Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Rais Dkt. John Maguful.
……………………………………………………………………………..
Na Emmanuel J. Shilatu
Mara baada ya kupata Uhuru wa
Tanganyika mwaka 1961 Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alitangaza
vita dhidi ya maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini.
Mwalimu Nyerere alisema wazi kuwa ili Taifa letu liendelee halina budi
kupambana dhidi ya
maadui hao.
Kwenye mapambano dhidi ya
‘ujinga’ tumeshuhudia Serikali ikijenga shule za msingi kwenye kila
kijiji na mtaa, Serikali ikijenga shule za sekondari kwenye kila kata;
Serikali ikitoa elimu bure kuanzia ngazi ya shule ya msingi mpaka
Sekondari; Serikali ikitoa mikopo ya elimu ya juu kwa wenye sifa vyuoni;
Serikali ikiboresha miundo mbinu ya maabara, maktaba na madawati;
Serikali ikihakikisha Waalimu wanakuwepo wa kutosha na wakiwahudumia kwa
kuwapatia mishahara na makazi.
Upande wa mapambano dhidi ya
umaskini Serikali imekuwa ikitoa ajira rasmi na zisizo rasmi; Serikali
inaboresha kilimo kuwa cha kibiashara na chenye tija zaidi; kujenga
viwanda; kuhimiza uwekezaji nchini; kuboresha mikataba ya madini n.k
Hata kwenye upande wa adui maradhi mapambano ya adui huyu bado ni makali Serikali ikijitahidi kumshinda.
Katika vipindi mbalimbali
tumeshuhudia Serikali ikijenga vituo vya afya, zahanati na hospital
kwenye maeneo mbalimbali nchini; kujenga hospitali ya Moyo nchini ambapo
inafanya mpaka upasuaji mkubwa wa moyo.
Tumeshuhudia Serikali ikiendelea
kununua vifaa tiba, mashine, vitanda, kupambana na maleria, kifua kikuu,
ukimwi na magonjwa mengineyo hatarishi.
Serikali imeboresha kwa kiwango kikubwa huduma ya uzazi ya Mama na Mtoto na kujivunia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Pamoja na mambo mazuri Serikali
inayoendelea kufanya kuboresha sekta ya afya nchini kulikuwa na matatizo
makuu mawili upande wa madawa. Mosi; Tatizo sugu la upatikanaji wa
madawa nchini ambapo kwenye hospitali za Serikali hazipatikani licha ya
kuwa zilikuwa zinapelekwa na mgonjwa akiandikiwa dawa anaambiwa akanunua
duka la nje la hospitali ya Watu binafsi.
Tumeona jitihada za dhahiri za
Serikali za kujenga maduka ya madawa ndani ya hospitali ambapo jukumu
hilo la ujenzi na usimamizi wamepewa MSD na sasa dawa zinapatikana ndani
ya hospitali na sio tena kuagizwa kwenda kununua maduka ya nje.
Pili; Kulikuwa na tatizo la dawa
kuuzwa kwa bei kubwa na hivyo kumfanya mtu wa hali ya chini kushindwa
kumudu gharama za ununuzi wa madawa.
Hivi karibuni Waziri wa Afya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu jijini Dar es
salaam alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Bahari ya Dawa (MSD)
amesema Serikali imesema kuwa imepunguza bei ya vifaa mbalimbali
vinavyotumika katika sekta ya afya zikiwemo bei za dawa, vitendea kazi
na vifaa tiba vya maabara vinavyonunuliwa na kusambazwa na Bohari ya
Dawa(MSD) kwa asilimia 15. Mfano sasa Serikali wamepunguza kodi kwenye
dawa mpaka asilimia 67 (67%) hali iliyopelekea kupunguza zaidi bei za
dawa nchini.
Hayo ni matokeo ya utaratibu wa
ununuzi wa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji kama Rais Dkt. John
Magufuli alivyowagiza Wizara ya Afya kufanya na sio kununua tena kwa
mawakala.
Hakika, hii ni habari njema kwa
Watanzania waliokuwa wakiteseka kwa kutumia gharama Kubwa kununua madawa
na ni habari mbaya kwa wale waliozoea ulanguzi wa bei za dawa. Hakuna
tena sababu ya kulanguliwa wala mtu kufa kwa kukosa dawa.
Sio tu kodi za kwenye madawa zimepunguzwa bali hata kodi za kubebea Wagonjwa imetolewa kabisa.
Heko ziwaendee Serikali ya Rais Magufuli kwa kuendelea kusimama na kuwa watetezi wa wanyonge nchini.
No comments :
Post a Comment