WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekabidhi pikipiki 49 kwa vijana wa wilaya ya Ruangwa ili waweze kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.
Amekabidhi pikipiki hizo leo
(Jumatano, Julai 12, 2017), baada ya kumaliza kuhutubia wananchi kwenye
uwanja wa shule ya msingi Likangara.
Baada ya kukabidhi pikipiki
hizo, Waziri Mkuu amewataka vijana hao kuhakikisha wanakuwa waaminifu
kwa kufanya kazi kwa bidii ili pikipiki hizo ziwe na tija.
Amesema vijana wanaoendesha pikipiki maarufu bodaboda wanatakiwa kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali.
“Ukiendesha pikipiki lazima
uhakikishe kwamba una leseni, bima, vaa kofia ngumu wewe na abiria wako
na marufuku kubeba abiria zaidi ya mmoja.”
Wakizungumza baada ya kukabidhiwa
pikipiki hizo vijana hao ambao walikuwa wakiendesha pikipiki za watu
ambazo hazina tija, wameahidi kufanya kazi kwa bidii.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu ametembelea mradi wa ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika
zahanati ya Nandagala na kuridhishwa maendeleo yake.
Amesema kukamilika kwa majengo
hayo kutarahisisha upatikanaji wa haraka wa huduma za afya kwa mama na
mtoto. Pia itawapunguzia kutembea umbali mrefu kwenda kufuata huduma
hizo katika hospitali ya wilaya ya Ruangwa.
No comments :
Post a Comment