NA BENNY MWAIPAJA, WFM-ARUSHA
WAKAZI wa Jiji la Arusha wameondokana na
na adha ya umeme kukatika mara kwa mara baada ya kukamilika kwa mradi wa
umeme katika Kituo cha kupoozea umeme cha Njiro kilichoko Mkoani Arusha chenye
uwezo wa kuzalisha megawati 130.
Hali hiyo inatokana na Benki ya Maendeleo ya
Afrika-AfDB kuwekeza kiasi cha Dola milioni 4.2, ukiwa ni mkopo wenye masharti
nafuu kwa ajili kuongeza uwezo wa Kituo hicho kuzalisha umeme unaotumika kwa
ajili ya makazi ya watu, maeneo ya biashara na viwanda.
Msimamizi Mkuu wa Kituo cha Usambazaji umeme cha Njiro
Mhandisi Lembrice Mollel amesema mradi huo umesaidia kuongeza
Megawati 130 za umeme ambao umekidhi mahitaji ya Jiji la Arusha linalo hitaji
Megawati 60 hivyo kubakiwa na Umeme wa ziada kiasi cha Megawati 70.
Alisema kuwa tatizo la kukatika katika kwa umeme
katika mji huo wa kitalii na kibiashara litakuwa historia na kwamba umeme
unaozalishwa kituoni hapo unasafirishwa kwenye maeneo mengine yenye uhitaji
ikiwemo mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.
Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa Umeme wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB) Mhandisi Frorence Gwang’ombe amesema kuwa lengo la
mradi lilikuwa kupatikana kwa umeme wa uhakika na kuimarisha miundombinu ya
usambazaji na kupooza umeme jambo ambalo limefikiwa kikamilifu.
Alisema kuwa uboreshaji wa Kituo hicho cha kupoozea
Umeme cha Njiro ni sehemu ya utekelezaji wa uboreshaji wa Sekta ya Umeme nchini
kupitia mradi ujulikana kama Electricity V, uliofadhiliwa na AfDB
kupitia mkopo nafuu wa kiasi cha Dola milioni 8, ukihusisha pia mkoa wa Dar es
Salaam, Vituo vya kupooza umeme vya Sokoine na Ilala.
“Mradio huu umelenga kuwahudumia wananchi takribani
8,400 hivyo kukamilika kwa mradi huo ni neema kwa wananchi wengi kwa kuwa
utasaidia kuimarisha uwezo wao wa kibiashara ndani ya Jiji la Arusha na maeneo
mengine ya nchi” alisema Mhandisi Gwang’ombe
Alifafanua kuwa uboreshaji wa mradi wa Kituo cha
Kupooza Umeme cha Njiro umehusisha ufungaji wa transfoma mpya 2 zenye uwezo wa
kufua megawati 50 kila moja na nyingine 2 zenye uwezo wa kubeba megawati 15
kila moja, hatua iliyosaidia kuongeza kiwango hicho cha umeme.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB), anayehudumia Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro,
ameelezea kuridhishwa na utekelezaji pamoja na manufaa ya mradi huo
utakaosaidia kukuza biashara na kusisimua uwekezaji wa viwanda katika mkoa wa
Arusha.
‘Arusha ni mji wa Kitalii hivyo unahitaji kuwa na
umeme wa kutosha utakaosaidia katika uwekezaji na ufanisi wa biashara,
upatikanaji wa umeme wa uhakika utachochea shughuli za Kilimo na viwanda kwa
kasi kubwa’, aliongeza Dkt. Weggoro.
Amewataka wakazi Arusha na Watanzania kwa ujumla
kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotokana na kuboreshwa kwa miundombinu ya
umeme ili kwenda sambamba na Sera ya Serikali ya kufikia uchumi wa kati ifikapo
mwaka 2025.
Baadhi ya wakazi wa Mji wa Arusha, wakiwemo Bw.
Jackson William na Bw. Steven Chitara wamekiri kuwa maisha yao yamebadilika
kiuchumi kutokana na kuimarika kwa upatikanaji wa umeme ikilinganishwa na hapo
awali.
Wamesema kuwa vijana wengi wamejiajiri kupitia
shughuli mbalimbali za uzalishaji mali zinazotegemea uwepo wa nishati hiyo kama
kuchomelea vyuma, vinyozi, ufundi wa aina mbalimbali pamoja na wafanyabiashara
wakubwa kuanza kuvutiwa kuwekeza mkoani humo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB), Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt Nyamajeje Weggoro (kushoto) na Mshauri
wake Amos Cheptoo wakionesha kufurahishwa na ufanisi wa mradi wa
kusambaza umeme wa Njiro Jijini Arusha baada ya kukagua na kujiridhisha
na thamani ya mradi huo uliofadhiliwa na Benki yake kwa gharama Dola milioni
4.2. (PICHA NA WFM)
Msimamizi Mkuu wa Kituo cha Kupoozea Umeme cha Njiro
Mkoani Arusha, Mhandisi Lembrice Mollel, akitoa maelezo kuhusu mitambo ya Kituo
hicho kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kanda ya
Afrika Mashariki, Dkt Nyamajeje Weggoro (kulia) alipotembelea Kituo hicho
kukagua mradi wa kusambaza umeme uliofadhiliwa na AfDB, uliogharimu Dola
milioni 4.2, Jijini Arusha
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB), Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt Nyamajeje Weggoro (wa pili kulia)
akipewa maelekezo ya namna mitambo ya usambazaji umeme katika Kituo cha Njiro
Jijini Arusha inavyoendeshwa kwa mfumo wa Kidigitali. Mitambo hiyo imefadhiliwa
na Benki ya AfDB ukiwa ni mkopo wenye masharti nafuu.
Muonekano wa mitambo iliyofadhiliwa na Benki ya
Maedeleo ya Afrika (AfDB), katika kituo cha kusambaza umeme cha Njiro, Mkoani
Arusha. Mitambo hiyo imesaidia kupatikana kwa umeme wa ziada wa Megawati 70.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro (kushoto) akipata maelekezo kutoka kwa wataalamu wa Kituo cha Kupoozea Umeme cha Njiro, Mkoani Arusha, kuhusu usalama wa mitambo kutakapo tokea dharula. Mitambo hiyo imefadhiliwa na Benki ya AfDB, ikiwa ni mkopo wenye masharti nafuu.
No comments :
Post a Comment