Na: Agness Moshi – MAELEZO.
Ulaji wa nyama una faida lukuki
kwa afya ya binadamu ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa virutubisho vya
aina ya protini ambayo ni rahisi kutumika mwilini, madini mbalimbali
(Calcium, Magnesium, Phosphorus, Zinc na Chuma); vitamini aina ya folic
asidi, E, B na B12 ...
ambayo inapatikana katika nyama pekee.
Nyama pia inasaidia katika ukuaji
na kuongeza afya ya mlaji kutokana na uwezo mkubwa wa kujenga mwili,
kukarabati seli za mwili zilizokufa, kuzalisha chembe hai mpya,
kurekebisha kinga ya mwili, kuongeza damu na kuimarisha mifupa.
Hata hivyo faida zote hizo
zinapatikana tu, kwa walaji wa nyama iliyo bora na yenye kiwango. Hivyo
ni vizuri wananchi wakazingatia kanuni za ulaji wa nyama yenye kiwango
ili kujiepusha na athari zinazoletwa na nyama isiyo na kiwango.
Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania
(TMB) Bi.Suzana Kiango amesema kuwa nyama yenye kiwango na bora huanzia
kwenye utunzwaji wa mifugo wenye kuzingatia kanuni za uzalishaji bora,
unenepeshaji wa mifugo yenye umri mdogo kwa kuwalisha chakula
mchanganyiko kwa muda usiopungua siku 90 kabla ya kuchinja.
Bi.Kiango amesema kuwa hatua
nyingine ni katika uchinjaji ambapo inashauriwa ufanyike kwenye
machinjio bora ambayo yanakidhi viwango vya usafi. Hii ni pamoja na kuwa
na sakafu na kuta zinazosafishika, maji ya kutosha na sehemu za
kuning’iniza wakati wa kuchuna na kupasua.
“Kanuni za uchinjaji ni pamoja na
kupumzisha mifugo ili kuipoteza fahamu na kumfanya mnyama asiogope na
kuzalisha asidi nyingi inayosababisha nyama kuwa ngumu, pia iwe rahisi
kutoa damu yote katika misuli. Uning’inizwaji wa chune mara baada ya
kuchinjwa unasaidia kuondoa damu iliyo mwilini. Endapo damu haitatoka
yote kwenye chune itasababisha nyama kuwa na rangi nyeusi na kuharibika
mapema”, alisema Bi.Kiango.
Madhara ya ulaji wa nyama
isiyo na viwango na bora ni pamoja na kupata magonjwa ya tumbo,
kuharisha na kutapika endapo nyama itapata vimelea vya magonjwa hayo,
kuugua magonjwa ya kuvimba miguu, kifua kikuu, shinikizo la damu,
kisukari na kansa.
Hata hivyo, Bi. Kiango
amesisitiza kuwa magonjwa haya yanaweza kuwatokea pia watu ambao
hawatumii kabisa nyama kwa hivyo si nyama pekee ndio chanzo cha magonjwa
haya japo inaweza kuwa sababu ya mtu kuugua.
“Bodi imeendelea kutoa elimu kwa
watumiaji na wachinjaji wa nyama kupitia vyombo mbalimbali vya habari
kama vile, redio, televisheni na magazeti. Pia katika maonesho
mbalimbali kama Saba saba na Nane nane ambapo wataalamu wa bodi hutoa
elimu kwa wananchi wanaotembelea mabanda ikiwa ni pamoja na kusambaza
vipeperushi” amesema Bi.Kiango.
Namna nyingine ya kutoa elimu ni
pamoja na kutumia matamasha ya nyama choma, wiki ya mayai na maonesho ya
kuku, wiki ya chakula salama na siku ya chakula duniani. Wakati wa
shughuli hizi wanashiriki hupatiwa elimu kuhusu faida na athari za kula
nyama isiyo na viwango ili kunusuru afya zao.
Aidha walaji huelekezwa maeneo
mbalimbali wanayoweza kupata nyama hiyo, na kwa upande wa
wafanyabiashara wa nyama hupewa maelekezo ya kuboresha miundombinu ya
kuzalisha, kuchinja na kuuza kwa kuzingatia viwango vya ubora na
usalama.
Kutokana na baadhi ya
wafanyabiashara ya nyama kuendelea kuwauzia walaji nyama isiyo na
viwango kwa kujua au kutojua madhara ya nyama hizo, Bi.Kiango alisema
kuwa Bodi inachukua hatua za kuhakikisha wafanyabiashara hao wanapata
uelewa wa kutosha.
“Bodi imeanza kutoa mafunzo
kwa watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao watashiriki katika
kutekeleza majukumu ya Bodi ikiwa ni pamoja na kusimamia uzalishaji wa
nyama na kuelimisha wachinjaji ,walaji na wadau wengine
wanaojishughulisha na uzalishaji wa nyama”alifafanua Bi.Kiango.
Aliendelea kusema mafunzo hayo
yameshatolewa kwa vitendo kwa watumishi wanne kutoka katika kila Mamlaka
za Serikali za Mitaa za mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na
Dodoma ambapo hadi sasa jumla ya wadau 490 katika maeneo tajwa
wamekwisha patiwa elimu hiyo. Pia mafunzo yanatolewa na wadau wengine
ambao ni Chuo cha nyama cha VETA, Dodoma na Kampuni ya nyama ya jijini
Arusha.
No comments :
Post a Comment