Monday, July 3, 2017

Watafiti wa Afya Waaswa Kutofungia Tafiti zao ‘Kabatini’

unnamed
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa Tano wa Sayansi ya Afya waChuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) Dk. Irene Kida akitoa majumuisho ya Mkutano huo mbele ya Mkurugenzi wa Elimu ya juu, Wizara ya Elimu, Sayansi, teknolojia na mafunzo ya Ufundi, Profesa Sylvia Temu (wa tatu kushoto meza kuu) wakati wa hafla fupi ya kuhitimisha mkutano huo uliofanyika kwa mwishoni mwa wiki  jijini Dar es Salaam. Wengine ni pamoja na walimu na uongozi wa chuo hicho akiwemo Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa ( wa pili kushoto)
1
Mkurugenzi wa Elimu ya juu, Wizara ya Elimu, Sayansi, teknolojia na mafunzo ya Ufundi, Profesa Sylvia Temu (wa pili kushoto) akisikiliza maelezo kuhusiana na dawa za asili zinazoandaliwa na kitengo cha tiba asili katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) alipotembelea maonyesho ya shughuli zinazofanywa na MUHAS mara
baada ya kuhitimisha Mkutano wa tano wa kisayansi ulioandaliwa na chuo hicho jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita. Wanaoshuhudia ni pamoja na viongozi wa Chuo hicho akiwemo  na Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa (kushoto)
…………………………
Na Mwandishi wetu,
SERIKALI imetoa wito kwa taasisi za elimu ya afya na mashirika mbalimbali yanayofanya tafiti za afya hapa nchini kuhakikisha tafiti hizo zinafika kwa wadau na wananchi kwa ujumla ili zilete tija zaidi kwa jamii badala ya kuzifungia kwenye ofisi zao.
Wito huo wa serikali ulitolewa mwisho wa wiki jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Elimu ya juu, Wizara ya Elimu, Sayansi, teknolojia na mafunzo ya Ufundi, Profesa Sylvia Temu alipomuwakilisha Katibu Mkuu Wizara hiyo, Dk. Leonard Akwilapo kwenye hafla ya kuhitimisha Mkutano wa tano wa kisayansi ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS).
“Kwa sasa tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda na miongoni mwa sekta muhimu ambazo pia zinatarajia wawekezaji ni pamoja na sekta ya afya hivyo basi muelekeo na mapendekezo ya tafiti za afya ndio zitakazoweza kuwasaidia wadau na serikali kufahamu aina ya ukwekezaji huo pamoja na maeneo gani yanafaa kulingana na mahitaji. Tafiti hizi zikifungiwa kwenye makabati tafsiri yake ni kwamba hata hii mikutano itakosa tija pia.’’ alisisitiza.
Aliongeza kuwa Serikali kwa kiasi kikubwa inajitahidi kutumia tafiti hizo katika kuandaa sera mbalimbali zinazohusiana na masuala ya afya huku akitoa pongezi kwa uongozi wa chuo hicho kwa kuendelea kuandaa wataalamu wanaoandaa tafiti hizo kwa weledi na ufanisi mkubwa.
“Zaidi umuhimu wa mkutano huu ni pale unapowakutanisha wataalamu wa afya tena katika ngazi tofauti wakiwemo wale waliobobea pamoja na wanafunzi na hivyo kuwa kama jukwaa kwa wao kuweza kubadilishana ujuzi. Jumla ya tafiti 160 tofauti za afya zimewasilishwa kupitia mkutano huu ambapo tafiti 70 kati ya hizo zilijadiliwa kwa kina na wataalamu hawa,’’ aliongeza.
Awali, akizungumza kwenye hafla hiyo Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa alisema nyingi kati ya tafiti zilizowasilishwa kwenye mkutano huo wa siku mbili zilijikita katika vipaumbele vya taifa yakiwemo masuala ya HIV/AIDS, kifua kikuu, afya ya uzazi na mtoto, magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ajali pamoja na magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika.
“Ndio maana tunaishukuru sana serikali ya Sweden kupitia Shirika la Sida ambao kwa kushirikiana na wadau wengine wamewezesha mkutano huu muhimu.,’’ alisema Prof Kamuhabwa huku akibainisha kuwa chuo hicho kimejipanga kuhakikisha tafiti hizo zinawafikia walengwa ikiwemo Serikali, mashirika na taasisi mbalimbali pamoja na wananchi kwa ujumla.

No comments :

Post a Comment