Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub
Mohamed Mahmoud akikagua madarasa ya skuli ya msingi Jang’ombe ‘B’
yaliyofanyiwa ukarabati na kampuni ya Bima Jubilee ikiwa ni sherehe ya
kutimiza miaka 80 tokea kuanzishwa. Kulia, ni Mwalim Mkuu wa skuli hiyo
Bi. Salila Adam Sadik.
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub
Mohamed Mahmoud akikata utepe kuashiria uzinduzi wa madarasa sita
yaliyofanyiwa ukarabati na kampuni ya Jubilee katika skuli ya Jang’ombe
‘B’. Wa kwanza kushoto ni Kamishna wa mamlaka ya usimamizi wa Bima
Zanzibar Mohammed Ameir, akifuatiwa na Meneja wa Bima Jubilee Zanzibar
Abdulrauf Suleiman pamoja na Mwenyekiti wa kamati ya skuli ya Jang’ombe
‘B’ Taifani Vuai Makame.
Meneja wa Kampuni ya Bima Jubilee
Zanzibar Abdulrauf Suleiman (katikati) katika picha maalum na Mkuu wa
Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud pamoja na Mwalimu Mkuu wa
Skuli ya Jang’ombe ‘B’ Bi. Salila Adam Sadik.
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub
Mohamed Mahmoud akimtunuku cheti Meneja wa kampuni ya Bima Jubilee
Zanzibar Abdulrauf Suleiman kwa kuthamini mchango wake wa kampeni ya
mimi na wewe katika hafla iliyofanyika skuli ya msingi Jang’ombe mjini
Zanzibar.
Picha na Makame Mshenga.
……………………….
Na Miza Kona-MAELEZO ZANZIBAR
Mkuu wa Mkoa Mjini magharibi Ayoub
Mohamed Mahmoud, ameitaka Wizara ya Elimu na ...
Mafunzo ya Amali kuweka
mpango maalum wa kuyafanyia matengenezo madarasa na madawati pale
yanapoharika ili kuepusha hasara.
Ameyasema hayo huko Skuli ya
Msingi Jang’ombe katika hafla ya Uzinduzi wa Madarasa sita yaliyofanyiwa
matengenezo na Kampuni ya Bima ya Jubilee katika kusheherekea miaka 80
tangu kuanzishwa kwake.
Alisema mpango huo mbadala
utasaidia kupunguza gharama za matengenezo na kuweka majengo katika
mazingira mazuri yatayomwezesha mwanafunzi kusoma katika hali ya
kuridhisha.
Alisema kuwepo utaratibu wa
kuwatoza fidia kwa mwanafunzi au raia yeyote atakaharibu kitu ili kuweza
kudhibiti majengo na vifaa vya skuli na kuiepushia serikali hasara ya
kuyafanyia matengenezo kwa gharama kubwa.
Alieleza kuwa serikali inachukua
jitihada ili kuhakikisha skuli zote zake zote zinapatiwa madawati
ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
“Tatizo la madawati katika skuli litafikia ukomo wake mwishoni mwa mwaka huu,” alifahamisha Mhe. Ayoub.
Mkuu huyo wa Mkoa amewaomba wazazi
na walezi kujiunga na bima ya elimu kwa ajili ya watoto wao ili
kuwekeza katika elimu na kuwajengea mazingira mazuri ya maisha yao ya
baadae.
Aidha alieleza kuwa kuna
changamoto nyingi katika jamii hasa kwenye sekta ya elimu na afya, hivyo
jamii inatakiwa kushirikiana ili kuzipatia ufumbuzi wa pamoja kasoro
zinazojitokeza.
Ayoub pia ameipongeza kampuni ya
Bima ya Jubilee kwa mchango wake huo wa kiunga mkono serikali katika
sekta ya elimu na kuwataka wadau wengine kutoa michango yao katika
huduma za kijamii ili kuleta maendeleo nchini.
Alikabidhi cheti kampuni hiyo kwa
kuwa mdau mkuu wa kutoa mchango katika huduma za jamii na kuunga mkono
kampeni ya Mimi na Wewe.
Akisoma risala, Meneja wa kampuni
ya Bima Jubilee Zanzibar Abdulrauf Suleiman alisema kampuni yake
imejitolea kukarabati madarasa sita katika sehemu zilizobomoka, sakafu
pamoja na kuta, kuweka madirisha, milango na kupaka rangi ndani na nje
ili kuwaondoshea watoto kero zinazowakabili na kujali afya zao wakati
wa masomo.
Aidha ameitaka jamii kuzitunza
mali za serikali kwa kuzingatia kwamba skuli ni mali ya jamii hivyo ni
wajibu kuzienzi na kuzilinda ili ziweze kunufaisha vizazi vya sasa na
vijavyo.
Mapema akimkaribisha mgeni rasmi,
Mwenyekiti wa Kamati ya skuli ya Jang’ombe Taifani Vuai Makame, alisema
tatizo kubwa la skuli hiyo ni kuvuja kwa paa lake wakati wa mvua, hali
inayofanya wanafunzi wasiweze kuendelea na masomo.
No comments :
Post a Comment