Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimpokea Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe.
Yoweri Kaguta Museveni katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu JK
Nyerere Dar es Salaam tayari kuelekea jijini Tanga kwa Sherehe za Uwekaji wa
Jiwe la Msingi la Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi toka Hoima Uganda hadi Tanga
Tanzania utakaofanyika tarehe 5 Agosti 2017 katika eneo la Chongoleani.
Wakati huo huo, Agness Moshi wa MAELEZO anaripoti katika makala hii kuwa, takribani
mwaka mmoja sasa tangu taarifa za kujengwa kwa Mradi wa Bomba la Mafuta
litakaloanzia Hoima Nchini Uganda mpaka Tanzania kwenye
bandari ya Tanga kuenea kwenye vyombo vya habari ,mitandao ya kijamii na kwa
wakazi wa Mkoa wa Tanga ambao ndio wahusika wakuu kwenye mradi huu japo
unajengwa kwa manufaa ya mataifa haya mawili kwa ujumla.
Mradi huu ni
moja kati ya miradi mikubwa ambayo Nchi imeweza kutekeleza na utagharimu kiasi
cha dola za Kimarekani Billioni 3.5 ambazo ni sawa na Tsh Trillioni 8 kwa fedha
za kitanzania. Bomba hili linategemewa kuwa na urefu wa kilometa 1,445 likiwa
na uwezo wa kusafirisha mapipa ya mafuta takribani 2,016,000 kwa siku na kutoa
ajira zaidi ya 1,000 na vibarua zaidi ya 30,000.
Taarifa hizo
zilianza kuwa rasmi, mnamo tarehe 14 marchi 2016 ambapo Makamu wa Rais wa
kampuni ya Total Afrika Mashariki Bw.Javier Rielo alimhakikishia Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kuanza kwa ujenzi wa
Mradi huo.
Nyota njema
ya Mradi huu ilianza kuonekana Aprili 24 ya mwaka jana, baada ya aliyekua
Waziri wa Nishati na Madini Prof.Sospeter Muhongo kurejea Nchini kutoka Uganda,
kuongea na waandishi wa habari kuhusu makubaliano yaliyofikiwa kwa mradi huo.
Bwana Muhongo
alisema kuwa, kulikua na mjadala mkubwa wa kuchagua wapi Mradi huo ujengwe na
wapinzani wakubwa kwa Tanzania walikua Kenya lakini kutokana na ubora wa
bandari ya Tanga ukilinganisha na bandari nyingine Tanzania ilichaguliwa
kunufaika na mradi huu.
“Bandari ya
Tanga ni bora kwa sababu ina kina kirefu ambacho ni zaidi ya mita 23 ambayo
ndicho kinayotakiwa Kimataifa kwasababu hiyo kinaweza kufanya kazi mwaka
mzima”, alisema Prof. Muhongo.
Chagizo la
kuanza kwa mradi huu lilipamba moto Marchi 28 mwaka huu, baada ya
Rais Magufuli kukutana na Mawaziri wa Nishati na Madini wa Serikali zote mbili
katika Ukumbi wa Baraza la Mawaziri Ikulu, Jijini Dar es Salaam ili kujadili
Maendeleo ya Mradi huo.
Wahenga
walisema “Hata Mbuyu ulianza kama Mchicha” wakiwa na maana kila kitu kikubwa
kilianza kikiwa kidogo vivyo hivyo Mradi huu ulianza kwa ahadi, makubaliano na
hatimaye utekelezaji.
Mei
21 mwaka huu, Rais
Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni walitia rasmi
saini ya tamko la pamoja ili kukamilisha majadiliano ya vipengele vya mkataba
wa utekelezaji wa mradi huo.
Wakazi wa
Mkoa wa Tanga, wanahesabu miezi miwili tangu kusainiwa rasmi kwa
mkataba wa mradi huo utakaowapeleka kwenye mafanikio mbalimbali ikiwemo fursa
za ajira , ukuaji wa kasi wa maendeleo , na kuurudishia umaarufu uliopotea wa
mji huo.
