Na Benny Mwaipaja, WFM-Dodoma
Serikali imeeleza kuwa
inajitahidi kuboresha miundombinu kama vile teknolojia ya Mawasiliano,
Barabara, Ulinzi, Maji na Umeme katika maeneo ya vijijini ili kuweka
mazingira bora yatakayovutia wawekezaji kutoka sekta binafsi kuwekeza
katika sekta ya fedha ili
kupanua huduma hiyo katika maeneo ya mijini na
vijijini.
Hayo yameelezwa Bungeni mjini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji
(Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Josephine
Chagulla (CCM), aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuwapa wanawake
elimu kuhusu mikopo pamoja na kufikisha huduma za kibenki maeneo ya
vijijini ili waweze kufikiwa na huduma za kifedha.
Mhe. Josephine Chagulla ameeleza
kuwa wanawake wengi wa vijijini hawakopesheki kwa sababu benki
haziwafikii, pia hawana mafunzo maalumu ya kuwasaidia ujuzi wa namna ya
kuzifikia huduma hiyo ya kukopeshwa
Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji
alisema kuwa, elimu ya fedha inahusisha wadau mbalimbali ikiwemo
Serikali na Taasisi zake, ambapo kwa upande wa Serikali, Benki Kuu
inaratibu uanzishwaji wa taasisi ya kitaifa itakayokuwa na jukumu la
kuratibu, kuwezesha na kusimamia utoaji wa elimu ya fedha kwa jamii.
“Serikali kupitia Benki Kuu
imetoa mwongozo wa Uwakala wa Huduma za Kibenki ili kupanua wigo wa
huduma za kibenki kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi na kwa gharama
nafuu hasa katika maeneo ya vijijini”. Alisema Dkt. Kijaji.
Alisema kuwa baada ya kuunda
taasisi ya kitaifa ya Uratibu wa Elimu ya Fedha, kutakuwepo na mfumo
rasmi nchini wa utoaji wa elimu ya masuala ya fedha kwa wananchi wote
wakiwemo akina mama wa vijijini.” Alisema Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji alifafanua kuwa,
Taasisi za fedha zina utaratibu wa kutoa elimu ya fedha kwa wateja wao
wakiwemo wanawake ili kuhakikisha kwamba wateja wao wanaendesha
biashara zao kwa ufanisi.
“Serikali inatambua umuhimu wa
wananchi kupata huduma za kibenki karibu na maeneo yao, pia inatambua
umuhimu wa taasisi hizo katika kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi.”
Alieleza Dkt. Kijaji.
Aidha, Dkt. Kijaji aliongeza kuwa
Serikali inatambua benki nyingi zinaendesha shughuli zake mijini kwa
sababu ya urahisi wa upatikanaji wa miundombinu muhimu kwa ajili ya
uendeshaji wa shughuli za kibenki.
Katika swali la nyongeza Mbunge
wa Viti Maalum Mhe. Josephine Chagulla (CCM), alitaka kujua mpango
Serikali wa kufungua matawi ya benki ya Wanawake katika mikoa yote ya
Tanzania ili kuwasaidia wanawake kupata mikopo kwa urahisi.
Swali hilo lilijibiwa na Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu,
ambaye aliahidi kuwasiliana na Wizara ya Fedha na Mipango ili itimize
ahadi iliyotolewa na Rais wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete ya
kuipatia mtaji Benki ya Wanawake Tanzania ili iweze kufungua matawi nchi
nzima na kutoa mikopo yenye masharti nafuu ikilinganishwa na benki
nyingine.
No comments :
Post a Comment