwimu, vibarua mbalimbali
kwa ajili ya nguvu kazi n.k. Sehemu ya wafanyakazi hawa watatokana na waliopo
sasa kwenye Bandari watakaopangiwa kazi hizo. Hata hivyo TPA inatarajia kuajiri
wengine ambao watalazimika kufanya kazi hizo kulingana na taratibu za ajira za
TPA.
Pamoja na kuwa
na bomba la mafuta, kijiji cha Chongoleani
kitafaidika na ujenzi wa barabara ya kilometa 8 itakayounganisha bandari na barabara
kuu ya Horohoro – Tanga, ambapo kwa kiasi kikubwa itainua uchumi wa wananchi
wanaoishi maeneo hayo kusafirisha mazao, samaki na bidhaa nyingine kwa urahisi.
Akifafanua uwekaji
wa jiwe la msingi Ruzangi amesemakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt, John Pombe Magufuli na Mgeni wake Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni
wanatarajia kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Bomba la Mafuta tarehe 05 Agosti
2017.
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Chongoleani, Bw.
Mbwana Nondo amesema; “Kwa
moyo wa dhati kabisa, naomba nimshukuru sana sana Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kwa kutujali wananchi wake na kutuletea
neema ya Mradi wa Bomba la Mafuta, katika maisha yetu wanachongoleani,
hatutaweza kumsahau kwa kizazi hiki kinachoshuhudia mradi huu na vizazi
vijavyo”.
Nondo
alisema kuwa anamuhakikishia Mhe. Rais kuwa kuwa wote watakaopata fursa kwenye mradi wa
Bomba la Mafuta, watafanyakazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo ya mtu mmoja
mmoja na Taifa kwa ujumla.
Bomba
la Mafuta la kutoka Hoima Uganda mpaka Tanga Chongoleani lina urefu wa Kilometa
1445 ambapo kwa upande wa Tanzania itakuwa na jumla ya kilometa 1115 na
Uganda 330. Aidha, Mradi utatarajia
kusafirisha mapipa laki mbili na kumi na sita
elfu (216,000) kwa siku .
Kijiji cha
Chongoleani ndio kituo cha mwisho ambapo mitambo mikubwa itasimikwa katika eneo
hili kwa ajili ya kusukuma mafuta eneo la baharini ili, kuweka kwenye vyombo vya usafirishaji
kusafirisha maeneo mbalimbali duniani ambayo Uganda watakuwa wamepata soko.
Tanzania
itafaidika na mradi huu kutokana na kodi, tozo na mrahaba wa bomba la mafuta, itakayofanywa moja kwa
moja na mradi huo. Faida nyingine ambazo, sio za moja kwa moja ni ajira, fursa za kufanya biashara na uwezekano
wa mikoa 8 ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma,
Morogoro na Tanga.
No comments :
Post a Comment