Ikumbukwe
Mkoa huo, ulikua maarufu miaka ya 1960 na 1970 kutokana uwepo wa
viwanda mbalimbali ikiwemo vya uzalishaji katani ambalo ni zao kuu la biashara
mkoani humo .Lakini umaarufu huo ulipotea baada ya viwanda hivyo kushindwa
kuendelea kuzalisha bidhaa za kutosha kama vile kiwanda cha saruji Tanga.
Licha ya mji
huu kupoteza umaarufu bado ni kivutio kikubwa cha Utalii kwani kuna Mapango ya
Amboni ambayo yamekua yakiupamba mji huo wenye kilomita za mraba 27,348 na
Wilaya 10 ambazo ni Handeni Vijijini, Handeni Mjini, Kilindi, Korogwe Vijijini,
Korogwe Mjini, Lushoto, Mkinga, Muheza, Pangani na Tanga Mjini pamoja na
majimbo 11 ya uchaguzi ambayo ni Tanga Mjini, Pangani, Handeni, Korogwe Mjini,
Korogwe Vijijini, Lushoto, Bumbuli, Mlalo, Kilindi Mkinga na Muheza.
Miaka , na
miezi ilipita hatimaye, Mkoa huo umefufua umaarufu wake kupitia Kata ya
Chongoleani inayopatikana katika moja ya Wilaya mkoani humo,
yenye wakazi wapatao 4,737 , kwa mujibu wa sensa iliyofanyika
mwaka 2012 ,ambao pia karibu nusu ya wakazi wake ni wanufaika wa huduma ya
umeme tangu mwaka 2015 kufuatia mpango wa serikali wa usambazaji umeme
vijijini.
Agosti
5 mwaka huu (kesho), Tanga inatarajia kurudisha sifa na umaarufu uliopotea kwa
zaidi ya miaka takribani 60 kufuatia shughuli za uwekwaji wa jiwe la
msingi la Mradi itakayofanywa na Rais Magufuli na Museveni ambao
utapelekea Nchi zote mbili kwenye mapinduzi ya kiuchumi kwa Nchi na
wakazi wa Mkoa huo kupitia fursa mbalimbali hususani kwenye upatikanaji
wa Ajira, biashara, chakula ,malazi, bima na huduma za kifedha.
Kwa Upande
wake, Mkurugenzi Wa Mawasialiano Ikulu Bw.Gerson Msigwa ametoa wito kwa
Watanzania wanaoishi mbali na Mkoa huo kufuatilia matangazo na
machapisho mbalimbali yanayotolewa ili kupata taarifa kuhusiana na shughuli
hiyo na kwa upande wa wakazi wa Mkoa huo amewasihi kuhudhuria ili waweze kushuhudia
tukio hilo la kihistoria.
Ifike wakati
Watanzania tujivunie na tumpongeze Rais Magufuli kwa juhudi anazozifanya
ili kuinua kipato kwa Wananchi kuanzia ngazi ya chini kwa
kutengeneza fursa mbalimbali za ajira, miundo mbinu ili kurahisha shughuli za
biashara na Afya kwa ujumla badala ya kushabikia mambo yasiyo na tija kwa
maendeleo.
Kwa wakazi
Mkoa Tanga, Serikali imetekeleza ahadi iliyotolewa hivyo basi ni wajibu wao
kuunga mkono Mradi huu kwa kutoa ushirikiano hususani katika kufanya kazi kwa
bidii, kulinda ili kuzuia uharibifu au kukwamisha shughuli hizo kwa namna
yoyote.
Rais Museveni akipokewa na Mkuu, Mh.Kassim Màjaliwa alipowasili kwenye uwanja Wa ndege jijini Tanga jioni hii ya Agosti 4, 2017. |
No comments :
Post a Comment